UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116539

E-mail: press@ikulu.go.tz

Website:  www.mawasilianoikulu.go.tz  

Fax: 255-22-2113425

 

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amekialika Kituo cha Ushirikiano wa Nchi Zinazoendelea cha South Centre cha Uswisi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kuazimisha miaka 50 ya uhuru inayosheherekewa mwaka huu.

Rais Kikwete ametoa mwaliko huo leo, Jumanne, Januari 25, 2011, wakati alipotembelea Kituo hicho kilichoko mjini Geneva akakutana na kuzungumza na wajumbe wa Bodi na wafanyakazi wa Kituo hicho kilichoko chini ya uenyekiti wa Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa. Kituo hicho kilianzishwa chini ya uongozi na uenyekiti wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere katika miaka ya 1980.

Rais Kikwete amewasili mjini Geneva asubuhi ya leo kwa ajili ya kuendesha kikao cha kwanza cha Tume ya Kimataifa ya Kuzungumzia Afya ya Akinamama na Watoto kinachofanyika kesho.

Rais Kikwete ametoa mwaliko huo baada ya kusikiliza maoni ya baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Kituo hicho, akiwamo Chifu Emeka Anyaoku wa Nigeria na Rais Mkapa ambao wote walisema kuwa njia bora zaidi ya kukumbuka uongozi wa mwalimu na mchango wake kwa Tanzania, Afrika, na Jumuia ya kimataifa ni kwa South Centre kushiriki kikamilifu katika sherehe za miaka 50 za taifa alilolianzisha.

“Nakubaliana nanyi kuwa miaka 50 ya uhuru wetu ni miaka ya kusherehekea Kumbukumbu ya Maisha ya Mwalimu Nyerere na yote ambayo ametufanyia sote – sisi Watanzania, sisi Waafrika, sisi wana-jumuia ya kimataifa,” amesema Rais Kikwete katika mkutano na Bodi hiyo na wafanyakazi wote wa South Centre.

Rais Kikwete amekipongeza Kituo cha South Cenre kwa kazi nzuri inayofanywa na kituo hicho katika kutetea maslahi ya nchi masikini zinazoendelea duniani kuhusu masuala mbali mbali ya kimataifa na kusisisitiza kuwa kituo hicho kinafuata kikamilifu nyayo za kweli kweli za Mwalimu Nyerere.

Rais ameambiwa katika kituo hicho kuhusu masuala muhimu ambayo yamekuwa yanashughulikiwa na Kituo hicho katika miaka mitatu iliyopita.

Masuala hayo ni pamoja na Mikataba ya Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA) isiyokubalika kati ya nchi za Afrika na Carribbean, na zile za Umoja wa Ulaya (EU); zahama ya kiuchumi duniani; suala la hatimiliki, hasa zile za dawa ambazo zinatishia kupandisha sana bei ya dawa za binadamu duniani kwa namna ambayo hazitaweza kununuliwa na watu masikini; pamoja na suala la mabadiliko ya tabianchi lililoanza kuziathiri nchi masikini zaidi kuliko zile tajiri hata kama mchango wa nchi masikini katika kuvuruga mazingira na mabadiliko ya tabia nchi ni mdogo.

Akizungumza kwenye mkutano huo uliofanyika kwenye makao makuu ya Kituo hicho cha South Centre, Chifu Emeka Anyaoku amemwelezea Rais mstaafu Mkapa kama mwenyekiti aliyefufua moyo wa Mwalimu katika maendeleo ya kituo hicho, na akamweleza Rais Kikwete kama “mfuasi asiyepingwa wa Julius Mwalimu Nyerere”.

Rais Mkapa ni mwenyekiti wa tano wa Bodi ya Kituo hicho ambacho mwenyekiti wake wa kwanza alikuwa Mwalimu Nyerere. Wengine ambao wamekuwa wenyeviti wa Bodi ya Kituo hicho ni Luis Fernando Jaramilla wa Colombia, Gamani Corea wa Sri Lanka na Boutros Boutros Ghali wa Misri ambaye pia amepata kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

 

Mwisho.

Imetolewa na:

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais

Safarini, Geneva.

25 Januari, 2011