Sekta Binafsi

Ili kwenda sambamba na mabadiliko katika mfumo wa kiuchumi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania imechanganua upya  wajibu wake kwa raia ambao ni pamoja na kutengeneza sera, kulinda sheria za nchi, kutoa huduma muhimu za kijamii na miundo mbinu ya kiuchumi na kusaidia maendeleo ya kiuchumi.  Serikali inatambua kwamba ina wajibu wa kusaidia sekta binafsi na taasisi nyingine za kiuchumi katika juhudi zao za kuwekeza katika shughuli za kuzalisha mali na biashara kwa madhumuni ya kuharakisha ukuaji wa kiuchumi na maendeleo. Serikali inaweza kufanya haya kwa kuweka sawa sera zinazofaa, kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji nchini na nje ya nchi, kusimamia mabadiliko ya kitaasisi kwa minajili ya kusaidia maendeleo ya sekta binafsi, kuchechemua imani ya wawekezaji kwa kuweka wazi taratibu za kiutawala zilizo madhubuti katika Taasisi za serikali na kuweka viunzi vya kanuni na sheria. 

Kwa kutambua umuhimu huu wa kuandaa na kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya maendeleo ya sekta binafsi, serikali imekuwa ikifanya mabadiliko katika taasisi na sera zake.  Serikali imelegeza masharti ya kiuchumi, imefanya mabadiliko na kutunga sheria na sera mpya kadhaa zinazohusiana na masuala ya uwekezaji. Aidha imefanya mabadiliko katika mfumo wa fedha, imelegeza masharti ya biashara, na imeweka vivutio kwa wawekezaji. Aidha imefanya juhudi mbalimbali kuinua na kuendeleza sekta binafsi. Tanzania sasa imekuwa moja ya sehemu huru za kuwekeza barani Afrika. 

Katika kuunga mkono juhudi za sekta binafsi katika kusukuma maendeleo ya jamii kiuchumi, serikali imeandaa utaratibu wa kurasimisha uhusiano wake na sekta binafsi. Badala ya kukutana pale tu inapotokea  dharura sasa sekta binafsi inahusishwa katika kuandaa sera zinazohusu sekta binafsi na nyinginezo (k.m. Sekta binafsi imeshiriki katika Kamati ya Serikali ya Kuangalia Mfumo wa Kodi na vikundi mbalimbali vya kuangalia Matumizi ya Serikali.) Aidha Sekta binafsi pia imekuwa ikiwasiliana  na kutoa mchango wake mara kwa mara kwa serikali kupitia taasisi nyingine kama Chama cha Wafanyibiashara wa Viwanda na Kilimo Tanzania, Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania,  Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania na Baraza la Biashara la Taifa ambalo limezinduliwa  mwezi April, 2001. Baraza la Biashara la Taifa jukumu lake kubwa ni kutoa nafasi kwa sekta binafsi na za umma kushauriana juu ya mikakati ya kukuza na kuendeleza uchumi. 

Sekta binafsi imekuwa ikiyachukulia mabadiliko hayo kwa uangalifu mkubwa na kuyaunga mkono. Ukiritimba katika Sekta ya fedha umeondolewa na sasa kuna benki binafsi zaidi ya ishirini (20) na  Taasisi nyingine za fedha ambazo zinamiliki karibu asilimia themanini (80%)  ya rasilimali katika mfumo wa benki. Soko la bima limefunguliwa kwa makampuni binafsi ya hapa nchini na nchi za nje, na soko la kuuza na kununua hisa limefunguliwa jijini Dar es Salaam. Zaidi ya makampuni ya umma mia mbili na hamsini (250) kati ya mia nne (400) yamebinafsishwa. Sekta ya Kilimo na miundo mbinu ambayo hapo awali zilikuwa chini ya serikali zinazidi kubinafsishwa.  Viwanda mbalimbali vilivyokuwa chini ya umiliki wa serikali vimebinafsishwa. Eneo ambalo limepata wawekezaji wengi zaidi kutoka ndani na nje ya nchi ni utafutaji na uchimbaji madini pamoja na utalii.

Title

.

Title

.

Title

.