DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail: press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

RAIS Jakaya Mrisho Kikwete leo (Jumatatu, Julai 28, 2008) amepokea hati za utambulisho za mabalozi watatu watakaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.

 

Mabalozi hao ni Dk. Ishaya Samaila Majanbu wa Nigeria, Japhet Isaack wa Namibia na Brahim Salem El-Mami Buseif wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Sahrawi.

 

Katika mazungumzo na Balozi Majanbu Ikulu, Dar es Salaam, mara tu baada ya kuwa amewasilisha hati zake, Rais Kikwete ameisifia Nigeria kwa mchango wake mkubwa katika kutatua migogoro katika Afrika.

 

Nigeria inaendelea kutoa mchango mkubwa katika kutafuta usuluhishi wa mgogoro wa Darfur katika Sudan, na pia ilichangia kwa kiasi kikubwa katika kumaliza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe katika nchi za Afrika Magharibi za Sierra Leone na Nigeria,” amesema Rais.

 

Rais pia amesifia mchango wa Rais wa Nigeria, Umaru Yar’Adua katika masuala mbalimbali ya kimataifa hasa kuhusiana na utetezi wa maslahi ya Bara la Afrika.

 

Rais pia amezungumzia uhusiano wa kiuchumi unaoanza kujengeka sasa kati ya Tanzania na Nigeria kutokana na mfanyabiashara mmoja wa maarufu wa Nigeria kuonyesha nia dhabiti ya kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya saruji Mtwara na Mwanza.

 

Katika mazungumzo na Balozi Issack wa Namibia, Rais amesifia uhusiano imara kabisa wa kisiasa kati ya Tanzania na Namibia na kuzitaka nchi hizo mbili kuanza kujenga uhusiano wa kiuchumi na ule wa wananchi wa nchi hizo mbili.

 

Balozi Isaack ametaka Tanzania kuisaidia Namibia katika sekta ya utalii na hasa katika kupata uzoefu wa Tanzania kuhusu jinsi ya kuwashirikisha Wanamibia wenyewe katika shughuli za utalii ambazo kwa sasa ziko mikononi mwa makampuni ya kigeni kwa kiasi kikubwa.

 

Naye Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania inahitaji kupata uzoefu wa Namibia katika sekta za uvuvi na mifugo ambako nchi hiyo imepiga hatua kubwa.

 

Tunazo karibu kiasi cha kilomita 1,000 za pwani ya bahari, na bado hatuna hata kiwanda kimoja cha kusindika samaki katika ukanda wa Pwani.  Kule kwenye ziwa, Ziwa Victoria, huko uwekezaji ni mzuri kiasi cha hata kuanza kuzuka kwa tatizo la ukosefu wa samaki wa kutosha,” amesema Rais.

 

 

Katika mazungumzo na Balozi Buseif, Rais Kikwete amesisitiza msimamo wa Tanzania wa kutaka wananchi wa Jamhuri ya Sahrawi kupata nafasi ya kupiga kura ya maoni kuamua hatma ya baadaye ya nchi hiyo inayokaliwa na Morocco.

 

Msimamo wa Tanzania haujapata kubadilika katika kuwaunga mkono wananchi wa Sahrawi kupata nafasi ya kuamua wenyewe hatma yao ya baadaye, kama wanataka kuwa huru ama wanataka kuwa sehemu ya Morocco.  Tunaunga njia ya kidemokrasia kumaliza tatizo hili. Hayo ndiyo matakwa yetu, huo ndiyo msimamo wetu,” amesema.

 

Imetolea na:

 

Kurugenzi ya Mawasilia ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

28 Julai, 2008