UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116539

E-mail: press@ikulu.go.tz

Website:  www.mawasilianoikulu.go.tz  

Fax: 255-22-2113425

 

Coat of Arms

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Alhamisi, Machi 31, 2011, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Zimbabwe, Mheshimiwa Morgan Tsvangirai.

 

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, mjini Dar es Salaam, Mheshimiwa Tsvangirai ambaye aliwasili nchini jana usiku akifuatana na maofisa saba, amemwelezea Rais Kikwete kuhusu hali ilivyo katika Zimbabwe na ushirikiano ulivyo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Zimbabwe.

 

Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Tsvangirai kuwa Tanzania itaendelea kuwa tayari kuisaidia Zimbabwe kutatua matatizo yake hasa yale ya kisiasa na pia kuisaidia Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili iweze kutekeleza majukumu yake.

 

Sisi katika Tanzania tunataka kuiona Zimbabwe yenye amani, Zimbabwe yenye mafanikio na tuko tayari kusaidia kwa namna yoyote ambayo wananchi na Serikali ya Zimbabwe inaona inafaa,” Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Tsvangirai katika mazungumzo hayo.

 

Mheshimiwa Tsvangirai ambaye aliwasili nchini jana usiku akitokea Malawi yuko kwenye ziara ya nchi za Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa nia ya kuwaelezea viongozi wa nchi hizo hali ilivyo katika Zimbabwe na changamoto zinazoikabili Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

 

Kabla ya kuja Tanzania, Mheshimiwa Tsvangirai alikuwa ametembelea Jamhuri ya Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Jamhuri ya Namibia, Mozambique, Afrika Kusini, Ufalme wa Swaziland na Zambia.

 

Mara baada ya mazungumzo na Rais Kikwete, Mheshimiwa Tsvangirai na ujumbe wake wameondoka mjini Dar es salaam kwenda Livingstone, Zambia kuhudhuria mkutano wa nchi tatu zinazounda Kamati Maalum (Troika) ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC inayokutana leo.

 

Kamati hiyo iliyoundwa Juni mwaka 1996 ndiyo yenye jukumu ya kujadili na kutafuta njia za kumaliza matatizo ya kisiasa katika eneo la nchi wanachama wa SADC na nchi tatu zinazounda Kamati hiyo kwa sasa ni Zambia, Afrika Kusini na Mozambique.

 

Rais Rupiah Bwezani Banda wa Zambia atakuwa mwenyekiti wa kikao hicho ambacho pia kinahudhuriwa na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini na Rais Armando Emilio Guebuza wa Mozambique.

 

Imetolewa na:

 

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

 

31 Machi, 2011