DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail: press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo, Jumanne, Machi 16, 2010, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Finland, Mheshimiwa Matti Vanhanen kuhusu masuala mbalimbali.

 

Mheshimiwa Vanhanen yuko katika ziara ya siku nne nchini kwa mwaliko wa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda. Ziara hiyo inalenga kuimarisha uhusiano wa miaka mingi kati ya Tanzania na Finland.

 

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, viongozi hao wawili wamejadili hali ya uhusiano kati ya Tanzania na Finland, hali ya kisiasa ilivyo katika Afrika, na kuhusu masuala ya kimataifa likiwemo suala muhimu la tabianchi.

 

Rais Kikwete ameishukuru Finland kwa misaada yake ya miaka mingi kwa Tanzania katika sekta za elimu, mazingira, kilimo, utawala bora, mageuzi ya Serikali za Mitaa, na nguvu za umeme.

 

Rais Kikwete pia amemwelezea Waziri Mkuu huyo kuhusu hali ya kisiasa ilivyo nchini na kumhakikishia kuwa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu yanakwenda vizuri.

 

 

Rais pia ameishukuru Serikali ya Finland kwa uamuzi wake wa kujenga chuo cha maendeleo cha Dar es Salaam Institute for Sustainable Development, chuo ambacho ufunguzi wake rasmi umefanyika wakati wa ziara ya Waziri Mkuu huyo.

 

Naye Mheshimiwa Vanhanen amemwambia Rais Kikwete kuwa ni vizuri kuona Tanzania inaendelea kuwa mfano wa amani na utawala bora katika Bara la Afrika ambalo kwa muda mrefu limekabiliwa na migogoro mingi, baadhi yao ikiwa mikubwa.

 

“Huwezi kujenga taifa imara bila utawala bora na Tanzania ni moja ya mifano ya jinsi utawala bora unavyoweza kutuliza nchi,” amesema Waziri Mkuu huyo.

 

Imetolewa na:

 

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

 

16 Machi, 2010