DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail:  ikulumawasiliano@yahoo.com

              press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

Coat of Arms

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais Jakaya Kikwete  amepanda miti katika maeneo ambayo patasimikwa mitambo ya kuzalisha umeme katika wilaya za Kasulu na Kibondo Mkoani Kigoma.
"Mkoa wa Kigoma umekuwa na matatizo ya umeme kwa muda mrefu tuaminiane, tuvumiliane ahadi yetu iko pale pale, kumaliza tatizo la umeme Kasulu na Kibondo" Rais amewambia wananchi wa Kasulu jana (16/06/2010) wakati wa ziara ya kikazi katika wilaya hizo mbili ambapo yuko kwa shughuli za kukagua maendeleo na kuona hatua zilizofikiwa katika kutatua kero mbalimbali za wananchi Mkoani Kigoma.

Mitambo hiyo miwili, kila mmoja una uwezo wa kuzalisha megawati mbili na nusu na inategemewa kuanza uzalishaji mwishoni mwa mwaka huu.
Katika ahadi yake hiyo ya kufikisha umeme katika makao makuu ya wilaya, itatimizwa pia katika wilaya za Bukombe, Longido, Nkasi, Nanyumbu, Namtumbo na  Ngorongoro.


Zote hizi zitapewa huduma ya umeme ndani ya bajeti hii ambayo ni ya mwisho kabla ya kufanyika tena kwa uchaguzi mkuu nchini.
Rais amewambia wananchi wa Kasulu kuwa serikali pia imedhamiria kuzalisha umeme kutoka Mto Malagalasi ambao utaongezea katika mahitaji mkoani humo hadi katika vijiji.

Miradi ya umeme katika mikoa hii miwili inafadhiliwa na fedha za serikali ambapo mradi wa Kasulu umegharimu Tshs Bil 7.2 na wa Kibondo shilingi Bil 7.9 ambapo mkandarasi ameanza kupeleka vifaa kwenye eneo.

Rais Kikwete amesema kero hizi kubwa zimefanya wananchi wa Kigoma kuona kuwa wametengwa.  Rais Kikwete pia amefanya ukaguzi wa ujenzi wa barabara unaoendelea mkoani humu ambapo amewaeleza wananchi wa Kasulu kuwa mbali na kuunganisha mikoa yote nchini kwa barabara za lami, serikali pia itaunganisha nchi yetu na nchi jirani kwa barabara za lami.

"Mwaka huu wa fedha ujenzi wa barabara utaendelea hadi Kasulu na mwakani tutaenda hadi Kibondo”. Rais amesisitiza.

Ahadi zingine kwa mkoa wa Kigoma ni utatuzi wa kero za maji na Rais amezindua mradi wa maji wa Mkongoro II.

Rais anamalizia ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani kigoma leo tare 17 Juni, 2010 na kuelekea Wilaya ya  Mpanda, mkoani Rukwa.


Mwisho.

Imetolewa na Premi Kibanga,

Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais,

Safarini Kigoma.

17 Juni, 2010