DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
UNITED
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116898 E-mail : press@ikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM. Tanzania. |
MHESHIMIWA RAIS
AMEFURAHISHWA NA HATUA YA
SERIKALI YA SUDAN YA KUANZISHA MCHAKATO WA KUMALIZA VITA.
Mwenyekiti wa Umoja
wa Afrika (AU), Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa amefurahishwa na hatua
zinazochukuliwa na Serikali ya Sudan wa kuanzisha mchakato wa kumaliza vita ya
Darfur.
Rais Kiwete pia
ameitaka Serikali hiyo ya Rais Omar El Bashir kutafuta njia za haraka kuanzisha majadiliano ya waasi nchini humo
kama njia ya kuleta amani ya kudumu katika Sudan.
Rais Kikwete
ameelezea matumaini yake hayo ya kukomeshwa kwa vita na zahama ya kibinadamu
katika Darfur wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na mjumbe maalum wa Rais
Bashir, Dk. Mustafa Osman, ambaye ni mshauri maalum wa kiongozi huyo wa Sudan.
Katika mazungumzo
hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam, Dk. Osman ambaye amefuatana na Waziri
wa Sheria wa Sudan, Sabidarat, mjumbe huyo maalum wa Rais Bashir amemwelezea
Rais Kikwete hatua ambazo zimekuwa zinachukuliwa na uongozi wa nchi hiyo
kumaliza vita ya Darfur ambayo imesababisha vifo vya maelfu ya watu.
“Nafurahi kusikia
kuwa mmeanzisha mchakato wa ndani kujaribu kumaliza matatizo ya Darfur.
Hatimaye, majibu ya mambo haya yote yako mikononi mwenu. Hii ni nchi yenu. Kazi
yetu sisi ni kuwaungeni mkono,” amesema Rais Kikwete.
Viongozi hao wawili
pia wamejadili kuhusu hati ya kukamatwa kwa Rais Bashir iliyotolewa na Mahakama
ya Kimataifa ya Uharifu (ICC) na athari zake katika kutafuta ufumbuzi wa
mgogoro wa Darfur. ICC inataka Rais Bashir akamatwe na kushitakiwa kwa uharifu
wa kivita.
Mjumbe huyo maalum
wa Rais Bashir pia amemwelezea Rais
Kikwete kuhusu hali ya uhusiano ilivyo kati ya Sudan na Chad na juhudi ambazo
zimekuwa zinafanyika kuondoa vikwazo vinavyosababisha mvutano kati ya nchi hizo
mbili.
Mwisho.
Imetolewa na
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais
Ikulu.
Dar es Salaam.
14 Novemba, 2008