DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail:  ikulumawasiliano@yahoo.com

              press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

Serikali ya Awamu ya Nne imeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma ya afya karibu na makazi yao na iliyo bora zaidi.

 

Rais Jakaya Mrisho Kikwete amemweleza Rais wa Zamani wa Ireland, Bi Mary Robinson wakati wa mazungumzo leo asubuhi.

 

“Lengo letu ni kuboresha huduma ya afya kwa kuongeza huduma bora, kuboresha hospitali, zahanati na vituo vilivyopo na pia kujenga zingine kwa lengo la kuhakikisha kuwa huduma za afya zinapatikana si zaidi ya kilomita tano kutoka wananchi wanapoishi” ameeleza.

 

Bi Robinson ni mwanzilishi wa shirika lisilo la kiserikali la “Realising Rights” ambalo lengo lake kubwa ni kuhakikisha kuwa haki ya huduma ya afya inapatikana kwa watu watabaka la chini kote duniani na pia upatikanaji  wa ajira zenye staha kwa binadamu.

 

Bi Robinson hufanya shughuli za kuhamasisha washika dau wakiwemo viongozi wa kiserikali, wafanya biashara na viongozi wengine katika nyanja mbalimbali kutafuta njia na mbinu za kusaidia katika kufanikisha na kuhakikisha kuwa watu wa kipato cha chini wanapata haki ya kupata huduma za kiafya na ajira bora.

 

Bi. Robinson amewahi kuwa Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa kati ya mwaka 1997 hadi 2002 mara tu baada ya kumaliza kipindi chake cha Urais wa Ireland, alishika uongozi wa nchi yake kati ya mwaka 1997-2002.

 

Katika kuboresha huduma hizo za afya nchini serikali itapanua na kuboresha hospitali za wilaya, mikoa na pia kujenga na kuongeza hospitali kuu hapa nchini, kuongeza mafunzo kwa wahudumu wa afya wakiwemo madaktari, manesi na watendaji wengine ikiwemo pia kuwaongezea ujuzi wahudumu waliopo sasa.

 

Serikali pia kwa kushirikiana na nchi marafiki, inaweka utaratibu ambapo wakunga wa jadi watapewa mafunzo na kupewa zana za afya kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma mahali walipo kwa njia iliyo bora na salama zaidi.

 

Rais Kikwete pia amemueleza Bi. Robinson kuhusu juhudi za serikali katika kupambana na magonjwa hatari kama malaria na ukimwi ambapo serikali inafanya jitihada kuhakikisha inautokomeza ugonjwa wa malaria moja kwa moja na kuhakikisha watu hawapati maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi.

 

Katika jitihada hizo pia serikali inafanya juhudi kubwa katika kuhakikisha malengo ya milenia ya kupunguza vifo vya mama na mtoto yanafanikiwa ambapo tayari hatua kubwa imepigwa katika kuongeza idadi ya watoto wanaopata chanjo.

 

Pamoja na hayo, kutokana na juhudi mbalimbali zilizokwisha fanywa kuhusu kupunguza vifo vya mama wajawazito, serikali imeanza kufanya sensa kuona mafanikio hayo yamefikia wapi ili kuongeza nguvu na mikakati zaidi na matokeo yake yanatarajiwa kutoka mwishoni mwa mwaka huu.

 

Leo katika Ikulu ya Dar-es-salaam, Rais pia ameongoza kikao cha Baraza la Mawaziri kinachotarajia kumalizika jioni.

 

Mwisho

 

Imetolewa na Premi Kibanga,

Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi

Ikulu-DSM

08 Oktoba, 209