DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail:  ikulumawasiliano@yahoo.com

              press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

 

 

Miradi ya maendeleo iliyokubaliwa kati ya Tanzania na Marekani chini ya Mpango wa Millenium Challenge Corporation (MCC) imefikia hatua kubwa na utekelezaji wake unatarajia kuanza hivi karibuni.

 

Balozi wa Marekani Alfonso Lenhardt amemueleza Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo asubuhi (Machi 25, 2010) alipofika Ikulu kumpa taarifa ya maendeleo ya makubaliano hayo ambapo kiasi cha Dola milioni 698 zimetolewa na Marekani kwa Tanzania na kutiwa saini.

 

Miradi hiyo ni ya barabara, Nishati na Maji ambapo tayari mjenzi wa barabara ya Tanga - Horohoro yuko katika eneo la ujenzi, Laela -Sumbawanga, Songea - Namtumbo ambazo  uchambuzi wa zabuni umeshaanza na wakandarasi wanatarajiwa  kuteuliwa Mwezi April, 20010.

 

Miradi mingine ni Tunduma – Ikana - Laela na Peramiho - Mbinga ambapo taratibu za zabuni zimeanza na zoezi la uchambuzi litaanza mwezi ujao.

 

Katika mradi wa Pemba, tayari nyaraka za zabuni zinatayarishwa na taratibu za fidia kwa wananchi zimeanza kuchambuliwa.

 

Katika miradi ya Nishati, mradi wa kusambaza umeme (Zanzibar Cable) taratibu zimeshafanyika na inatarajiwa kwamba shughuli ya kutiliana saini kati ya mkandarasi na serikali itafanyika mwezi ujao.

 

Katika mradi wa usambazaji wa Umeme katika mikoa 6 ya Tanzania Bara, taratibu za kumpata mzabuni  zimeshaanza ambapo mikoa ya Dodoma, Iringa, Mbeya, Morogoro, Mwanza na Tanga itafaidika na mradi huu utakapokamilika.

 

Balozi Lenhardt alikuwa ameambatana na Mkurugenzi Mwakilishi  hapa Tanzania Bw. Karl Fickenscher ambapo pia amemueleza Rais Kikwete kuwa miradi ya maji ya Ruvu Chini na mkoani Morogoro,  wajenzi wameshaanza kuorodheshwa na zoezi la kuandaa zabuni limeanza

 

Katika kikao hicho balozi Lenhardt amemueleza kuwa kufuatia Mazungumzo kati ya Rais Kikwete na Rais Obama mwaka jana, Marekani imeiteua Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 6 za Afrika zitakazofaidika na msaada wa kuendeleza sekta ya Kilimo katika jitihada za kuwa na usalama wa chakula.

 

Balozi pia amemueleza Rais Kikwete kuwa Marekani itatoa msaada wa ujenzi na ukarabati wa Reli ya Kati, Rais Kikwete amefurahishwa na msaada huo ambapo ameelezea kuwa huo ni mchango mkubwa kwa maendeleo na uchumi wa Tanzania kwani reli yetu kwa sasa ni ya zamani na finyu sana. Kufuatia msaada huu, mazungumzo kati ya serikali ya Tanzania na Marekani yanatarajiwa kuanza mara moja.

 

Katika mazungumzo hayo Marekani pia itaendeleza programu yake ya kuisaidia Tanzania katika mapambano ya Ugonjwa wa Ukimwi kwa muda wa miaka mitano ijayo ambapo serikali ya Marekani imetenga dola milioni 338 kwa mwaka.

 

Akielezea kuhusu mpango huo, Mkurugenzi wa Shirika la  Misaada la Marekani (USAID) hapa nchini Bwana Robert Cunnane amesema USAID itashirikiana na Wizara ya Afya nchini ili kuelekeza msaada huo katika jitihada za kitaifa za kupambana na Ukimwi.

 

Marekani imekuwa mstari wa mbele katika kuisaidia Tanzania katika jitihada hizi ambapo watu wengi zaidi wameweza kupata huduma za kupima na dawa za kupunguza makali.

 

Mambo mengine yaliyojadiliwa katika kikao hicho ni msaada kutoka marekani katika kupambana na maharamia katika bahari ya Hindi na kutoa msaada wa utaalamu na stadi za kuchimba na kuendeleza madini ya uranium hapa nchini ambayo yamegunduliwa huko kusini mwa Tanzania.

 

 

Imetolewa na:

 

Premi Kibanga,

Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

 

25 March, 2010