UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail: press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewashukuru viongozi wa dini nchini kwa kujali maendeleo ya wananchi na waumini wao kupitia utoaji wa huduma mbalimbali za jamii.

 

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa hakuna urithi bora zaidi ambao mzazi yoyote anaweza kutoa kwa mtoto wake kuliko kumpa elimu.

 

Rais Kikwete ameeleza hayo, usiku wa jana, Alhamisi 29, 2010, wakati wa chakula cha usiku cha kuchangisha fedha za ujenzi wa shule ya sekondari ya Ebenezer Lutheran Junior Seminary ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya Morogoro, kwenye ukumbi wa CCT mjini Morogoro.

 

Akizungumza kabla ya kuanza kwa uchangiaji, Rais Kikwete aliwaambia washiriki wa chakula hicho cha jioni: “Jitihada mnayofanya ya kupanua elimu kwa kujenga shule ni kielelezo tosha cha jinsi gani viongozi wetu wa dini mnavyojali maendeleo ya waumini wenu na wananchi kwa jumla.”

 

 

Aliongeza Mheshimiwa Rais Kikwete: “Sote tunatambua kuwa elimu ni ufunguo wa maisha. Hakuna urithi wenye thamani zaidi unaoweza kumpatia mtoto kuliko elimu. Nawapongezeni sana kwa uamuzi wenu huu wa kuwekeza kwenye elimu ya watoto wetu.”

 

Akimkaribisha Mheshimiwa Rais, Askofu Jacob Mameo Ole Paulo, Askofu wa Dayosisi ya Morogoro, alipongeza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nne kwa mafanikio makubwa katika miaka mitano iliyopita:

 

Mmepambana na rushwa na madawa ya kulevya. Mmepanua sana elimu na sasa nchi nzima imejaa shule za sekondari katika kila kata. Mmepanua sana huduma za afya. Umeonyesha dhamira ya dhati ya kupambana na ufisadi, mmeongeza wigo wa wananchi kupata haki kwa kuongeza sana idadi ya majaji na hivyo kupunguza mlundikano wa kesi. Mmepanua utalii.”

 

Askofu Ole Paulo alisema kuwa Dayosisi ya Morogoro ambayo ni moja ya dayosisi 20 za KKKT Tanzania nzima imeamua kujenga shule ya sekondari kwa sababu kwa sasa haina hata shule moja ya sekondari.

 

Alisema kuwa shule hiyo ya Ebenezer Lutheran Junior Seminary itakuwa ya mkondo wa sayansi na itaanza kwa kidato cha tano na sita kabla ya kuanza kwa kidato cha kwanza hadi cha nne na kuwa ujenzi utagharimu sh bilioni 2.41.

 

Askofu huyo ameishukuru Serikali kwa kulipatia dayosisi hiyo ekari 47 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo na ahadi ya kuongezewa ekari nyingine 53 ili kufikisha ekari 100.

 

Katika mchango wa jana, kiasi cha sh 131, 825,000 zilipatikana zikiwamo sh milioni 22 taslimu na kiasi kingine 46 kilikwishakuchangwa kabla ya hafla hiyo.

 

 

Imetolewa na:

 

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

 

 

30 Julai, 2010