UNITED
REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116539 E-mail: press@ikulu.go.tz Website: www.mawasilianoikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete mchana wa leo, Ijumaa, Machi 11, 2011,
amerejea nyumbani kutoka kwenye ziara ya kikazi mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Rais Kikwete aliondoka Jumatano wiki hii
kwenda Ethiopia ili kujiunga na marais wenzake wa Afrika ambao wamepewa jukumu
ya kutafuta suluhu katika mgogoro wa kisiasa wa nchi ya Afrika Magharibi ya
Ivory Coast.
Mjini Addis Ababa, Rais Kikwete alijiunga
na marais kutoka Afrika Kusini, Chad, Mauritania na Burkina Faso kuendelea na
jitihada za kutafuta jinsi ya kurejesha amani na demokrasia katika Ivory Coast.
Kundi hilo la marais wa Afrika lilipewa jukumu
hilo na Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU) katika kikao chake cha
Januari, mwaka huu, mjini hapo hapo Addis Ababa.
Mzozo wa Ivory Coast ulilipuka kufuatia
matokeo ya raundi ya pili ya Uchaguzi Mkuu wa Rais nchini humo Novemba 28,
mwaka jana, 2010.
Katika matokeo hayo, Tume ya Uchaguzi ya
Ivory Coast ilimtangaza aliyepata kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Alassane
Quattara kuwa mshindi.
Lakini siku nne baadaye, Baraza la Katiba ya
nchi hiyo lilibatilisha matokeo hayo kwa kufuata matokeo ya kura 600,000 katika
majimbo saba ya kaskazini mwa nchi ambako ndiko ngome ya Mheshimiwa Quattara.
Badala yake, Baraza hilo lilimtangaza aliyekuwa anatetea kiti chake, Mheshimiwa
Laurent Gbagbo kuwa mshindi.
Mwisho.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR
ES SALAAM.
11Machi,
2011