UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116539

E-mail: press@ikulu.go.tz

Website:  www.mawasilianoikulu.go.tz  

Fax: 255-22-2113425

 

Coat of Arms

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Ijumaa, Machi 11, 2011 amekutana na kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wazito kutoka nchi za Japan na Uturuki.

 

Katika mikutano hiyo miwili tofauti iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete kwanza amekutana na wajumbe wa Kamati ya Mahusiano ya Africa-Japan ya Chama cha Watendaji Waandamizi  wa Makampuni ya Japan cha Keizai Doyukai.

 

Kundi hilo la wafanyabishara kutoka Japan liliongozwa na  Bwana Sekiyama Mamoru,  Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Bodi ya Kampuni ya Marubeni Corporation.

 

Baadaye, Rais Kikwete amekutana na kuzungumza na kundi la wafanyakabiashara ya Uturuki wakiongozwa na Waziri wa Nchi wa Biashara wa Serikali ya Uturuki, Mheshimiwa Zafer Caglayan.

 

Rais Kikwete amewataka Wajapan hao wanaotembelea nchi za Tanzania, Kenya na Ethiopia kuongeza kasi yao katika kuwekeza katika uchumi wa Tanzania na hasa katika maeneo ya uzalishaji umeme, kilimo, uvuvi, usafirishaji wa mizigo na uchimbaji wa madini.

 

Aidha, Rais Kikwete, kupitia kwa ujumbe huo kutoka Japan, ametoa rambirambi na pole kwa nchi ya Japan na wananchi wake kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lilisababisha tsunami kwenye pwani ya nchi hiyo.

 

Kiasi cha watu kati ya 200 na 300 wanaripotiwa kupoteza maisha katika tsunami hiyo ambayo pia imesababisha kiasi cha mioto 80 katika sehemu mbalimbali za Japan ukiwemo moto uliolipuka katika kiwanda cha kusafisha mafuta.

 

Katika mazungumzo na Waziri  Caglayn na ujumbe wake, Rais Kikwete amerudia wito ule ule wa kuwakaribisha wafanyabiashara na makampuni ya Uturuki kuja kuwekeza Tanzania. Ujumbe huo ulikuwa nchini kwa mkutano na wafanyabiashara wa Tanzania.

 

Waziri huyo wa Uturuki pia amewasilisha kwa Rais Kikwete ujumbe maalum kutoka kwa Rais wa Uturuki, Mheshimiwa Abdullah Gur na mwaliko wa kumwomba ahudhurie mkutano wa nchi zenye maendeleo kidogo zaidi wa LDC ulipangwa kufanyika nchini Uturuki Mei mwaka huu.

 

Mwisho.

 

 

Imetolewa na:

 

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

 

11 Machi, 2011