DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail:  ikulumawasiliano@yahoo.com

              press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameagiza uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO kusimamia shughuli ya kutengeneza mashine zilizoharibika katika kituo cha umeme cha Lizaboni, mjini Songea kwa karibu zaidi ili wananchi waondokane na tatizo la ukosefu wa umeme linalowakabili kwa kipindi kipatacho miezi minne sasa.

 

Rais Kikwete ametoa maagizo hayo leo mara baada ya kukagua kituo hicho cha TANESCO na kukutana na wananchi wengi waliokuwa wanamlilia kuwatafutia ufumbuzi wa umeme ambao umekuwa kero kubwa kwao.

 

“Simamieni kwa karibu matengenezo ya mashine hizi ili tofauti ianze kuonekana baada ya siku nne” amesema.

 

Kulingana na taarifa za TANESCO katika mji wa Songea, mashine mbili kati ya sita zinazozalisha umeme katika mji huo zimeharibika na ziko katika hatua ya mwisho ya matengenezo na wamemweleza Rais kuwa kifaa kinachotakiwa  katika machine moja wapo kimeshaletwa na kufungwa ila wanasubiri mafundi kutoka kampuni ya Caterpillar waje kusimamia kuanza kwa uzalishaji wa umeme katika mashine moja wapo. Hata hivyo kifaa kingine kitachukua zaidi ya majumu mawili kwani kinahitaji matengenezo zaidi.

 

Rais Kikwete amesema hii ni hatua ya dharura kwa sasa kwani mji huo umo katika mpango wa baadaye wa kupata umeme kutoka katika grid ya Makambako ambayo itachukua muda mrefu.

 

Rais Kikwete amefika kituoni hapo akitokea Wilaya ya Namtumbo ambako alikwenda kukagua shughuli za maendeleo, kuhamasisha  na kufungua miradi ya wananchi ambapo amekamilisha ziara yake kwa kufungua ofisi ya mkuu wa Wilaya.

 

Akiwa katika Wilaya ya Mbinga na Namtumbo, Rais amesikiliza kero za wananchi kupitia kwa viongozi wao ambapo kero kubwa zimekua zinazohusu maji, afya, elimu na Kilimo.

 

Akijibu hoja za matatizo hayo, Rais ameelezea hatua mbalimbali na juhudi zinazofanywa na serikali katika kutatua matatizo hayo.

Katika elimu suala kubwa limekuwa shule, walimu na maabara, Rais amesema suala la walimu ni suala ambalo serikali inalifahamu na hivi karibuni walimu watahitimu na kuajiriwa katika shule zilizojengwa kwani serikali ilichukua hatua ya makusudi ya kuongeza vyuo vya elimu nchini vikiwemo vyuo vya  Chang’ombe, mkoani Dar-Es-Salaam, Mkwawa cha Mkoani Iringa na Chuo Kikuu cha Dodoma.

 

Rais pia amesema kuanzia mwaka ujao serikali, kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) na Benki ya Dunia  itaanza mpango mkubwa wa kujenga maabara kwa ajili ya shule zote hapa nchini. Rais amerejea Dar-Es-Salaam leo jioni.

 

Mwisho

 

Imetolelwa na Premi Kibanga

Ikulu.

Dar es Salaam.

13 Agosti, 2009