UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail: press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Ijumaa, Julai 30, 2010, ametuma salamu za rambirambi kwa Wakuu wa Mikoa ya Kagera na Shinyanga kufuatia vifo vya watu 16 vilivyotokana na ajali ya basi.

 

Ajali hiyo ilitokea majira ya saa tano asubuhi ya leo katika kijiji cha Kanegere, Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Shinyanga, wakati basi la Super Najimunisa lilipogongana ana kwa ana na lori la aina ya Fuso.

 

Basi hilo lilikuwa linatokea mjini Bukoba, Mkoa wa Kagera kuelekea Dar es Salaam na mbali ya watu 16 waliopoteza maisha, watu wengine 37 wameuamia na wako katika hali mbalimbali za maumivu. Majeruhi wamelazwa katika Hospitali za Wilaya za Kahama na Bukombe.

 

Katika salamu hizo za rambirambi kwa Mheshimiwa Mohammed Babu ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera na kwa Mheshimiwa Brigedia (mst) Dkt. Yohana Balele, Mheshimiwa Rais amesema:

 

Nimestushwa sana na habari za vifo vya wananchi wenzetu 16. Kwa hakika, nimesikitishwa mno na kuhudhunishwa sana na ajali hii mbaya, ambayo kwa mara nyingine, imesababisha vifo visivyokuwa vya lazima vya wananchi wenzetu. Nawatumieni salamu zangu za rambirambi na za dhati ya moyo wangu kuhusiana na ajali hii.”

 

Ameongeza Rais Kikwete: “Napenda kupitia kwenu kuwapa mkono wangu wa pole nyingi wafiwa wote ambao wamepoteza wapendwa wao katika ajali hii. Nawatakia moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na maombolezo. Napenda wafahamu kuwa moyo wangu uko nao katika kipindi hiki na kuwa msiba wao ni msiba wetu sote Watanzania.”

 

Kuhusu majeruhi, Rais Kikwete amesema: “Napenda pia kupitia kwenu kutoa mkono wa pole kwa wote walioumia katika ajali hii. Natakiwa pole sana na kuwaombea waweze kupata nafuu haraka ili warudi tena katika shughuli zao za maendeleo.”

 

Mheshimiwa Rais amewataka wakuu wa mkoa hiyo miwili na wilaya husika kuchukua kila hatua inayostahiki kuchunguza chanzo cha ajali hiyo na kuchukua hatua mwafaka.

 

Imetolewa na:

 

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

 

30 Julai, 2010