DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail: press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

Na Mwandishi Maalum

Rais Jakaya Mrisho Kikwete amerejea nyumbani leo, Alhamisi, Machi 19, 2009, akitokea London, Uingereza, ambako mwanzoni mwa wiki hii alihudhuria mkutano maalum wa maandalizi ya Mkutano wa Nchi za G-20, kuzungumzia matatizo makubwa yanayoukabili uchumi wa dunia.

Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar Es salaam, Rais Kikwete amelakiwa na viongozi mbali mbali wa Serikali wakiongozwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Rais Kikwete alikuwa miongoni mwa viongozi wanane wa Bara la Afrika walioalikwa na Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown kuwakilisha msimamo wa Afrika kama nchi za Afrika zinavyoutaka uelezwe kwenye Mkutano wa G-20, uliopangwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi ujao hapo hapo London.

Viongozi wengine wa Afrika waliohudhuria mkutano huo wa maandalizi uliofanyika Jumatatu, Machi 16, 2009, kwenye Jumba la Lancaster House chini ya uenyekiti wa Gordon Brown ni pamoja na Rais Khama Ian Khama wa Botswana, na Rais Ellen Johnson Sirleaf.

Wengine ni Waziri Mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi, Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga, Waziri wa Fedha wa Afrika Kusini Trevor Manuel, Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU) Jean Ping, na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Donald Kaberuka.

Viongozi hao kwa pamoja walimweleza Gordon Brown msimamo wa Afrika ambao wanataka uwasilishwe katika Mkutano huo wa G-20 ikiwa ni pamoja na:

·        Kusisitizwa kwa ukweli kuwa Afrika kama zilivyo sehemu nyingine duniani tayari imeanza kukabiliwa na  athari na matatizo makubwa kutokana na matatizo ya sasa ya uchumi duniani, hata kama Bara hilo halihusiki katika kuyaanzisha matatizo hayo.

·        Kwamba katika hali hiyo Afrika inazitaka nchi tajiri za G-8 kutenga raslimali maalum za kulisaidia Bara la Afrika kuondokana ma matatizo hayo kwa sababu Bara la Afrika pekee halina uwezo wa kufanya hivyo.

·        Kwamba nchi tajiri za G-20 zitimizwe ahadi zake za kulisaidia Bara la Afrika ambazo nchi hizo zilitoa huko nyuma lakini mpaka sasa halizijatelekezwa. Ahadi hizo ni pamoja na zile zilizotolewa Monterrey, Mexico na zile zilizotolewa Gleneagles, Scotland.

·        Kwamba makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa aina yake uliofanyika mwezi huu mjini Dar Es Salaam, kati ya Afrika na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kuhusu hali ya sasa ya matatizo ya uchumi duniani yakubaliwe na mkutano huo wa G-20 na yatekelezwe.

·        Kwamba Afrika inaunga mkono hatua ya Benki ya Dunia kuanzisha mfuko maalum wa kuzisaidia nchi masikini zikiwamo za Afrika kuhimili matatizo ya sasa ya uchumi duniani.

·        Kwamba yafanyike mageuzi makubwa katika mfumo wa utawala wa vyombo vya fedha duniani, ikiwamo IFM kwa lengo la kuliwezesha shirika hilo kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kusimamia uchumi wa dunia, na pia kutoa sauti kwa Bara la Afrika kusikika katika mfumo wa utawala wa shirika hilo.

·        Kwamba matatizo ya sasa ya uchumi yasiwe kisingizio cha nchi tajiri duniani kuweka vikwazo vya kujilinda zaidi kibiashara.

·        Kwamba nchi tajiri zisitumie matatizo ya sasa ya uchumi duniani kukata ama kupunguza misaada yao kwa nchi masikini za Afrika kwa sababu kufanya hivyo kutafuta kabisa mafanikio makubwa ambayo Bara hilo limepata katika miaka ya karibuni kutokana na kufanya mageuzi makubwa katika chumi za nchi za Bara hilo.

·              Kwamba kukata ama kupunguza misaada pia kutazifanya nchi za Afrika kushindwa kufikia Malengo ya Milenia, ambayo shabaha yake kuu ni kupunguza umasikini duniani kwa asilimia 50.

Mbali na kuhudhuria mkutano huo, akiwa London, Rais pia alikutana na watu mbali mbali akiwamo Waziri Mkuu wa Kenya, Odinga na Waziri wa Misaada ya Kimataifa ya Maendeleo wa Uingereza, Douglas Alexander.

Akiwa njiani kurejea nyumbani kutoka London, Rais Kikwete na ujumbe wake ulisimama kwa siku moja Dubai kwa shughuli nyingine za kikazi.

Mwisho.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais
Ikulu.
Dar es Salaam.