UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116539

E-mail: press@ikulu.go.tz

Website:  www.mawasilianoikulu.go.tz  

Fax: 255-22-2113425

 

Coat of Arms

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

SALAMU za rambirambi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya Spice Islander na kuua watu 202 zimezidi kumiminika nchini kutoka Jumuia ya Kimataifa.

 

Salamu hizo za rambirambi pia zimetumwa kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein.

 

Hadi leo, Jumatano, Septemba 14, 2011, Mheshimiwa Rais Kikwete alikuwa ametumiwa salamu za rambirambi kutoka sehemu mbalimbali 22, zikiwemo zile kutoka kwa Mfalme wa Sweden Mfalme Carl Gustaf R, Gavana Mkuu wa Canada Mheshimiwa David Johnston, Waziri Mkuu wa Mauritius Mheshimiwa Dkt. Navinchandra Ramgoolam na Katibu Mkuu wa Umoja wa  Mataifa Mheshimiwa Ban Ki Moon.

 

Salamu nyingine zimepokelewa kutoka nchi za Benin, Philippines, Ukraine, Poland, Belarus, Misri, na Khazkistan.

 

Aidha, salamu nyingine zimetumwa kwa Mheshimiwa Rais Kikwete kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mama Asha Rose Migiro, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mheshimiwa Mohammed Babu, Balozi wa Tanzania katika Ufaransa Mama Begum Karim Taj, na Balozi wa Tanzania katika nchi za Misri Mheshimiwa Ali Shauri Haji ambaye pia anaiwakilisha Tanzania katika Israel, Jordan, Libya, Lebanon, Syria na Palestine.

 

Mheshimiwa Rais Kikwete pia amepokea salamu za rambirambi kutoka kwa Kaimu Balozi wa Tanzania katika Oman Mheshimiwa Abdallah Abasi Kilima, Balozi wa Tanzania katika India Mhandisi John H. Kijazi, Balozi wa Tanzania katika Canada Mheshimiwa Alexander C. Masinda na Balozi wa Tanzania katika Brazil Mheshimiwa Francis Malambugi.

 

Salamu pia zimepolekewa kutoka kwa Katibu Mtendaji wa International Conference on the Great Lakes Region Balozi Liberata Mulamula na kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Mazao (Common Fund for Commodities), Mheshimiwa Ali Mchumo.

 

Meli ya Spice Islander ilizama kwenye pwani ya Zanzibar katika eneo la Nungwi usiku wa kuamkia Jumamosi, Septemba 10, mwaka huu, 2011 na mpaka sasa watu 202 wamethibitishwa kuwa walipoteza maisha katika ajali hiyo na wengine 619 waliokolewa katika ajali hiyo.

 

Hadi sasa meli hiyo iliyokuwa inasafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Pemba kupitia Zanzibar haijaweza kuopolewa  kutoka baharini hata kama wazamiaji wa ndani na kutoka Afrika Kusini wanaendelea na kazi ya kuitafuta meli hiyo.

 

Imetolewa na:

 

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

 

14 Septemba, 2011