UNITED
REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF
PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
|
Telephone:
255-22-2114512, 2116539 E-mail: press@ikulu.go.tz Website: www.mawasilianoikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S OFFICE,
THE STATE HOUSE, P.O. BOX 9120, DAR ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa ukosefu
wa ajira kwa vijana wa
Afrika ni jambo kubwa, linalohitaji
majawabu makini na ya haraka
na hatua kubwa zisizohitaji kucheleweshwa tena kutoka kwa viongozi
wa Bara hilo.
Aidha, Rais Kikwete amesema
kuwa uharaka wa kupata
majawabu ya tatizo hilo yanatokana
na ukweli kuwa kila nchi
ya Afrika inazalisha jeshi kubwa la vijana wasiokuwa na ajira
wanaoingia katika soko la ajira kila
mwaka baada ya kumaliza shule.
Rais Kikwete ametoa rai hiyo nzito
na kubwa kwa viongozi wenzake
wa Afrika jioni ya jana,
Alhamisi, Desemba 15, 2011,
wakati alipokuwa anashiriki katika mjadala kuhusu mada ya Ukatili
wa Kijinsia katika nchi za
eneo la Maziwa Makuu kwenye siku
ya kwanza ya mkutano wa mwaka
huu wa wakuu
wa nchi wanachama
wa eneo hilo.
Mkutano huo wa siku
mbili kwenye ukumbi wa Hoteli
ya Munyonyo Commonwealth
Resort, nje kidogo ya mji mkuu
wa Uganda wa Kampala, unawashirikisha wakuu wa nchi na
Serikali pamoja na wawakilishi wa nchi 11 za
Umoja wa Nchi za Maziwa
Makuu wa International
Conference on Great Lakes Region (ICGLR).
Wakati wa mjadala wa
mada hiyo, suala la ukosefu wa ajira kwa
vijana wa Afrika na athari
lake lilijitokeza kutokana na moja ya
mapendekezo ya azimio la mada hiyo ya Ukatili
wa Kijinsia na ndipo Rais
Kikwete alipoingia katika mjadala huo na kuwaambia
wakuu wenzake wa nchi na
Serikali:
“Suala hili la ukosefu wa ajira
kwa vijana wetu katika Afrika
ni suala kubwa sana na
linalohitaji majawabu ya haraka na
majibu makini kutoka kwetu sote
tuliopewa wajibu wa kuongoza nchi
zetu. Tunao wajibu wa
kutafuta na kupata majawabu sahihi ya tatizo
hilo.”
Kuhusu pendekezo kuwa wakubwa wa
ICGLR wajadili tatizo hilo katika kikao
kijao cha wakuu wa nchi hizo
katika miaka miwili ijayo mjini
Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Rais Kikwete amewaambia
wakuu wa nchi na Serikali
wenzake:
“Suala
hili ni suala
la haraka. Linahitaji mjadala wa
kina na makubaliano makini na majawabu
sahihi ya jinsi ya kupambana
na jeshi la vijana linaloingia katika soko la ajira kutoka shule
na vyuoni kila mwaka. Hatuwezi waheshimiwa
viongozi kuendelea kusubiri miaka miwili kujadili suala hili.”
Kufuatilia pandekezo lake, viongozi hao wa ICGLR wamekubaliana
kuwaagiza mawaziri wao wanaohusika na ajira na
sekta zinazohusiana na ajira kukutana
haraka katika muda wa miezi
sita ijayo kujadili na kutoa
mapendekezo kwa Serikali za nchi
wanachama wa ICGLR kuhusu namna gani
nchi hizo zinaweza kukabiliana na changamoto hiyo
ya ukosefu wa ajira kwa
vijana na hata watu wengine.
Marais sita wanawakilisha nchi zao katika mkutano
huo wa
siku mbili. Mbali na Rais Kikwete,
viongozi wengine wanaohudhuria mkutano huo ni Rais
Yoweri Museveni, mwenyezi wa mkutano
huo na mwenyekiti
mpya wa ICGLR, Rais Michael Sata wa Zambia ambaye amemaliza muda wake wa uenyekiti wa
Umoja huo, Rais Mwai Kibaki
wa Kenya, Rais Pierre Nkurunzinza wa Burundi na Rais Francois Bozize wa Jamhuri
ya Afrika ya Kati (CAR).
Nchi nyingine wanachama wa ICGLR zilizowakilishwa
na viongozi wengine waandamizi ni pamoja na
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Jamhuri ya Congo (Brazzaville),
Rwanda, Angola na Sudan. Mkutano
huo umepangwa kumalizika jioni ya leo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Safarini, Kampala.
16
Desemba, 2011