DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail: press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amekitaka Chama cha Wanasheria nchini kutafuta njia za haraka kupunguza gharama za huduma ya sheria nchini ambazo amesema kuwa ni kubwa mno na zinawanyima wananchi wengi zaidi nafasi ya kupata huduma hizo kwa gharama nafuu zaidi.

 

Aidha, Rais Kikwete amekipongeza chama hicho cha Tanganyika Law Society (TLS) kwa kazi nzuri na ya miaka mingi ya kuwatumikia wananchi wa Tanzania kwa kuhakikisha kuwa wanapata huduma za kisheria.

 

Rais Kikwete alikuwa anafungua mkutano wa siku mbili wa nusu mwaka wa Chama hicho cha Tanganyika Law Society kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) mjini Dodoma leo, Ijumaa, Agosti 13, mwaka huu, 2010.

 

Rais Kikwete amewaambia wanasheria hao: “Kwa bahati mbaya, kupata haki ya kisheria katika Tanzania limebakia kuwa jambo ghali sana. Matokeo yake ni kwamba Watanzania walio wengi wanashindwa kupata haki yao hii ya msingi. Wanashindwa kumudu gharama za kupatiwa huduma ya kisheria wakati wanapoihitaji.”

 

Rais amesema kuwa hali hiyo ni lazima itafutiwe ufumbuzi wa haraka. “Hili ni jambo ambalo haliwezi kuachiwa kuendelea. Lazima zichukuliwe hatua kufuta picha iliyojengeka kwamba taaluma yenu ni ghali mno, haiendi kwa wakati na kwa kasi stahili na kuwa bado ina mapungufu makubwa katika kujali wenzetu katika jamii yetu wenye uwezo mdogo zaidi.”

 

Ameongeza Rais Kikwete: “Wananchi wengi wasiokuwa na uwezo miongoni mwetu wasiachiwe kupoteza matumaini yao ya kupata haki zao za kisheria katika nchi ambako hakuna ukosefu wa wanasheria.”

 

Rais Kikwete pia amewataka wanachama wa TLS kuchukua hatua za kukabiliana na masuala ya ukosefu wa maadili na nidhamu miongoni mwa wanataaluma wa chama hicho.

 

“Naambiwa kuwa chama hiki kina mfumo wa kushughulika na masuala ya nidhamu ya wanachama wake. Nasikitika kusema kuwa ukosefu wa ufanisi wa mfumo huu umewaacha watu wengi wakitoa malalamiko yao dhidi ya baadhi ya wanachama wenu wenye sifa mbaya bila kupata ufumbuzi wa matatizo haya,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

 

“Ukomavu wa kitaaluma wa chama chenu unazo nguvu za kutosha kuwawezesha kupambana na wale ambao wanachafua jina na heshima yenu nzuri ambayo ni matokeo ya kazi ya miaka mingi.”

 

Amesisitiza Rais Kikwete “Naambiwa kuwa kilio cha gharama kubwa za huduma ya kisheria kingeweza kupungua kama nyie wanachama wa TSL mngeendelea kuegemea na kufuata misingi yetu ya maadili na sheria zenu wenyewe kuhusu malipo ya huduma za kisheria, ambayo naambiwa kuwa inavunjwa zaidi kuliko kufuatwa.”

 

Imetolewa na:

 

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

 

13 Agosti, 2010