UNITED REPUBLIC OF
TANZANIA
DIRECTORATE OF
PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
|
Telephone: 255-22-2114512, 2116539 E-mail: press@ikulu.go.tz Website: www.mawasilianoikulu.go.tz Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S
OFFICE, THE STATE HOUSE, P.O. BOX
9120, DAR ES SALAAM. Tanzania. |
TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
·
Mradi kabambe wa umeme
kujengwa
·
Rais Kikwete apokea ripoti ya maandalizi
·
Utagharimu mabilioni ya fedha
·
Utaunganisha mikoa yote kwenye
Gridi ya Taifa
Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
leo, Jumatano, Oktoba 12, 2011, amepokea ripoti kutoka makampuni
mawili ya kimataifa kuhusu Mpango Kabambe ya mradi mkubwa
wa umeme ambao utaunganisha kwenye Gridi ya
Taifa mikoa yote sita ambayo
kwa sasa haiko kwenye gridi
hiyo.
Rais Kikwete amepokea ripoti hiyo kutoka
makampuni ya China National
Machinery&Equipment Import&Export
Corporation (CMEC) ya China na Siemens ya Ujerumani ambayo kwa pamoja yanatarajia
kujenga kituo kikubwa cha kuzalisha umeme kutokana na gesi katika
eneo la Mnazi Bay, mjini Mtwara na
pia kujenga njia ya kusafirisha
umeme ya kilomita 1,100 kutoka Mtwara hadi Singida.
Mradi huo mkubwa wa
umeme wa megawati 300 utakaogharimu karibu dola za
Marekani milioni 684 na utakaozalisha umeme wa moja
kwa moja na wenye nguvu
kubwa ya 300 kV (300 kV
High Voltage Direct Current – HVDC) utagharimiwa kwa pamoja na
mkopo kutoka Benki ya Exim ya
China na Serikali ya Tanzania.
Umeme kutokana na
mradi huo utaunganishwa kwenye gridi ya taifa
na kutoka Singida hatimaye utavutwa kupelekwa katika mikoa ya
Kaskazini Magharibi mwa Tanzania ya Kagera, Kigoma na Rukwa ambako
pia utaongeza upatikanaji wa umeme katika machimbo
ya madini yaliyoko katika mikoa hiyo.
Kwa mujibu wa
ripoti hiyo, mbali na mikoa
hiyo mitatu, pia mikoa ya
Lindi na Mtwara ambayo nayo
haiko katika Gridi ya Taifa
nayo itaunganishwa katika Gridi hiyo
kupitia umeme huo.
Kuunganishwa kwa mikoa hiyo
sita katika Gridi ya Taifa
kupitia umeme wa mradi huo
pamoja na Mkoa wa Ruvuma ambao utaunganishwa katika Gridi hiyo
kwa mradi unaogharimiwa na Serikali ya Sweden kutakamilisha mpango wa Serikali ya
Awamu ya Nne kuunganisha mikoa yote ya
Tanzania kwenye umeme wa Gridi ya
Taifa.
Kwa sasa Mkoa wa Kagera unahudumiwa na umeme kutoka Uganda, wakati Mikoa ya
Kigoma na Rukwa inahudumiwa na umeme wa
mafuta ya dizeli. Mikoa ya
Mtwara na
Lindi inapata umeme wake kutoka kampuni ya Wentworth ambao haujaunganishwa kwenye gridi ya
taifa.
Kuunganisha mikoa yote ya
Tanzania kwenye Gridi ya Taifa ilikuwa
moja ya ahadi
kubwa zilizotolewa na Serikali
ya Rais Kikwete
wakati anaingia maradakani na kwa
kuuunganisha mikoa hiyo sita kwenye
Gridi hiyo, Serikali hiyo itakuwa
imetimimiza ahadi hiyo.
Akipokea ripoti hiyo, Rais
Kikwete ameishukuru Wizara ya Fedha,
Wizara ya Nishati na Madini
pamoja na Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) kwa juhudi zao zilizofanikisha makubaliano ya kujengwa kwa mradi
huo mkubwa wa umeme ambao
utachangia kuongeza wingi wa umeme
nchini katika kipindi ambacho kwa miezi kadhaa
Tanzania imekabiliwa na mgawo wa umeme
kutokana na ukame uliokausha maji kwenye mabwawa
makubwa ya uzalishaji umeme nchini.
Rais Kikwete pia ameitaka
Wizara ya Fedha kwa kushirikiana
na Benki ya EXIM ya China kuhakikisha kuwa fedha za kutekeleza
mradi huo zinapatikana haraka iwezekanavyo na pia ameitaka TANESCO na makampuni ya
CMEC na Siemens baada ya kupatikana kwa
fedha kuanza ujenzi wa mradi
huo kwa kasi
na kuukamilisha katika muda na
ubora unaotarajiwa.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano
ya Rais,
Ikulu,
DAR
ES SALAAM.
12
Oktoba, 2011