UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116539

E-mail: press@ikulu.go.tz

Website:  www.mawasilianoikulu.go.tz  

Fax: 255-22-2113425

 

Coat of Arms

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameondoka nchini asubuhi ya leo, Jumatano, Mei 25, 2011, kwenda Addis Ababa, Ethiopia kuhudhuria mkutano maalum wa wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika (AU).

 

Mkutano huo wa siku mbili utajadili hali ya amani na usalama katika Bara la Afrika kufuatia matukio ya karibuni na yanayoendelea katika nchi za Libya, Sudan, Somalia na Ivory Coast.

 

Mkutano huo ulioanza mchana wa leo na utaendelea kesho asubuhi umeitishwa kufuatia pendekezo la Tume ya Amani na Ulinzi (PSC) ya AU lililotolewa katika mkutano wa Tume hiyo uliofanyika Aprili 24, mwaka huu.  Hadi Mei 20, 2011, pendekezo hilo lilikwishakuungwa mkono na zaidi ya nchi 38 ambayo ni idadi zaidi ya theluthi mbili ambayo inatakiwa kwa AU kuweza kuitisha mkutano maalum wa wakuu wa nchi wanachama wa AU.

 

Moja ya mambo yatayojadiliwa kwa kina katika kikao hicho ni hali ya Libya, nchi ambayo imeingia katika machafuko na vita kubwa tokea nchi wanachama wa Umoja wa Kujihami wa Ulaya (NATO) zilipoanza kuishambulia nchi hiyo kwa ndege za kivita, ili kuunga mkono waasi wa utawala wa Muammar Gaddafi ambaye amekuwa anatawala nchi hiyo kwa miaka 41.

 

Hali ya usalama katika Libya ilianza kubadilika tokea Februari 16, mwaka huu, wakati waandamanaji kati ya 600 na 700 walipoingia mitaani katika mji wa pili kwa ukubwa wa Benghazi kupinga uongozi wa miaka mingi wa Gaddafi.

 

Machi 17, 2011, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC), kwa kuombwa na nchi za Kiarabu, lilipitisha Azimio 1973 la kuzuia ndege yoyote kuruka kwenye anga ya Libya na siku mbili baadaye nchi baadhi ya nchi wanachama wa NATO zilianza kuishambulia Libya kwa ndege za kivita.

 

Hali ya Sudan ambayo inajiandaa kwa ajili ya kuzaliwa kwa taifa jipya la Sudan Kusini iliingia katika dosari kubwa wiki iliyopita wakati majeshi ya Sudan yaliposhambulia na kuvamia jimbo la Abyei lililoko mpakani wa pande hizo mbili. Majeshi ya Sudan yalivamia jimbo hilo baada ya majeshi ya Sudan Kusini kudaiwa kushambulia msafara wa Umoja wa Mataifa (UN).

 

Hali hiyo imezua wasiwasi miongoni mwa mataifa mbalimbali duniani kuwa inaweza kuwa kikwazo katika kuiwezesha Sudan Kusini kwa taifa huru hapo Julai 9, mwaka huu, 2011.

 

Somalia inaendelea kukabiliwa na ukosefu mkubwa wa amani na usalama na miaka 20 sasa ikiwa haina Serikali huku ikiwa chimbuko kubwa la uharamia katika eneo la mashariki mwa Afrika. Ivory Coast itajadiliwa kwa maana ya wakuu wa nchi hizo kupewa ripoti ya hali ilivyo katika nchi hiyo kufuatia Rais Alasane Quattara kuapishwa kuwa kiongozi wa nchi hiyo hivi majuzi.

           

Imetolewa na:

 

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

 

25 Mei, 2011