DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
UNITED
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116898 E-mail: press@ikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S OFFICE, THE
STATE HOUSE, P.O. BOX 9120, DAR ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI
Na Mwandishi Maalum, Madrid, Hispania
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametaja sababu kuu za umasikini wa
Bara la Afrika, na kupendekeza mambo saba ambayo anasema kuwa yakifanyika
yatachangia kuliondoa Bara hilo katika udhalili wa umasikini wa sasa.
Aidha, Rais Kikwete amesisitiza kuwa
Bara la Afrika limeboreka sana katika miaka 15 iliyopita, na sasa liko tayari
kutoa mchango wake katika jumuia ya kimataifa kama juhudi za pamoja za Bara
hilo na Jumuia ya Kimataifa zitaendelezwa kuboresha hali katika Bara hilo.
Rais Kikwete alikuwa anazungumza
usiku wa leo, Jumatatu, Julai 19, 2010, kwenye ufungaji wa Mkutano wa Kimataifa
Kuhusu Maendeleo ya Afrika na Nafasi ya Siasa za Maendeleo katika Bara la
Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara uliofanyika katika Jumba la Palacio de
Congresos de Madrid, mjini Madrid, Hispania.
Rais Kikwete alikuwa miongoni mwa
viongozi wa kimaendeleo kutoka Bara la Afrika walioalikwa kuhudhuria Mkutano
huo ulioandaliwa kwa pamoja na chama tawala cha Hispania cha Socialist and
Workers Party of Spain (PSOE), chama tawala cha Afrika Kusini cha African
National Congress (ANC) pamoja na taasisi isiyokuwa ya kiserikali yenye
uhusiano wa karibu na PSOE ya Fundacion Idea.
Pamoja na Rais Kikwete kwenye
ufungaji wa Mkutano huo walikuwa ni Rais wa Cape Verde, Mheshimiwa Pedro Pires;
Waziri Mkuu wa Hispania, Mheshimiwa Jose Luis Rodriguez Zapatero; Waziri Mkuu
wa Ethiopia, Mheshimiwa Meles Zenawi; Rais wa zamani wa Serikali ya muda ya
Liberia, Mheshimiwa Amos Sawyer; na Rais wa chama tawala cha FPI cha Ivory
Coast, Mheshimiwa Pascal Affi N’Guessan.
Wengine walikuwa ni Rais wa chama
tawala cha Ghana cha National Democratic Congress, Mheshimiwa Kwabena Adjei na
Katibu Mkuu wa Chama cha Kisoshalisti cha Senegal, Mheshimiwa Ousmane Tanor
Dieng ambaye pia alikuwa mgombea urais wa nchi hiyo katika uchaguzi mkuu
uliopita.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Rais
Kikwete alitaja sababu kuu na chanzo cha umasikini wa Afrika kuwa ni pamoja na
mazingira adui ya kimataifa dhidi ya Bara la Afrika ambayo ni pamoja na
ukoloni, mfumo adui kabisa wa kiuchumi duniani ikiwa ni pamoja na nafasi finyu
za Afrika kufanya biashara na ukosefu wa masoko ya uhakika ya Afrika kuuza
bidhaa zake, tena kwa bei ya haki.
Rais Kikwete amesema kuwa sababu
nyingine za umasikini wa Afrika ni siasa za nchi za Afrika zenyewe ambazo huko
nyuma hazikuzaa matunda yaliyokusudiwa na zilizolazimishwa kwa nchi za Afrika
na taasisi za kimataifa za Bretton Woods – yaani Benki ya Dunia na Shirika la
Kimataifa la Fedha Duniani (IMF).
“Lakini makosa mengine yalikuwa ya
kwetu wenyewe, ikiwa ni pamoja na sera ambazo hazikuzaa matunda na mgawo mkubwa
mno wa ukosefu wa utulivu wa kisiasa, mapigano, upinduaji wa Serikali,” amesema
Rais Kikwete na kuongeza huku akishangiliwa na mamia ya washiriki wa mkutano
huo:
“ Tulikuwa hakuna nafasi ya
kufikiria jinsi ya kuondoa umasikini na kuendeleza watu wetu kwa sababu tulikuwa
na kazi na shughuli za kupigana, kugombea madaraka na kuuawa.”
Hata hivyo, Rais Kikwete amesema
kuwa hali ya Afrika imebadilika sana katika miaka 15 iliyopita. “Hili siyo tena
Bara la ovyo, siyo Bara ombaomba tena. Tuna utulivu mkubwa zaidi wa kisiasa,
ukiondoa Somalia, Bara la Afrika halina mgogoro wa kisiasa ambao kwa sasa hauna
majibu yake. Demokrasia inapaa, kuna hali bora zaidi ya utawala bora,
tunapambana kweli kweli na rushwa, tunajali haki za binadamu. Tunafanya vizuri,
lakini tunahitaji kufanya vizuri zaidi kwa kuwekeza katika hali na maisha ya
watu wetu.”
“Sasa tufanye nini?” Rais Kikwete
alijiuliza mwenyewe na kuanza kutoa majibu ya kuongeza kasi ya kulitoa Bara la
Afrika na watu wake katika umasikini akisisitiza:
“La kwanza ambalo lazima tufanye ni
kudumisha na kulinda mafanikio ambayo tumeyapata mpaka sasa. La pili ni
kuwekeza zaidi katika watu wetu. Tunahitaji kuboresha zaidi elimu, kuwapa watu
wetu maji safi na salama, tunahitaji kujenga miundombinu bora zaidi kwa maana
ya barabara, njia za umeme, kuboresha mifumo ya reli na bandari zetu.” Rais Kikwete amesema kuwa jambo la tatu
linalostahili kufanyika ni kufanya mageuzi ya kuboresha kilimo cha Afrika.
“Asilimia 70 ya watu wetu wanaishi
katika sehemu za mashamba na shughuli yako kubwa ni kilimo. Hii ndiyo njia
rahisi ya kuwatoa watu wetu katika umasikini. Afrika ina asilimia 10 tu ya
wakazi wote wa dunia, lakini Bara letu lina asilimia 30 ya watu wote masikini
zaidi duniani.”
Rais Kikwete amezitaja njia nyingine
za kulitoa Bara la Afrika katika umasikini haraka zaidi kuwa ni pamoja na
kuanza mageuzi ya ujenzi wa viwanda hasa vile za kuongeza thamani ya mazao ya
kilimo.
“Hatuwezi kuendelea kuuza mazao
ghafi kwenye masoko ambayo yanabadilisha thamani ya mazao hayo na kutuuzia
mazao yetu wenyewe tena kwa gharama kubwa zaidi.”
Ameongeza kuwa njia nyingine za
kulitoa Bara la Afrika katika umasikini ni kuongezeka kwa uingiaji wa mitaji
katika Bara hilo. Kwa sasa Bara la Afrika linapata asilimia mbili tu ya mitaji
yote ya uwekezaji duniani.
Rais Kikwete ametaja ongezeko kubwa
zaidi la biashara kama njia nyingine ya kupunguza umasikini wa Afrika. Kwa sasa
Afrika inachangia asilimia mbili tu katika biashara duniani. Pia ametaja
umuhimu wa kuongeza kasi ya ushirikiano wa kikanda miongoni mwa nchi za Afrika
na umuhimu wa kumalizika kwa mazungumzo ya kuleta mfumo mpya wa kibiashara
duniani chini ya majadiliano ya Doha.
Akizungumza baada ya hotuba ya Rais
Kikwete, Waziri Mkuu Zapatero alikubaliana na mapendekezo mengi ya Rais Kikwete
na kuahidi kuwa Hispania imeamua kuwa sehemu na kuchangia ya maendeleo ya
Afrika. “Napenda kutangaza kuwa kuanzia leo hii Hispania iko ndani ya Afrika,
na Afrika iko ndani ya Hispania.”
Imetolewa na:
Salva Rweyemamu,
MADRID,
HISPANIA.
20 Julai, 2010