UNITED REPUBLIC OF
TANZANIA
DIRECTORATE OF
PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116539 E-mail: press@ikulu.go.tz Website: www.mawasilianoikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S
OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX
9120, DAR ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
Balozi: Papa
Benedict afurahishwa na amani ya kidini Tanzania
Pamoja na kutaka kujua
hasa nini siri ya mafanikio
ya utulivu na uvumilivu huo
wa kidini katika Tanzania, Baba Mtakatifu pia amewapongeza viongozi wa nyanja
na sekta mbalimbali katika Tanzania kwa kudumisha uvumilivu
huo na kuwataka
kuendeleza kushikilia siri ambayo imedumisha
utulivu huo kwa miaka 50 tokea
uhuru.
Msimamo huo wa Papa Benedict wa 16 umeelekezwa leo, Alhamisi, Septemba 29, 2011, na Balozi wa Makao
Makuu ya Baba Mtakatifu ya Vatican katika Tanzania, Mhashamu Askofu Mkuu Joseph Chennoth wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Ikulu, Dar es Salaam.
Mhashamu Askofu Mkuu Chennoth
alikuwa anamuaga Rais Kikwete baada
ya kumaliza muda wake wa
uwakilishi wa Vatican katika Tanzania. Askofu Mkuu Chennoth amekaa nchini miaka
sita ikiwa sehemu ya miaka
15 ambako ameiwakilisha
Vatican katika nchi mbalimbali za Afrika.
Balozi Chennoth ambaye aliwasili nchini Agosti 22, mwaka 2005, na kuwasilisha
hati zake za utambulisho siku tisa baadaye,
Septemba Mosi, mwaka huo huo,
anahamishiwa Japan.
Katika mazungumzo kati ya viongozi hao,
Balozi Chennoth amemwambia Rais Kikwete: “Siku zote Baba Mtakatifu amekuwa anaulizia juu ya siri
ya mafanikio ya uvumilivu wa kidini katika Tanzania. Kwa hakika, Baba Mtakatifu anatambua hali hii, anawapongeza viongozi wa
Tanzania kwa kulisimamia na pia anaombea
hali hii iendelee kuwepo katika Tanzania.”
Balozi Chennoth pia amemwambia
Rais Kikwete kuwa kiongozi wa kweli kweli wa dini
huhubiri amani, umoja na mapenzi
na wala siyo
mifarakano na mapigano.
Balozi pia amesifia ushirikiano
uliopo katika Tanzania kati ya viongozi
wa dini
na wale wa siasa. “Sisi siyo washindani, siyo wapinzani. Sisi ni wabia na washiriki
katika shughuli za kuwahudumia wananchi na kuwafikishia
huduma za kijamii. Tunashirikiana katika utoaji elimu,
katika utoaji huduma za afya
na huduma
nyingine za kiroho na kimwili.
Kwa kweli imekuwa ni
faraja yangu kubwa kutumikia katika nchi hii
yenye historia ya kutukuka duniani,
nchi ya Mwalimu
Kambarage Nyerere.”
Rais Kikwete amempongeza Balozi huyo kwa kukuza uhusiano kati ya
Tanzania na Vatican katika kipindi chake cha uwakilishi akisema, “umesaidia sana katika kuimarisha uhusiano kati ya
Vatican na nchi yetu, kati ya
umoja wa Kikatoliki duniani na wananchi wetu.
Tunakushukuru sana.”
Rais Kikwete pia amesifia
uhusiano ulioko kati ya Serikali
yake na
Kanisa Katoliki na kuwataka viongozi
wa kisiasa na kidini kukumbuka
kuwa wao wanayo dhamana kubwa ya kuendeleza
uhusiano huo na pia kudumisha
uvumilivu wa kidini katika Tanzania.
“Ni wajibu wetu sisi viongozi
wa kisiasa
na viongozi wa dini kuhakikisha
kuwa nchi yetu inaendelea kuwa ya amani
na tunaendelea kuishi kwa namna
hii ya kuvumiliana
kidini, kuoleana na kubakia ndugu.
Jukumu hili liko mikononi
mwetu. Tukivuruga utulivu huo tutakuwa
tumeivuruga nchi yetu kwa
namna ya kudumu hatutaupata tena utulivu huo
kwa sababu ni vigumu sana
kuutengeneza upya.”
Rais Kikwete pia ametumia
nafasi ya mazungumzo hayo kumkumbusha Balozi Chennoth kuhusu mwaliko wake ambao aliutoa kwa
Baba Mtakatifu wakati alipotembelea Vatican mwaka 2008.
“Nilimpa mwaliko Baba Mtakatifu wakati tulipokutana Vatican wakati wa ziara
yangu aliponialika nimtembelee na baada ya hapo
tulipokutana mjini Napoli. Bado Wakatoliki wa Tanzania na
Watanzania kwa jumla wanaendelea kumsubiri.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR
ES SALAAM.
29
Septemba, 2011