DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail: press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

Rais Jakaya Kikwete leo, Jumatatu, Juni 8, 2009, amekutana na kufanya mazungumzo na mabalozi wa Cuba na Saudi Arabia katika Tanzania.

 

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Balozi wa Cuba, Ernesto Gomez Diaz amemkabidhi Rais Kikwete mwaliko kutoka kwa Rais Raul Castro Ruz kumwomba atembelee Cuba baadaye mwaka huu.

 

Rais Kikwete ameshukuru kupata mwaliko huo. Pia Rais ameukubali mwaliko huo na kumwahidi Balozi huyo kuwa itatafutwa tarehe mwafaka kuweza kufanikisha mwaliko huo na ziara hiyo.

 

Naye Balozi wa Saudi Arabia, Ali Abdallah Suleiman Al-Jarbou amemwambia Rais Kikwete kuwa ziara yake katika nchi hiyo, Aprili, mwaka huu, imefungua milangoyotekwa aina mpya ya ushirikiano kati ya Tanzania na Saudi Arabia.

 

Amesema kuwa ziara hiyo pia imetoa mwelekeo mpya wa Saudi Arabia na wananchi wake kuhusu Tanzania, na amemshukuru Rais Kikwete kwa kukubali mwaliko wa kufanya ziara hiyo.

 

 

Rais Kikwete amekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania kualikwa na kutembelea Saudi Arabia.  Pia Rais Kikwete amekuwa kiongozi wa kwanza wa Afrika kualikwa kwa ziara rasmi katika nchi hiyo ya Kiarabu.

 

Vile vile Rais Kikwete alikuwa kiongozi wa kwanza kupewa nishani maalum na taifa la Saudi Arabia, na Balozi Al Jarbou amesema kuwa nishani ya pili ya aina hiyo amepewa Rais Barak Obama wa Marekani.

 

Balozi Al-Jarbou ameshauri kuwa sasa umefika wakati kwa mawaziri wa Tanzania kutembelea Saudi Arabia, ili kufuatilia utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa katika mazungumzo kati ya Rais Kikwete na kiongozi wa Saudia Mfalme Abdullah bin Abdul Aziz al Saud.

 

Imetolewa na:

 

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

 

08 Juni, 2009