UNITED
REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116539 E-mail: press@ikulu.go.tz Website: www.mawasilianoikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O.
BOX 9120, DAR
ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jioni ya leo, Jumamosi, Septemba 10,
2011, ametembelea Viwanja vya Maisara mjini Zanzibar kujionea mwenyewe zoezi la
kutambua miili iliyoopolewa kutoka baharini kufuatia ajali ya kuzama kwa meli
ya Mv Spice Islander alfajiri ya
kuamkia leo.
Akifuatana na Mama Salma
Kikwete, Mheshimiwa Rais Kikwete amewasili Uwanja wa Ndege wa Zanzibar saa 12:10 jioni na
kwenda moja kwa moja kwenye Viwanja vya Maisara ambako mamia kwa mamia ya
waombolezaji walikuwa wamekusanyika kujaribu kutambua miili za jamaa, ndugu na wapendwa
wao ambao wamepoteza maisha katika ajali hiyo.
Kwenye Viwanja hivyo, Rais
Kikwete amepokelewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
(SMZ) Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wawili wa Rais wa Zanzibar, Waheshimiwa
Seif Sharif Hamad na Balozi Seif Idd, Rais Mstaafu wa Zanzibar Mheshimiwa Amani
Abeid Karume na uongozi karibu wote wa juu wa SMZ.
Hali ilikuwa ya huzuni sana
kwenye Viwanja hivyo wakati Mheshimiwa Rais akifuatana na uongozi huo wa juu wa
Zanzibar ulivyopitia kwenye mahema ya muda ya zoezi ya utambuzi wa miili ya
watu waliopoteza maisha yao katika ajali hiyo ya meli hiyo iliyokuwa inasafiri
kutoka Dar-Zanzibar-Pemba. Imezama katika eneo la Nungwi, Zanzibar.
Katika eneo hilo la utambuzi,
Mheshimiwa Rais ameshuhudia miili ya watu wazima iliyokuwa imefungwa ama
kufunikwa na ile ya watoto wadogo ambao sura zao zilikuwa zimeachwa wazi kwa
ajili ya utambuzi wa haraka kwa mujibu wa sura zao.
Kwenye Viwanja hivyo,
Mheshimiwa Rais ameambiwa kuwa hadi jioni hiyo ya leo, watu kiasi cha 192 walikuwa
wamethibitishwa kuwa wamepoteza maisha na miili yao kuopolewa wakati kiasi cha
watu 630 walikuwa wameokolewa kutoka ajali hiyo ya meli ambayo hadi sasa
haijulikani ilikuwa imebeba watu wangapi.
Baadaye, Rais Kikwete
ametembelea Hospitali ya Mnazi Mmoja kuwaona na kuwatakia heri waliokoka katika
ajali hiyo na kulazwa katika hospitali hiyo ya Serikali.
Hadi jioni ya leo, Serikali ya
Jamhuri ya Muungano ilikuwa imechukua maamuzi kadhaa kukabiliana na hali ya
ukoaji wa watu katika ajali hiyo. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na
kuchangia kiasi cha sh milioni 300 ili kusaidia zoezi hilo ikiwa ni pamoja na
kusaidia kusafirisha na kuzika miili ya watu waliopoteza maisha katika ajali
hiyo. SMZ imetoa sh milioni 100 kwa shughuli hiyo.
Serikali ya Muungano pia
imeamua kukubali msaada wa wapigaji mbizi kutoka Afrika Kusini kwa ajili ya kusaidia
kufanya tathmini ya jinsi meli ilivyozama na kuokoa maisha ya watu ambao
watakuwa wamebanwa ndani ya meli hiyo.
Kesho, Jumapili, Septemba 11,
2011, Kamati ya Taifa ya Ulinzi na Usalama itafanya kikao chake mjini Zanzibar
kuzungumzia hali ya ajali hiyo kwa maana ya kupata maelekezo kamili kuhusu
ajali hiyo, kupokea ripoti ya ajali, kufanya tathmini ya ripoti hiyo na kutoa
maelekezo ya jinsi ya kukabiliana na hali ya sasa na hali ya baadaye ya usafiri
wa maji nchini.
Hata kabla ya kikao hicho,
tayari Mheshimiwa Rais Kikwete ameamua kufanyika kwa uchunguzi wa kina kubaini
chanzo cha ajali hiyo.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES
SALAAM.
11 Septemba, 2011