DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail: press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

 

Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameitaka Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kuacha kuchukua maamuzi makubwa kuhusu uendeshaji wa Reli ya Kati bila kuishirikisha Serikali, kwa sababu Reli hiyo siyo mali ya kampuni hiyo bali mali ya Serikali ya Tanzania na ya Watanzania.

 

Rais amesema kuwa maamuzi yote makubwa kuhusu Reli hiyo lazima yafanywe kwa kuishirikisha Serikali ya Tanzania ambayo inamiliki asilimia 49 ya hisa katika TRL. Kampuni ya RITES ya India inamiliki asilimia 51 ya hisa katika kampuni hiyo.

 

Rais Kikwete ametoa msimamo huo leo, Ijumaa, Januari 16, 2009, wakati wa kikao kati yake na uongozi wa Wizara ya Miundombinu pamoja na uongozi wa TRL katika mfululizo wa mikutano yake na Wizara mbalimbali za Serikali yake kufuatilia utendaji wa Wizara hizo.

 

Sisi kama Serikali ya Tanzania ni mbia-mwenza na siyo mshirika mdogo katika makubaliano ya kuendesha Reli hii. Nyie hamna haki na hamwezi kutoa maamuzi yenu peke bila kuishirikisha Serikali.  Reli mali yetu.  Njia ya kudumu ya reli ni ya kwetu. Sisi ndiyo wamiliki wa Reli hiyo kwa asilimia 100. Nyie tumewaajiri tu kama waendeshaji tu,” amesisitiza Rais Kikwete katika mkutano huo uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

 

Sisi tuko katika ubia, na kila yanapotakiwa kuchukuliwa maamuzi makubwa kuhusu Reli ni lazima tuwasiliane na kukubaliana kwa pamoja. Msichukue maamuzi peke yenu. Hii siyo Reli yenu. Reli ni yetu,” amesema Rais katika kikao hicho.

 

Rais amelazimika kutoka msisitizo huo baada ya kuwa amepata maelezo kutoka kwa uongozi wa TRL kuhusu mipango ya uendeshaji wa Reli hiyo katika mkutano huo ambao pia umehudhuriwa na uongozi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mali za Reli (RAHCO).

 

Miongoni mwa mipango hiyo ni kujaribu kupata mkopo mkubwa wa kuendesha shughuli za Reli hiyo bila ridhaa ya Serikali, mipango ya kuacha kutoa huduma kwenye baadhi ya vipande vya Reli kwa madai kuwa havina faida, hali ya usalama ya Reli yenyewe, maombi ya TRL kuzidi kupungizwa kodi, na hata kutaka mipango ya kung’oa kipande cha reli kati ya Tanzania na Kenya kwa madai kuwa hakina faida.

 

TRL inasema kuwa haipati faida kwenye njia za reli za Tanga-Moshi-Arusha, Kahe-Taveta, Kidatu-Kilosa na Dodoma-Singida.

 

Rais Kikwete amesema: “Kama ni mkopo lazima upatikane baada ya kuwa tumekubaliana sote wawili na wala siyo nyie kuchukua maamuzi pekee yenu kwa sababu mikopo yenyewe inalipwa na Serikali ya Tanzania. Na kama unataka msimamo wetu kuhusu maombi ya mkopo bila kutushirikisha, sisi basi ni kwamba hatuukubali mkopo huo.”

 

Kuhusu mipango ya uongozi wa TRL kuacha kutoa huduma kwenye baadhi ya vipande vya reli hiyo kwa sababu hakuna faida, Rais amesema:

 

Tumekodisha Reli nzima, siyo kwa vipande. Mlifanya uhakiki na kujua hali ya Reli nzima. Mlijua tokea mwanzo kwamba baadhi ya sehemu za Reli hiyo zilikuwa haziingizi faida. Hamwezi sasa kubadilika leo na kuweka msimamo tofauti.”

 

Kuhusu usalama wa Reli, Rais Kikwete amesisitiza: “Kuna uharibifu mkubwa katika baadhi ya maeneo ya Reli. Hali ya usalama wa Reli inaonekana kuwa hatarini kwa sababu nyie mnaonekana kama hamjali.”

 

Kuhusu ombi la kuzidi kupunguziwa kodi, Rais Kikwete ameuambia uongozi wa TRL: Hivi mnataka tuwaondolee kodi zote, ili sisi Watanzania tupata nini? Hivi mnataka tupate nini katika ubia huu? Sisi ndiyo tunakopa, ndio tunalipa madeni, na sasa mnataka hata tuwaondolee kodi.”

 

Ameongeza: “Mnataka tuwaondolee kodi zote ili tupate nini? Hivi mnaweza vipi kuhalalisha mpango wa namna hii kwa walipa kodi wetu? Tukifanya hivyo tuwaambie wananchi wetu nini? Kwamba nyie mpo hapa nchini kufanya nini hasa?”

 

Kuhusu hisia za kutaka kung’oa Reli kwa sababu ya kutokuwa na faida, Rais amesema: “Hili litachukuliwa kama hujuma. Kama hiyo ndiyo aina yenu ya fikra basi mtaiweka nchi yetu mahali pabaya, mtashindwa kuusaidia uchumi wetu kukua. Kung’oa sehemu yoyote ya Reli ni kutuambia kuwa hamuijali nchi hii na kwa kweli hatuwezi kuwa na washirika wa namna hiyo.  Haya ni mawazo ya kushangaza kabisa. Msiondoe hata kipande kimoja cha Reli.”

 

 

 

Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa Tanzania kuendelea kuwa na njia za reli zinazoungana na nchi nyingine za jirani. Tunahitaji mahusiano na nchi nyingine. Hatuwezi kufanya jambo la ovyo kiasi hicho.”

 

Kuhusu maelezo ya uongozi wa TRL kuwa imepeleka injini mbili ili zifanyiwe ukarabati nchini India kwa sababu za kiufundi, Rais amesema kuwa Serikali inataka kuona ukarabati wa mabehewa unafanyika katika karakana ya Reli iliyoko Morogoro na siyo kwingineko.

 

 

Imetolewa na:

 

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

 

16 Januari, 2009