DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
UNITED
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116898 E-mail : press@ikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA YA SERIKALI KWA VYOMBO VYA
HABARI KUHUSU KUSUDIO LA WALIMU LA KUTAKA KUGOMA
1. Tarehe 13 Oktoba, 2008 Mahakama Kuu,
Divisheni ya Kazi ilitoa amri ya kusitisha mgomo usiokuwa na ukomo wa walimu
uliokuwa umekusudiwa kuanza tarehe 15 Oktoba, 2008 na kuendelea, ili kutoa
fursa kwa majadiliano yaliyokuwa yanaendelea kati ya Serikali na Chama cha
Walimu Tanzania (CWT) kufikia ufumbuzi.
CWT hawakuridhika na uamuzi huo hivyo walipeleka maombi yao ya marejeo
ya uamuzi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi kwenye Mahakama ya Rufani. Katika
maombi yao hayo, walidai kuwa Mahakama Kuu ilisikiliza shauri ambalo lilikuwa
limepelekwa mbele ya Mahakama ile chini ya Kifungu kisichokuwa sahihi
kulingana na maombi
husika.
2. Mahakama ya Rufani, katika uamuzi wake
kuhusu suala hilo ulioandaliwa tarehe 11 Novemba, 2008 na kusomwa tarehe 13
Novemba, 2008, ilikataa maombi ya CWT ya kutaka kurejewa kwa uamuzi wa Mahakama
Kuu na kuelekeza kuwa walipaswa kukata rufaa badala ya kuomba marejeo.
3. Hata hivyo, Mahakama ya Rufani, kwa
kutumia mamlaka yake yenyewe iliamua pia kuwa maombi ya Serikali
yaliyowasilishwa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, yalikuwa yamewasilishwa
kupitia Kifungu cha Sheria kisicho sahihi. Kwa sababu hiyo, Mahakama ya Rufani
ilifuta mwenendo wote pamoja na maamuzi juu ya shauri lile.
4. Ni vema isisitizwe hapa kwamba Mahakama
ya Rufani haikutamka kwamba mgomo usio na kikomo uliokusudiwa kuanzishwa na CWT
ulikuwa halali na wala haikuruhusu kufanyika kwa mgomo huo.
5. Baada ya uamuzi huo wa Mahakama ya
Rufani, Serikali imepata taarifa ya Tamko la CWT la tarehe 14 Novemba, 2008
lililotolewa na Mwal. Gratian Mukoba, Rais wa CWT kupitia vyombo vya habari
kwamba, pamoja na mengineyo, wanachama wa CWT wataanza mgomo wao usio na kikomo
siku ya Jumatatu tarehe 17 Novemba, 2008.
Pia katika tamko
lao, CWT wametoa mapendekezo ya namna ya kuboresha zoezi la uhakiki wa madai ya
madeni yao linaloendelea ambayo wanaitaka Serikali
kuyafanyia kazi.
6. Serikali kwa upande wake imeendelea
kulipa madai mbalimbali ya walimu na watumishi wengine kwa mujibu wa taratibu
zilizopo. Aidha, Mheshimiwa Rais katika
hotuba yake ya mwisho wa mwezi kwa Taifa ya tarehe 31 Oktoba 2008, alielekeza
na kuahidi kuwa Serikali italipa madeni yote ya walimu yaliyohakikiwa. Maelekezo ya Mhe. Rais yalirejewa tena na
Mhe. Waziri Mkuu tarehe 7 Novemba, 2008 alipokuwa akitoa hoja ya kuahirisha
Mkutano wa 13 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuahidi kwamba
Serikali itakamilisha uhakiki huo mapema iwezekanavyo. Serikali hivi sasa inakamilisha zoezi la
uhakiki wa madeni ya walimu na italipa madeni yote yaliyohakikiwa ifikapo tarehe
30 Novemba 2008. Kuanzia tarehe 17 Novemba, 2008, Wizara ya Fedha na Uchumi
itaanza kupeleka fedha kwenye Halmashauri zote 133 tayari kwa malipo. Kwa hiyo,
Serikali inawataka walimu kuwa na subira kwani kwa hatua hizi zinazochukuliwa
na Serikali hatuoni busara ya walimu kugoma.
7. Walimu ni watumishi wa umma, na kama
ilivyo kwa watumishi wote wa umma, masuala yahusuyo mgomo lazima kwanza yawe
yameshughulikiwa na kukamilika chini ya Sheria ya Majadiliano ya Pamoja Katika
Utumishi wa Umma Na. 19 ya mwaka 2003 ambayo imeweka masharti yanayohitaji
kutimizwa kabla ya watumishi kugoma. Katika kusudio la walimu la kutaka kugoma,
baadhi ya masharti hayakutimizwa na ndio maana Serikali inapinga mgomo batili
usio na kikomo unaokusudiwa.
Tayari Serikali
imekwishawasilisha katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi Maombi Anuai Na. 21
ya 2008 kuiomba Mahakama Kuu izuie mgomo usio na kikomo unaokusudiwa. Aidha, CWT wamepelekewa samansi ya kuitwa
Mahakamani kwa ajili ya shauri hilo la maombi anuai ambalo limepangwa
kusikilizwa tarehe 17 Novemba, 2008.
8. Kutokana na hatua hizi zinazoendelea
kuchukuliwa, Serikali inakitaka Chama cha Walimu kufanya yafuatayo:-
•
Kusitisha
mgomo wao usio na ukomo unaokusudiwa kuanza tarehe 17 Novemba 2008, kwa kuwa
tayari Serikali inashughulikia kwa ukamilifu madai ya madeni yao.
•
Serikali
inawashauri CWT wawasilishe rasmi Serikalini mapendekezo yaliyo kwenye tamko
lao, kuhusu namna ya kuboresha zoezi la uhakiki wa madai ya madeni ya walimu,
na Serikali iko tayari kuyafanyia kazi. Serikali inaamini kwamba iwapo mgomo
utaendelea, utainyima fursa ya kushughulikia mapendekezo ya CWT yaliyo katika
tamko lao.
9. Kwa kuwa mgomo unaokusudiwa haukutimiza
masharti yote yaliyotajwa katika Sheria ya Majadiliano ya Pamoja katika
Utumishi wa Umma, mgomo huo machoni mwa Serikali kama mwajiri ni batili na
walimu watakaoshiriki kwenye mgomo huo wanaweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu
kwa mujibu wa sheria hiyo. Aidha, kwa mujibu
wa Sheria ya Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004 mtumishi atakayeshiriki kwenye
mgomo batili, hatalipwa mshahara na Serikali, kama mwajiri kwa kipindi chote
cha mgomo. Itabidi mshahara wake ulipwe
na aliyeitisha mgomo huo.
10. Ikumbukwe kuwa tayari suala hili liko
Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, hivyo walimu hawapaswi kugoma kwa sababu
kufanya hivyo ni kuishinikiza mahakama kutoa maamuzi ambayo walimu wanayataka,
kitendo kinachoingilia uhuru wa mahakama.
Mgomo huo hauna maslahi kwa umma na hata kwa walimu wenyewe kwa sababu
unakusudiwa kufanyika katika kipindi ambacho wanafunzi wanapaswa kufanya mitihani
yao ya kuvuka madarasa au vidato.
11. Hivyo, kwa kuwa Serikali inayafanyia kazi
madai ya madeni ya walimu, na kwa kuwa mgomo unaokusudiwa kufanyika ni batili
na usio na maslahi yoyote kwa Taifa, Serikali inawataka CWT kusitisha kusudio
lao la kufanya mgomo usio na kikomo uliopangwa kuanza tarehe 17 Novemba, 2008
na kuwataka walimu wote kuendelea na kazi zao kama kawaida.
(Phillemon L.
Luhanjo)
KATIBU MKUU
KIONGOZI NA
MKUU WA UTUMISHI WA
UMMA
15 Novemba, 2008