DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail:  ikulumawasiliano@yahoo.com

              press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

Coat of Arms

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

Serikali inatarajia kuanzisha Benki ya Kilimo nchini ili kuweza kutoa mikopo kwa wakulima nchini.

 

Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema hayo jana  katika uwanja wa Nelson Mandela katika Manispaa ya Sumbawanga akitokea Namanyere wilayani Nkasi.

 

Tunahangaika kuanzisha Benki ya Kilimo ili tuweze kuwakopesha wakulima waweze kuendeleza Kilimo chao kwa njia za kisasaRais amesema na kueleza kuwa serikali imezungumza na serikali ya China ili kupata kianzio cha Benki.

 

Rais amesema katika Kilimo Kwanza, shabaha ya kwanza ni kujitosheleza kwa chakula na hivyo hakuna budi kuongeza matumizi ya maji, mbegu bora na mbolea.

 

Rais Kikwete pia ameelezea jitihada za serikali za kupata mbegu bora ambazo zimezalishwa kitaalamu na kulingana na mazingira ya nchi yetu.

 

Rais amewaasa wananchi wa Rukwa kutafuta mawakala wa mbolea walio waaminifu baada ya serikali kuwaondoa watumishi wake wasio waaminifu.

 

Hawa watumishi wa serikali wameshirikiana  na mawakala wasio waaminifu, mawakala ni wenu hangaikeni nao msifanye kazi ya kuendelea kuwanufaisha, hilo liko kwenye mamlaka yenu,” Rais amesema.

 

Rais Kikwete pia amewapongeza wananchi wa Rukwa kwa kujenga nyumba za walimu 1460 za walimu kutoka 400 zilizokuwepo awali.

 

Rais amezishauri taasisi zinazotoa matangazo yanayokosoa serikali kuwa zimejenga shule za walimu kidogo na kuwashauri watoa matangazo hao kufanya utafiti badala ya kupotosha na kudanganya watu kama kweli wana nia nzuri, na ikibidi watembelee mikoa ya Rukwa na Kigoma ambapo nyumba za walimu zimejengwa kwa wingi.

 

Mapema jana asubuhi Rais alifungua soko la mazao katika makao makuu ya wilaya ya Nkasi, Namanyere na baadaye kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya lami kutoka Sumbawanga-Kanazi-Kizi-Kibaoni, yenye jumla ya urefu wa kilometa 151.6.

 

Ujenzi wa barabara hii ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2005 inayoelekeza kujenga barabara za lami zinazounganisha makao makuu ya mikoa yote nchini.

 

Barabara hii inaunganisha makao makuu ya Mkoa wa Kigoma na Tabora kupitia Mpanda na lengo la serikali ni kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Sumbawanga-Kanazi-Kizi-Sitalike-Mpanda, Mpanda-Inyonga-Koga-Ipole hadi Tabora na Mpanda-Uvinza-Kanyani hadi Nyakanazi. Kwa upande wa sehemu ya Mpanda-Inyonga-Koga-Ipole-Tabora, usanifu unaendelea na unatarajiwa kukamilika Januari 2011.

 

Mara baada ya kuzungumza na wananchi, Rais alizindua rasmi ujenzi wa barabara ya Sumbawanga-Matai-Kasanga Port yenye urefu wa kilometa 112 inayogharamiwa na serikali ya Tanzania kwa asilimia mia moja.

 

Leo Rais Kikwete anaweka jiwe la msingi  kituo cha umeme katika manispaa ya Sumbawanga na kuzindua maabara ya hospitali ya Sumbawanga na kusalimia wananchi wa Usevya na baadaye kuelekea Mkoa wa  Kagera kuhudhuria maadhimisho ya Karne ya Injili ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini Magharibi na Dayosisi ya Karagwe.

 

Mwisho.

 

Imetolewa na Premi Kibanga,

Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,

Sumbawanga

Rukwa.