DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail: press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

 

Na Mwandishi Maalum

 

 

Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Tanzania inapenda kufanya mazungumzo ya haraka, ili kuona jinsi gani ya kufikia makubaliano juu ya deni la dola za Marekani milioni 128.05 ambazo Tanzania inadaiwa na Algeria.

 

Ili kuanzisha mazungumzo hayo, Rais Kikwete amemwambia Balozi wa Algeria, anayemaliza muda wa utumishi wake katika Tanzania, Bwana Abdelmoun’aam Ahriz kuwa atawatuma mawaziri wawili kwenda Algeria kukutana na wenzao.

 

Nitawatuma Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, pamoja na Waziri wa Fedha na Uchumi, kwenda Algeria kufanya mazungumzo ya jinsi ya kufikia  mwafaka kuhusu deni hilo la muda mrefu,” Rais Kikwete amemwambia Balozi huyo ambaye anamaliza muda wake wa kuiwakilisha nchi yake katika Tanzania.

 

Kati ya deni hilo ambalo Algeria inaidai Tanzania, kiasi cha dola za Marekani milioni 58.03 ni deni lenyewe, na kiasi cha dola za Marekani 70,02 ni riba. Deni hilo linatokana na Algeria kuipatia Tanzania mafuta katika miaka ya nyuma.

 

Tokea mwaka 2004, nchi hizi mbili zimekuwa zinajadiliana jinsi ya kumaliza deni hilo, na mwaka 2006, wakati Rais Kikwete alipokutana na Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika Banjul, Gambia, kiongozi huyo wa Algeria alionyesha dalili kuwa Algeria ilikuwa tayari kulifuta deni hilo.

 

Balozi Ahriz anayeondoka nchini Ijumaa, wiki hii, amekuwa Balozi wa Algeria katika Tanzania tokea Desemba 2005.

 

Rais Kikwete pia amesema kuwaTanzania na Algeria zimekuwa na uhusiano mzuri kwa miaka mingi na zimekuwa na misimamo inayokubaliana kuhusu masuala mbalimbali ya kimataifa likiwamo lile la kuitaka Morocco kuipatia  Sahara Magharibi uhuru wa kujiamulia mambo yake yenyewe.

 

Rais Kikwete pia ameishukuru Algeria kwa kuendelea kutoa nafasi za masomo kwa wanafunzi wa elimu ya juu wa Tanzania. Mpaka sasa, nchi hiyo imetoa nafasi 441 za masomo ya elimu ya juu katika nyanja za ufamasia, utalii, udaktari, lugha, uhandisi wa maji, na kwenye masomo ya Kiislamu na Kifaransa.

 

Balozi Ahric amesema kuwa mwaka huu, nchi hiyo imetoa nafasi 60 kwa wanafunzi wa Tanzania kwenda kusoma katika Algeria.

 

 

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

 

03 Novemba, 2009