UNITED REPUBLIC OF
TANZANIA
DIRECTORATE OF
PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116539 E-mail: press@ikulu.go.tz Website: www.mawasilianoikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S
OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX
9120, DAR ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete ameiagiza Wizara ya Ujenzi kukishughulikia
mara moja kile alichokiita “genge la watu waliojipanga
kuidhulumu Serikali na wananchi” kwa
kuwalipa mabilioni ya fedha makandarasi
ambao ujenzi wao wa barabara
ni wa kiwango
hafifu na cha chini.
Aidha, Rais
Kikwete ameigiza Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi
kuacha mara moja kugawa maeneo
ya wazi na
badala yake kuyasimamia ipasavyo maeneo hayo yakiwamo
yale ya watoto
kuchezea kwa kuzuia kabisa ujenzi katika maeneo hayo.
Ili
kutekeleza hilo, Rais Kikwete, ameagiza
kuondolewa na kubomolewa mara moja kwa mabati
yaliyozungushiwa katika eneo la Jangwani, Dar es Salaam, ambalo kwa jadi ni
eneo la viwanja vya kuchezea watoto
na hivyo kuzuia ujenzi uliopangwa
kufanyika katika eneo hilo.
Rais Kikwete
ametoa maagizo hayo leo,
Jumatatu, Aprili 4, 2011, wakati alipoweka jiwe la msingi la upanuzi wa Barabara
ya New Bagamoyo Road, eneo la Mwenge-Tegeta, katika sherehe iliyofanyika Mwenge mjini Dar es Salaam. Rais Kikwete ameshirikiana
na Balozi
wa Japan katika Tanzania, Mheshimiwa Hiroshi Nakagawa katika
uwekaji huo wa jiwe la msingi.
Ujenzi wa kipande hicho cha kilomita 12.9 kutoka Mwenge hadi
Tegeta unagharimiwa kwa kiasi cha shilingi
bilioni 88 na serikali ya Japan na barabara hiyo
inajengwa kwa kiwango cha lami kwa njia nne
na vituo 22 vya mabasi.
Akizungumza kwenye
sherehe za uwekaji wa jiwe
hilo la msingi ya upanuzi wa
barabara hiyo, Rais Kikwete pia
alitangaza kuwa Serikali baada ya kuwa imeendesha
kwa mafanikio Mfuko wa Barabara
(Road Fund) sasa inaanzisha
Mfuko wa Maendeleo ya Barabara
(Road Development Fund) akifafanua kuwa Road Fund kazi yake ni kufanya
matengenezo ya barabara na mfuko
mpya utakuwa na jukumu la kujenga
barabara.
Rais Kikwete
pia amekejeli baadhi ya madai
ambayo yamekuwa yanatolewa na
baadhi ya wananchi kuwa maendeleo
ya Tanzania yanakwenda kwa kasi ndogo
kulinganisha baadhi ya nchi nyingine
za Afrika zikiwamo baadhi ya nchi za
jirani.
“Tanzania
ni nchi kubwa. Ukubwa una uzuri wake na una gharama zake. Umeme uliovutwa kutoka Kidatu hadi Tarime,
kwa mfano,
kama ungewekwa katika baadhi ya
nchi nyingine, umeme huu ungefungwa
hata kwenye matendegu ya vitanda.
Na hata ujenzi wa barabara
za lami wa
barabara tunazozijenga katika miradi yetu
105 katika nchi nyingine barabara hizi zingeingia hata majumbani mwa watu. Jamani, Tanzania ni nchi kubwa
na maendeleo yetu ni makubwa,
tuache kuilinganisha na nchi nyingine
hizi ndogo ndogo.”
Kuhusu ujenzi
wa barabara kwa kiwango kisichoridhisha,
Rais Kikwete amesema: “Barabara zina gharama kubwa
sana na nyingine
zinajengwa kwa kiwango hafifu kwa sababu mbili.,
Moja ni kwamba
mhandisi mshauri wetu ni mzembe
ama Wizara na Wakala wa
Barabara (Tanroads) nao wanazembea na kuwalipa makandarasi
ambao barabara zao ni za
kiwango duni.”
“Tunawalipa
kwa nini? Nimelisemea
hili na
sitaki kulisemea tena. Lipo genge zima la watu waliojipanga kudhulumu – Waziri hili lazima liishe.
Sitaki kulisemea tena,” Rais amemsisitizia
Waziri wa
Ujenzi, Mheshimiwa John Pombe Magufuli ambaye kabla ya
hapo alikuwa ametoa hotuba ya
kusisimua kuhusu mafanikio makubwa ya Serikali ya
Kikwete katika ujenzi wa barabara
nchini.
Kabla ya hapo, Rais Kikwete
amezungumzia ugawaji holela wa
viwanja katika maeneo ya wazi
wazi na yale
ya watoto kuchezea michezo: “Na nyie watu wa
Ardhi, juzi nimepita Jangwani nikienda Morogoro na kuona mtu
amezungushia mabati kwenye kiwanja cha kuchezea watoto. Kabomoeni wenyewe mabati yale.
Nimelisemea mara nyingi hili la kulinda maeneo ya wazi na maeneo ya watoto wetu
kuchezea. Sitaki kulisemea tena.
Nendeeni mkaondoe yale mabati
yote na eneo
libakie la watoto kuchezea.
Rais Kikwete
pia ameishukuru Serikali ya Japan na watu
wake kwa kuendelea kutoa misaada muhimu
katika maendeleo ya Tanzania.
Rais Kikwete
pia amewaomba walioshiriki katika sherehe hiyo kusimama
kwa dakika
moja kuwakumbuka maelfu kwa maelfu
ya wananchi wa Japan ambao majuzi wamepoteza maisha yao katika
mafuriko na uharibifu uliosababishwa na tetemeko kubwa
la ardhi lililofuatiwa na kimbunga cha tsunami.
Imetolewa na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR
ES SALAAM.
04
Aprili, 2011