DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail: press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

SALAMU ZA RAMBIRAMBI ZA MWENYEKITI WA CCM – TAIFA NA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

 

          Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) – Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Katibu Mkuu wa CCM, Mhe. Yusuf Makamba kuomboleza kifo cha Amani Nzugile Jidulamabambasi kilichotokea tarehe 2 Agosti, 2010 alipokuwa akiwahishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando mkoani Mwanza kupatiwa matibabu.

 

          Marehemu Jidulamabambasi alikuwa miongoni mwa wanachama wa CCM waliokuwa wamejitokeza kuwania kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi kugombea Ubunge katika Jimbo la Uchaguzi la Maswa Magharibi.

 

          “Ninakutumia salamu za rambirambi wewe Katibu Mkuu wa CCM na wana – CCM kote nchini kwa kumpoteza mmojawapo wa makada katika chama chetu”,  amesema Mhe. Kikwete katika salamu zake, na kuongeza, “aidha kupitia kwako, natuma salamu za rambirambi na pole nyingi kwa familia ya marehemu Amani Nzugile Jidulamabambasi kwa kuondokewa na kiongozi muhimu wa familia yao”.

 

 

          Katika salamu hizo za rambirambi, Mhe. Kikwete amemwelezea marehemu kuwa miongoni mwa makada jasiri wa CCM wasiokata tamaa katika medani za siasa na mpambanaji hodari aliyekuwa na dhamira ya dhati ya kulitumikia Taifa na Umma wa Watanzania hususan wananchi wa Jimbo la Maswa Magharibi kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi.

 

          Amesema anamwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aiweke mahali pema peponi roho ya Marehemu Jidulamambasi na kuwaomba wafiwa pamoja na ndugu, jamaa na marafiki kuwa na moyo wa uvumilivu na subira wakati huu wa maombolezo kwani yote ni mapenzi yake Mola.

 

Imetolea na:

 

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

 

03 Agosti, 2010