UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116539

E-mail: press@ikulu.go.tz

Website:  www.mawasilianoikulu.go.tz  

Fax: 255-22-2113425

 

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

       P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, kesho, Jumanne, Januari 25, 2011, ataongoza mkutano wa kwanza wa Tume ya Kimataifa Kuhusu Afya ya Akinamama na Watoto utakaofanyika kwa siku moja mjini Geneva, Uswisi.

Rais Kikwete amewasili mjini Geneva leo, Jumanne, Januari 25, 2011, tayari kuendesha kikao hicho kwa ushirikiano na Waziri Mkuu wa Canada, Mheshimiwa Stephen Harper, ambao ni wenyeviti wenza wa Tume hiyo iliyoundwa na Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Shirika la Afya Duniani (WHO).

Kazi kubwa ya Tume hiyo yenye makamishna 30 na wazito kutoka maeneo mbali mbali ya ujuzi na uzoefu duniani, itakuwa ni kuangalia njia za jinsi ya kupunguza vifo vya akinamama na watoto na jinsi ya kuhakikisha kuwa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDG’s) katika maeneo ya afya ya akinamama na watoto yanaweza kufikiwa ifikapo mwaka 2015, mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa malengo hayo ya maendeleo ya milenia.

Tume hiyo pia itapendekeza njia bora zaidi ya kuziwezesha nchi mbali mbali duniani kupata, kutunza na kutoa taarifa sahihi kuhusu afya ya akinamama na watoto na jinsi nchi zinavyoweza kuwajibika zaidi katika matumizi ya fedha zinazotolewa kimataifa kukabiliana na matatizo ya afya yanayowakabili akinamama na watoto.

Mkutano wa leo utahudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Ban Ki Moon ambaye atashiriki katika ufunguzi, na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Dkt. Asha Rose Migiro ambaye vile vile ni kamishna wa tume hiyo.

Wengine ambao watahudhuria mkutano wa leo ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Mheshimiwa Margaret Chan na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Mawasiliano ya Simu (ITU) Mheshimiwa Hamadoun Toure ambao wote wawili ni makamu wenyeviti wenza wa mkutano huo.

Baada ya kuwa ametoa hotuba kwenye shughuli ya ufunguzi wa mkutano huo, Rais Kikwete atakuwa mwenyekiti wa kikao kitakachojadili uwajibikaji katika matumizi ya fedha za kimataifa za kupambana na changamoto za kiafya zinazowakabili akinamama na watoto na pia atakuwa mwenyekiti wa kikao cha majadiliano kuhusu masuala mtambuka katika suala zima la afya za makundi hayo mawili.

Rais Kikwete pia atazungumza kwenye kikao cha ufungaji wa mkutano huo na kwenye mkutano wa kimataifa wa waandishi wa habari utakaofuatia shughuli ya ufungaji wa kikao hicho.

 

Mwisho.

Imetolewa na:

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,

Safarini, GENEVA.

25 Januari, 2011