UNITED
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116539 E-mail: press@ikulu.go.tz Website: www.mawasilianoikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa walimu
wa Tanzania wanao uwezo wa kufundisha
somo la Kiingereza vizuri kama wakiwezeshwa
kwa kupatiwa vitabu vya kiada
vilivyojaribiwa, tahiniwa na kupimwa (tried and tested text
books) kwa ubora wake kama moja ya
njia muhimu za kuinua kiwango
cha elimu nchini.
Aidha, Rais Kikwete amewataka
wadau wa
elimu kushirikiana katika kubaini vitabu hivyo ambavyo
amesema kuwa kwa miaka mingi
vimethibitika kuwa bora zaidi katika kuwafundishia
watoto na wanafunzi wa Tanzania.
Rais Kikwete ameyasema hayo leo,
Jumatatu, Novemba 14, 2011,
Ikulu, Dar es Salaam wakati alipokutana na kufanya mazungumzo
na Bibi Katy Allen, mtunzi wa vitabu
vya lugha ya Kiingereza vya
Oxford.
Bibi Katy Allen alikuwa anamwelezea Rais Kikwete kuhusu
jitihada ambazo shirika lake lisilokuwa la kiserikali la Village Education Project Kilimanjaro (VEPK) limekuwa linafanya kuchapisha na kuboresha
kutunga vitabu vya kufundishia na kujifunza lugha
ya Kiingereza vya Oxford Engilish Books vilivyokuwa vinatumika kufundishia lugha hiyo nchini katika
miaka ya nyuma.
Bibi Katy Allen anasema kuwa shirika
lake linaamini kuwa kama vitabu
hivyo vikianza kutumika tena katika
shule za Tanzania, ufundishaji wa lugha ya Kiingereza
unaweza kuboreka haraka zaidi.
Vitabu hivyo vilivyokuwa vinatumika kuanzia shule za msingi
hadi shule za kati, yaani
kuanzia darasa la tatu hadi la nane,
viliacha kutumika kwenye miaka ya
1970 baada ya kufanyika mageuzi katika mfumo wa elimu nchini.
Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete na
Bibi Katy Allen wamejadili kwa undani kuhusu
ufundishaji wa somo la lugha
ya Kiingereza na jinsi gani
ufundishaji wa lugha hiyo unaweza
kuboreshwa kwa kutumia vitabu hivyo ambavyo mama huyo ameviandika upya kwa kusaidiwa
na mwomgoza wa mwalimu.
Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete amesema
kuwa ni
dhahiri walimu wa Tanzania wanaweza kufanya kazi nzuri
zaidi kama watawezeshwa na wadau mbalimbali wa elimu kwa
njia nyingi ikiwa ni pamoja
na kupatiwa vitabu bora zaidi vya kiada vya
kuongoza namna bora zaidi ya mbinu
za ufundishaji.
Wakati huo huo, Rais
Kikwete amekutana na kufanya
mazungumzo na Michio Ogimura, Makamu wa Rais
Mtendaji na Mshauri Maalum wa Kampuni ya
Sumitomo ya Japan katika nchi za Afrika
Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete amemwelezea kiongozi huyo kuhusu
fursa za uwekezaji zilizoko Tanzania hasa katika eneo
la nishati na madini.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR
ES SALAAM.
14
Novemba, 2011