UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail: press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

SALAMU ZA RAMBIRAMBI ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE

 

            Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Eng. Dr. James Alex Msekela kutokana na ajali mbaya ya barabarani iliyotokea tarehe 9 Julai, 2010 na kusababisha, vifo vya watu 15 na wengine zaidi ya 40 kujeruhiwa katika kata ya Mnenia baada ya lori walilokuwa wakisafiria kwenda mnadani kupinduka.

 

            “Ni kwa majonzi na huzuni kuu, kupitia kwako wewe Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, ninawapa pole za dhati kabisa familia zilizopotelewa na ndugu zao katika ajali hiyo mbaya.  Ninawahakikishia kuwa nipo pamoja nao katika msiba huu mkubwa na namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema aziweke mahali pema peponi roho za marehemu wote, Amina”, amesema Rais Kikwete katika salamu zake hizo.

 

            Aidha, Rais Kikwete amesema anamuomba Mwenyezi Mungu awawezeshe watu wote waliojeruhiwa katika ajalai hiyo kupona haraka ili waungane tena na ndugu, jamaa na marafiki zao na kuendelea na maisha yao ya kawaida.

 

            Rais Kikwete ameendelea kuzisisitizia mamlaka zinazohusika na masuala ya usalama barabarani kuongeza umakini katika utekelezaji wa majukumu yao, kwani mojawapo ya sifa nzuri za mamlaka hizo ni uwezo wao wa kupunguza kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani au ikiwezekana kuondokana nazo kabisa.

 

Imetolewa na:

 

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

 

10 Julai, 2010