UNITED REPUBLIC OF
TANZANIA
DIRECTORATE OF
PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116539 E-mail: press@ikulu.go.tz Website: www.mawasilianoikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S
OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX
9120, DAR ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
SALAMU ZA
RAMBIRAMBI ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO
KIKWETE
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mheshimiwa John Mwakipesile kutokana na kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Bwana John Mwankenja.
Marehemu John Mwakenja alikufa kifo cha kikatili kwa kupigwa risasi jioni ya tarehe 19 Mei, 2011 wakati akiteremka katika gari lake mara tu baada ya kuwasili nyumbani kwake.
“Nimemfahamu Marehemu John Mwankenja enzi ya uhai wake kama kiongozi shupavu aliyekuwa na dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi wake kwa bidii na uaminifu mkubwa.” Amesema Rais Kikwete na kuongeza, “Kifo chake siyo tu kimeleta simanzi na huzuni kubwa kwa familia yake iliyokuwa inamtegemea kama mhimili na kiongozi wake, bali pia kimeacha pengo kubwa la uongozi kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe na Taifa kwa ujumla.”
Rais Kikwete amemuomba Mkuu huyo wa Mkoa kumfikishia salamu zake za pole kwa familiA ya Marehemu John Mwankenja kwa kumpoteza kiongozi wake muhimu huku akiihakikishia familia hiyo kuwa yupo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya mpendwa wao.
Amesema anamuomba Mola awajalie wafiwa moyo wa uvumilivu na ujasiri katika kipindi chote cha maombolezo ya msiba huo mkubwa.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu
DAR ES SALAAM.
20 Mei, 2011