DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail: press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa kuchangia maendeleo ya Tanzania, mchango ambao ni pamoja na kugharamia ujenzi wa daraja kwenye Mto Malagarasi, Mkoani Kigoma.

 

Aidha, Rais Kikwete ameishukuru Jamhuri ya Korea kwa kugharamia miradi ya sekta ya afya, na hasa kukubali kuchangia katika ujenzi wa hospitali ya kisasa katika eneo la Mulogazira, nje kidogo ya Dar es Salaam.

 

Rais Kikwete ametoa shukurani hizo, Ikulu, Dar es Salaam, leo, Jumanne, Septemba 16, 2009, wakati alipozungumza na kuagana na Balozi Young Jun Kim anayemaliza muda wake katika Tanzania baada ya kuwa nchini kwa miaka mitatu.

 

“Nakushukuru sana kwa kuifanyia mengi nchi yetu. Sasa Tanzania na Korea zina uhusiano maridadi kabisa. Nakushukuru sana. Sasa tunayo kila sababu ya kushangilia…Uhusiano wetu ni mzuri sana iwe kwenye ngazi ya kisiasa ama kiuchumi,” amesema Rais Kikwete.

 

Kuhusu ujenzi wa daraja kwenye Mto Malagarasi, Rais Kikwete amesema kuwa daraja hilo litakuwa ni mnara wa kumbukumbu ya uhusiano kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea.

 

Ujenzi huo umepangwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu kwa gharama ya sh bilioni 28.6 na utarahisisha sana mawasiliano kati ya Mkoa wa Kigoma na mikoa mingine.

 

Mbali na kugharimia ujenzi wa daraja kwenye Mto Malagarasi, Jamhuri ya Korea imegharamia miradi mingine katika sekta za maji katika wilaya za Chamwino na Bariadi katika mikoa ya Dodoma na Shinyanga, na kwenye sekta ya afya ambako wanashiriki katika kuinua kiwango cha vituo vitatu vya afya kuwa hospitali za wilaya katika Mkoa wa Dar es Salaam.

 

Rais Kikwete amemtaka balozi huyo kuendelea kuwa rafiki mzuri wa Tanzania hasa kwa kuyashawishi makampuni zaidi ya Korea kuja kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.

 

“Tunataka makampuni zaidi na zaidi ya Korea kuja kuwekeza katika uchumi wa Tanzania. Uchumi huu hautakua bila uwekezaji,” amesisitiza Rais.

 

Aidha, Rais ameishukuru Korea kwa mpango wake wa kuleta wataalamu wa kujitolea kutoka Korea kuja kufanya kazi kwa muda katika sekta mbalimbali nchini. “Nashukuru, sasa tuna madaktari wengi zaidi, wahandisi wengi zaidi na walimu wengi zaidi kutoka Korea.” Kiasi cha wataalam 100 wa namna hiyo sasa wanakuja Tanzania kwa mwaka.

 

Rais pia amesema kuwa mpango wa Korea wa kujenga vituo vya ufundi stadi nchini ni jambo muhimu katika kukuza na kuboresha ujuzi wa Watanzania. Kwa sasa Korea iko katika mchakato wa kujenga vituo vya namna hiyo katika mikoa ya Lindi, Pwani, Kigoma na Manyara.

 

Imetolewa na:

 

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

 

16 Septemba, 2009