DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

 

Telephone: 255-22-2114512, 2116898

E-mail:  ikulumawasiliano@yahoo.com

              press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425

 

PRESIDENT’S OFFICE,

      THE STATE HOUSE,

              P.O. BOX 9120,  

DAR ES SALAAM.

Tanzania.

 

 

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

Norway yampogeza Rais Kikwete

kwa kupambana na rushwa

 

Norway imeipongeza Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kwa hatua zake za kuboresha utawala bora na kupambana na rushwa.

 

Pongezi hizo zimetolewa leo (Jumatatu, Aprili 21, 2008) na Waziri Mkuu wa Norway, Mhe. Jens Stoltenberg wakati wa mazungumzo rasmi kati ya Tanzania na Norway, yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

 

Katika mazungumzo hayo ambayo yalikuwa ni sehemu ya ratiba ya ziara ya siku mbili ya Waziri Mkuu Stoltenberg katika Tanzania, kiongozi huyo wa Serikali ya Norway amesema kuwa pia nchi yake imefurahishwa na uamuzi wa Rais Kikwete kuteua Kamati ya Kuchunguza Sekta ya Madini nchini.  Norway ni moja ya nchi zinazowekeza katika sekta ya madini nchini.

 

Amesema kuwa Norway pia inafurahi kuona kuwa Tanzania imeanza kunufaika na matunda ya mageuzi ya kiuchumi ambayo yamekuwa yanaendelea kwa miaka 19 iliyopita.

 

Mhe Stoltenberg amesema pia kuwa nchi yake inatiwa moyo na mafanikio ambayo Tanzania inapata katika jitihada zake za kupambana na vifo vya watoto.

 

 

 

“Tunajua ni kazi ngumu na ya muda mrefu kuweza kuondokana na tatizo la vifo vya watoto, lakini mwanzo wenu umekuwa mzuri kwa namna ya kampeni ya chanjo na upatikanaji wa neti za kuzuia mbu,” amesema Waziri Mkuu huyo.

 

Naye Rais Kikwete ametumia mazungumzo hayo kumshukuru mgeni wake kuhusu hatua ambazo Norway imekuwa inazichukua kuisaidia Tanzania na mchango wa Norway katika nyanja ya kimataifa.

 

“Tunafurahi kwamba umepata muda wa kuja kututembelea, Tanzania na Norway zimekuwa marafiki kwa miaka mingi sana,” amesema Rais Kikwete mwanzoni mwa mazungumzo hayo kabla ya kumwelezea kwa undani hali ya kisiasa na kiuchumi nchini, pamoja na hali katika nchi jirani na Tanzania.

 

Mbali na kutoa shukurani za Tanzania kwa misaada ya Norway, Rais Kikwete pia amesifia mchango wa nchi hiyo katika nyanja ya kimataifa,

 

“Kwa miaka mingi, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Tanzania na Norway zimeungana mkono katika masuala mbalimbali ya kimataifa, amesema Rais Kikwete na kuongeza:

 

“ Kwa hakika, Norway imeonyesha uongozi katika masuala ya kimataifa kuanzia kwenye uanzishwaji wa dhana nzima ya “UN Moja”, kuja kwenye Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDG) hasa nne na tano, uanzishwaji wa Mtandao wa Viongozi Duniani wa Network of Global Leaders, mabadiliko ya hali ya hewa na mazingira duniani, hadi usuluhishaji wa migororo ya Darfur na Sri Lanka.”

 

Imetolewa na:

 

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais na Habari,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

 

21 Aprili, 2008