HOTUBA YA WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UBINAFSISHAJI,
MHESHIMIWA DK. ABDALLAH O. KIGODA (MB.) AKIWASILISHA BUNGENI, MAKADIRIO YA MATUMIZI YA OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UBINAFSISHAJI KWA MWAKA 2001/02
Kujenga Uwezo wa Kuendeleza Utafiti na Uchambuzi wa Masuala ya Kitaifa ya Kiuchumi na Kijamii
4. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua uzito wa majukumu yetu, Ofisi ya Rais Mipango na Ubinafsishaji kwa kushirikiana na Idara Kuu ya Utumishi imetekeleza zoezi la kuchambua dira, madhumuni, majukumu na uwezo wa taasisi yetu ili kutambua maeneo yanayohitaji kuboreshwa. Utekelezaji wa mkakati huu utaiwezesha Ofisi kutoa huduma bora za usimamizi wa uchumi, upangaji wa mipango inayotekelezeka na kutoa taarifa kwa wakati.
5. Mheshimiwa Spika, ili Ofisi hii iweze kutekeleza majukumu yake, ujenzi wa uwezo ni muhimu kwa kuboresha mazingira ya utendaji kazi, upatikanaji wa nyenzo za kufanyia kazi na upatikanaji wa wataalamu wa kutosha. Hatua mbali mbali zimeanza kuchukuliwa kwa mfano kuboresha. vitendea kazi kama vile kompyuta, kuendeleza mafunzo, kuajiri wachumi na maafisa mipango wapya 57, kujenga mtandao wa taifa (National Website) ambao unajumuisha mitandao yote ya Serikali n.k. Madhumuni ya mtandao huu ni kutoa fursa kwa yeyote anaetaka kupata taarifa zozote za kiuchumi, kijamii, biashara n.k. kwa wakati. Anuani ya Website yetu ni www.tanzania.go.tz.
6. Aidha, kazi ya Ofisi yangu ni kuratibu majukumu yanayotekelezwa na sekta zingine na ndiyo maana Ofisi inashiriki katika ujenzi wa taaluma ya mipango katika sekta zingine. Kwa mfano baadhi ya wataalam wapya watakaoajiriwa wengine watapangiwa kazi katika wizara na mikoa, tunaimarisha Chuo cha Mipango vijijini Dodoma na Chuo cha Takwimu ili viweze kutosheleza mahitaji ya mafunzo ya maofisa mipango wilayani na tutachangia gharama za kuendesha mafunzo hayo ili Serikali za mitaa ziweze kumudu gharama za kuendesha mafunzo hayo.
Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025
7. Mheshimiwa Spika, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ilipitishwa rasmi na Serikali mwaka 1999. Utekelezaji wa Dira unahitaji kuwekewa mikakati makini katika ngazi zote, kama vile; kuhusisha sera, kurekebisha sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza uchumi. Mikakati hii pia inalenga katika kukuza mauzo nje, kupunguza umaskini n.k.. Kasi ya utekelezaji wa Dira inategemea kutengemaa kwa vigezo muhimu vya uchumi kama vile kasi ya upandaji bei, kukua kwa Pato la Taifa, na kuongeza mapato ya Serikali. Mafanikio yameanza kuonekana, kinachohitajika sasa ni kuchambua fursa katika ngazi zote na kubaini vikwazo ili kutayarisha Mpango wa Muda wa Kati wa Kutekeleza dira hii. Mpango huu wa kitaifa, utajumuisha programu na miradi mikubwa iliyopo na inayoendelea na mingine itakayobuniwa kutoka ngazi za Wilaya, Mikoa na Sekta, kwa kutumia utaratibu mpya wa mpango shirikishi unaojumuisha wananchi na washikadau wengine muhimu katika kupanga, kutekeleza, kusimamia na kutathmini mipango hiyo ya maendeleo.
Uchambuzi wa Sera, Mikakati na Mwenendo wa Vigezo mbali mbali:
8. Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka 2000/01, Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji ikishirikiana na Wizara mbali mbali iliendelea na juhudi za uchambuzi wa sera, mikakati na mwenendo wa vigezo mbali mbali vya kupima maendeleo ya uchumi na kubainisha maeneo yanayohitajika kufanyiwa kazi zaidi. Aidha, Ofisi imeshiriki katika zoezi la uchambuzi na kuandaa Mpango wa Kati wa Mapato na Matumizi ya Serikali, kuandaa Mkakati wa Kuendeleza Kilimo, Mkakati wa Maendeleo Vijijini, Urekebishaji wa Mfumo wa Ugani Nchini, uchambuzi wa sera za Ukimwi, jinsia na kushiriki kikamilifu katika kufanya marekebisho ya sera za kisekta kama Uendelezaji wa Maliasili nchini, Sera za Fedha, Mawasiliano, Sera ya Biashara, Sera ya Idadi ya Watu, pamoja na kuandaa vigezo mbali mbali vya kupima umaskini na maendeleo ya kiuchumi kama vile “Human Development Index”. Katika mwaka 2001/02 Ofisi ya Rais Mipango na Ubinafsishaji itaendelea kufuatilia sera zilizohuishwa na mikakati iliyoandaliwa na kuweka vigezo vya kupima maendeleo katika sekta hizo.
Uimarishaji wa Kitengo cha Kufuatilia Mashirika ya Umma Yanayobinafsishwa na Maendeleo ya Sekta Binafsi
9. Mheshimiwa Spika, kitengo cha Ufuatiliaji utendaji wa mashirika yaliyokwisha kubinafsishwa katika Ofisi hii kimeendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na vitengo vya ufuatiliaji vya Wizara zenye mashirika yaliyobinafsishwa kama Kilimo na Chakula, Maliasili na Utalii, Viwanda na Biashara, Mawasiliano na Uchukuzi. Ofisi imetenga fedha za kuimarisha kitengo ikiwa ni pamoja na ununuzi wa gari la kutembelea mashirika/viwanda husika na ununuzi wa kompyuta Aidha kitengo kitaimarisha nguvukazi kwa kuongeza wataalam wa ufuatiliaji. Taarifa za utekelezaji za robo mwaka zitatolewa . Programu hii itaiwezesha Serikali kuchukua hatua madhubuti kwa wale wawekezaji wasiokuwa waaminifu katika kuheshimu mikataba waliosaini na kukiuka programu zao za utekelezaji. Pamoja na hatua hizo, katika jitihada za kukusanya madeni ya mauzo kutoka kwa wawekezaji/wanunuzi sugu, wakusanyaji madeni walikwishateuliwa na Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika na wamekwishaanza kazi.
10. Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua nafasi ya sekta binafsi katika kukuza uchumi imeanzisha Baraza La Taifa la Biashara “Tanzania National Business Council” (TNBC) ambalo litajenga mfumo wa mawasiliano na mashauriano katika masuala ya kisera na mikakati ya kukuza Uchumi baina ya Serikali na Sekta Binafsi. Shughuli za Chombo hiki zitaratibiwa na Ofisi ya Rais Mipango na Ubinafsishaji.
Mpango wa Uhai, Ulinzi na Maendeleo ya Mtoto (CSPD)
11. Mheshimiwa Spika, mpango huu kati ya Serikali na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) una madhumuni ya kuboresha na kupanua huduma mbali mbali za afya pamoja na chanjo, lishe, maji, usafi wa mazingira na elimu ili kuboresha hali ya mama na mtoto; kabla hajazaliwa na baada ya kuzaliwa hadi kufikia miaka kumi na minane.
12. Mheshimiwa Spika hivi sasa ofisi yangu inaandaa mpango mwingine wa miaka mitano wa ushirikiano na UNICEF katika kipindi cha 2002 hadi 2006. Lengo la mpango huu ni kuimarisha huduma za mama na mtoto katika wilaya 55 za Tanzania Bara na wilaya zote za Zanzibar. Aidha mpango huu utahusika katika kujenga uwezo wa kukabili majanga, kupambana na janga la ukimwi, kuhuisha sera mbali mbali zinazohusu maendeleo ya mtoto na kujenga uwezo wa jamii wa kupanga na kutekeleza maendeleo yao.
Utekelezaji wa Sera ya Idadi ya Watu.
13. Mheshimiwa Spika, Ofisi yangu imeshirikiana na UNFPA katika maandalizi ya sensa ya watu ya 2002 na kuwa taasisi ya kwanza kutoa mchango wa fedha na utaalamu na kuhamasisha wahisani wengine kushiriki. Mwaka huu wa 2001 ndio uliokuwa mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa mpango wa nne wa ushirikiano kati yetu na UNFPA. Ofisi yangu kwa kushirikiana na taasisi husika tumekwisha andaa mpango wa tano wa ushirikiano kwa kipindi kingine cha miaka mitano 2002 hadi 2006. Mpango huu unalenga katika kuimarisha masuala ya Jinsia, Uhamasishaji, Afya ya Uzazi na Maendeleo ya Watu. Aidha, UNFPA itaelekeza juhudi za ziada katika kuboresha huduma za uzazi katika wilaya 26 za Tanzania Bara na Visiwani.
14. Mheshimiwa Spika, Tanzania pamoja na nchi za Uganda, Botswana na Ghana zimepatiwa msaada wa $.16.5 milioni kila moja kutoka Mfuko wa Bill na Melinda Gates wa Marekani ili zitumike katika kuboresha huduma za uzazi kwa vijana hasa kupambana na janga la ukimwi. Katika awamu ya kwanza Wilaya zilizochaguliwa ni wilaya zote za Dar es Salaam, Kasulu, Kibondo, Musoma Mjini na Arusha Mjini. Kwa upande wa Zanzibar ni mikoa ya Mjini Magharibi na Kusini Pemba. Mradi utatekelezwa na taasisi za Serikali na nyinginezo zilizomo katika wilaya husika. Vikundi vya vijana vitapewa kipaumbele wakati wa kuteuwa watekelezaji wilayani ili kuwashirikisha vijana katika kuamua na kutekeleza mambo yanayowahusu.
Ushirikiano wa Kiuchumi Kimataifa:
15. Mheshimiwa Spika, juhudi za kimataifa za kuleta mfumo mpya wa kiuchumi na maendeleo ya nchi zinazoendelea bado unahitaji msukumo zaidi hasa kuhusu suala la misaada ya maendeleo ili kutanzua matatizo ya nchi maskini sana duniani. Tunayokazi kubwa ya kushawishi viwango vya ODA kuongezeka. (Angalia Kielelezo) Tunayo kazi kuendeleza kutetea kupunguziwa deni letu la Taifa pamoja na HIPIC. Tunayo kazi ya kuendelea kuzungumzia taratibu za kuweza kufikia masoko ya nje na kupata bei nzuri za bidhaa zetu za kilimo duniani. Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia maendeleo (UNDP) limekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza programu za kupunguza umaskini, kuboresha mazingira, kuimarisha utawala bora nchini na kuboresha uwezo wa kupanga mipango yetu kwa ufanisi zaidi. Tanzania iliwasilisha programu ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo ya nchi zilizo maskini sana duniani katika mkutano uliofanyika Brussels-Ubelgiji mwezi Mei mwaka 2001 chini ya mpango wa Umoja wa Mataifa wa kusaidia nchi zilizo nyuma sana kimaendeleo.
16. Mheshimiwa Spika, Tanzania inashiriki katika kuendeleza na kuboresha ushirikiano wa kiuchumi na nchi za SADC na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. (Angalia Kielelezo) Katika eneo la TCDC, Tanzania ina mpango wa kutekeleza mradi wa kubadilishana wataalam, ushauri na mafunzo na nchi za China, Indonesia, Thailand na India. Tunaratibu pia mpango unaotokana na Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Tokyo kwa ajili ya Maendeleo ya Afrika TICAD II ambao Serikali ya Japan imeziahidi nchi za Afrika msaada wa Yen billioni 90 ili kukabiliana na umaskini, kuimarisha utawala bora, kupunguza mzigo wa madeni na pia kusaidia kusuluhisha migogoro baina ya nchi na nchi.
Mkakati wa Kukuza Mauzo ya Nje
17. Mheshimiwa Spika, baada ya Serikali kuidhinisha Mkakati wetu wa Kukuza Mauzo Nje, (EDS) yamebainishwa maeneo manne kama vikwazo: sera na sheria, taasisi zinazosimamia mauzo nje, miundo mbinu na uwezo wa wafanyabiashara. Sera na sheria zinazokwamisha biashara ya nje zimeainishwa na ziko katika hatua mbali mbali za marekebisho. Bodi ya Biashara ya Nje nayo inafanyiwa marekebisho ya ki-muundo. Hivi karibuni Serikali imeunda chombo cha mashauriano (Tanzania National Business Council) kwa lengo la kuongeza uwezo wa wafanyabiashara kushiriki katika masoko ya kimataifa. Tayari Serikali, kwa kutumia Shirika lake la Maendeleo ya Taifa imeanzisha kitengo cha kuanzisha maeneo huru ya uwekezaji (EPZ) yatakayozalisha bidhaa zakusafirishwa nje. Aidha, tayari taratibu za kutoa vivutio kwa sekta ya Nguo kwa kufuta kodi mbali mbali, ili kuongeza uzalishaji zimeshaanza kufanyiwa kazi.
18. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2001/02 mbali ya kuendelea kuratibu utekelezaji wa Mkakati wa Mauzo Nje, Ofisi yangu inakusudia kufanya uchambuzi wa kina wa matatizo ya jumla yanayokabili biashara yetu nje na kuanzisha Benki ya Takwimu zinazohusu biashara. Hatua zitachukuliwa ili kubaini ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini ili kuhimili ushindani wa bidhaa kama hizo zinazozalishwa nchi za jirani.
Utekelezaji wa Sera ya Uwekezaji Rasilimali
19. Mheshimiwa Spika, zoezi la kujenga uwezo wa kitaalam ndani ya TIC linalenga kukiwezesha Kituo hicho kutoa huduma bora kwa wawekezaji na kupata ufanisi unaokubalika. Ili kutekeleza azma hiyo katika kipindi cha miezi 9 kituo kimebuni na kutekeleza mpango wa kuwatembelea wawekezaji ili kuratibu matatizo waliyonayo kwa lengo la kupata ufumbuzi wa matatizo hayo. Utaratibu huo wa “after care service” umeanza vizuri na tayari miradi zaidi ya 400 imekwisha tembelewa na TIC. Sambamba na hili utaratibu wa kukifanya Kituo kiwe “One stop Centre” unaendelea vizuri. Kituo kimekuwa kikiwahudumia moja kwa moja wawekezaji katika masuala ya uhamiaji, vibali vya kazi, kuanzisha biashara, ardhi na masuala ya kodi bila wawekezaji kutembea wao wenyewe ofisi hadi ofisi kupata huduma hizi.
20. Mheshimiwa Spika, uhamasishaji wa uwekezaji toka nje wa kuvutia FDI kubwa zaidi utaimarishwa. Uhamasishaji huu utafuata “targeted approach” kwa kupanga nini kifanywe kwenye kila bara na tulenge nchi gani katika hilo bara. Pia kila tutakapohamasisha uwekezaji tutakwenda na mkakati wa kuwavutia wawekezaji hao katika maeneo maalum kutokana na uzoefu tulioujenga kuhusu nchi hizo na maeneo wanayopenda kuwekeza. Kwa hali hiyo Kituo kitafanya kazi kwa karibu na viongozi wa mikoa ili kila mkoa ujenge uwezo wa kutangaza utajiri walio nao utakaovutia wawekezaji. Kwa hiyo napenda kuchukua fursa hii kuwaomba viongozi wa mikoa watayarishe “land use plans”, “Project Profiles” n.k. ili TIC iweze kuzitumia kikamilifu kuinadi nchi yetu. Sambamba na jitihada hizi TIC itafanya kazi kwa karibu na SMEs ili ziweze kunadi miradi yao na kupata wabia na teknolojia.
21. Mheshimiwa Spika, ili jitihada za Kituo ziweze kufanikiwa, Watendaji serikalini wanawajibika kuondoa vikwazo ambavyo vinakwamisha uwekezaji nchini. Baadhi ya vikwazo hivi ni pamoja na urasimu. Ili kukabiliana na matatizo haya hatua zifuatazo zimechukuliwa:
(a) Mheshimiwa Rais tayari ameunda kamati maalum ya uwekezaji (National Investment Steering Committee) chini ya uenyekiti wa Mheshimiwa Waziri Mkuu na kuwapa uwezo wa maamuzi ya moja kwa moja ya kuwahudumia wawekezaji .
(b) Serikali kwa kushirikiana na wafadhili toka Uingereza, Uswisi na Sweden, imefanya utafiti kuainisha nini kifanyike ili kuondoa kero katika sekta ya uwekezaji. Taarifa ya utafiti huu inaitwa “Business Environment Strengthening for Tanzania” (BEST). Utafiti huu unapendekeza mkakati utakaofuatwa katika kuhuisha sheria zote zinazodhibiti uwekezaji ili kubainisha sheria zipi zifutwe, zipi ziunganishwe, na sheria zipi mpya zitungwe ili kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji nchini. Mapendekezo ya marekebisho yote ya sheria yataletwa katika Bunge hili.
Utekelezaji wa Sera ya Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma
22. Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu ya Hali ya Uchumi nililiarifu Bunge lako kwamba hadi sasa ni mashirka 333 ambayo yamebinafsishwa. Pamoja na kwamba zoezi hili linaendeshwa kwa uwazi na taarifa kutolewa mara kwa mara, kumekuwa na manung’uniko kuhusu ni nani hasa anayenufaika zaidi kati ya Watanzania na wageni. Napenda kulifahamisha Bunge, kwamba katika jumla ya Mashirika 333 yaliyobinafsishwa, Mashirika 120 yamenunuliwa na wawekezaji wa Tanzania, mashirika 25 yamenunuliwa na wawekezaji wageni na mashirika 188 yameingia ubia kati ya Serikali, Watanzania na wawekezaji kutoka nje ya nchi. Kutokana na takwimu hizi, ni dhahiri kwamba Watanzania wameshirikishwa katika zoezi hili kwa kiwango cha kuridhisha.
23. Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza utekelezaji wa sera hii ya kurekebisha Mashirika ya Umma, mkazo mkubwa sasa utaelekezwa katika ubinafsishaji wa mashirika ya huduma na miundombinu. Mashirika hayo ni Shirika la Reli la Tanzania, Mamlaka ya Maji safi na Maji taka ya Dar es Salaam, Shirika la Umeme Tanzania, Shirika la Ndege la Tanzania, Shirika la Taifa la Bima, Benki ya Taifa ya Kuhudumia wawekezaji wadogo wadogo, Vitengo vya Kibiashara vya Mamlaka ya Bandari, Mashamba ya Mifugo, Mashamba makubwa ya nafaka, chai na kahawa. Shirika la Reli, vitengo vya Mamlaka ya Bandari na Mamlaka ya Maji Safi na Maji taka Dar es Salaam, hayatauzwa bali yatakodishwa kiuendeshaji na utoaji huduma wakati miliki ya miundo mbinu itabaki Serikalini.
24. Mheshimiwa Spika, hadi sasa mashirika mawili, Kampuni ya Simu na Kitengo cha Makontena cha Mamlaka ya Bandari yamebinafsishwa kwa njia ya uuzaji wa hisa na kukodisha. Kuhusu ubinafsishaji wa mashamba makubwa serikali inaandaa mkakati wa kuwawezesha Watanzania kuyamiliki na kuyaendesha kibiashara ili yaweze kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.
25. Mheshimiwa Spika, kwa jumla mashirika mengi yaliyobinafsishwa yanafanya kazi vizuri na yanaonyesha maendeleo ya kudhirisha. Mengine yapo katika hatua mbali mbali za kufufuliwa hasa ikizingatiwa kwamba, mashirika mengi ya umma yalikuwa katika hali mbaya sana wakati yanabinafsishwa. Kwa maana hiyo, wawekezaji wapya wanalazimika kuchukua hatua za dhati za kuyarekebisha kabla ya kuanza uzalishaji. Kazi hii huchukua muda mrefu.
26. Mheshimiwa Spika, Katika utekelezaji wa Sera ya Ubinafsishaji baadhi ya faida zilizopatikana ni kama
ifuatavyo:-
27. Mheshimiwa Spika, licha ya mafanikio yaliyopatikana, utekelezaji wa sera ya ubinafsishaji unapambana na matatizo mbali
mbali.
28. Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na matatizo haya Ofisi yangu
itaendelea kuchukua hatua zifuatazo:-
Kuimarisha Ukusanyaji, Uchambuzi na Usambazaji wa Takwimu.
29. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2000/01, Ofisi ya Taifa ya Takwimu iliendelea kukusanya takwimu na kuimarisha ubora wa takwimu za kilimo, kiliendeleza utafiti wa wawekezaji kutoka nchi za nje kilifanya maandalizi za tafiti za Waajiri na Wageni ili kupata takwimu sahihi zinazohusu utalii. Ofisi ya Taifa ya Takwimu imeimarika kama Kituo cha rejea katika taaluma ya Takwimu na viwango vya ukusanyaji wa takwimu; imekwishajenga Benki ya Kumbukumbu za Kiuchumi na Kijamii, imefanya utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi wa mwaka 2000/2001, imefanya utafiti wa Watu wenye uwezo wa kufanya kazi na shughuli za watoto kwa mwaka 2000/2001. Vigezo vitakavyopatikana kutokana na tafiti hizo vitasaidia katika kufuatilia mpango mzima wa kupunguza umaskini.
30. Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mwaka 2001/02 taasisi hii itaendelea na
31. Mheshimiwa Spika, katika kuboresha takwimu za Pato la Taifa mwaka 1991 ulifanyika utafiti wa sekta isiyo rasmi nchi nzima. Utafiti kama huo ulifanywa tena mwaka 1995 Dar es Salaam. Tafiti zote mbili zilitumika katika kuboresha takwimu za pato la taifa wakati wa utekelezaji wa mradi wa Uimarishaji wa pato la taifa. Hata hivyo kwa kuwa ni muda mrefu tangu tafiti hizo zifanyike na shughuli zisizo rasmi zimezidi kupanuka miaka ya karibuni kuna haja ya kufanya utafiti mwingine. Tumeshaanza kutafuta wafadhili watakaogharamia utekelezaji wa utafiti huo. Utafiti huo, unatarajia kuboresha takwimu ikiwa ni pamoja na mchango wa wakina mama katika sekta isiyo rasmi. Utafiti huu utasaidia sana kuonyesha viwango halisi hususan vya kukua kwa Pato letu la Taifa.
Maandalizi ya Sensa ya Watu ya mwaka 2002
32. Mheshimiwa Spika, Sensa ya Watu sasa itafanyika Agosti mwaka 2002, ili kupata takwimu muhimu za kuandaa mipango ya maendeleo na kupima hali ya maisha ya watu katika ngazi ya taifa, mkoa, wilaya na ngazi za chini. Kazi muhimu ya zoezi la kutenga maeneo litakamilika mapema mwezi wa Machi 2002. Kazi zingine zitakazofanyika ni mafunzo kwa wadadisi, ununuzi wa vifaa, kufanya sensa ya majaribio na kuchapisha madodoso.
33. Mheshimiwa Spika, zoezi la sensa hugharimu fedha nyingi. na wahisani mbali mbali wameonyesha nia ya kugharamia mradi
huu.
Aidha, wafadhili wengine ambao wameonyesha nia ya kuchangia mradi huu ni Japan na Ubelgiji. Kasi ya kutafuta michango zaidi inaendelea.
Uendelezaji wa Taaluma ya Takwimu
34. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji ina jukumu la kusimamia Chuo cha Takwimu Cha Mashariki na Kusini mwa Afrika. Katika zoezi la Kurekebisha mfumo wa uendeshaji wa Serikali (Civil Service Reform Programme), imeamuliwa kwamba Chuo hicho kiendeshwe kama Wakala wa Serikali (Executive Agency). Matayarisho ya kukifanya Chuo kiwe Wakala wa Serikali karibu yamekamilika.
35. Kwa mwaka wa fedha 2001/02 Chuo kinatarajia kuendesha mafunzo ya kawaida ya Cheti na Stashahada; kufanya utafiti na kutoa ushauri utakaosaidia katika utayarishaji wa mipango katika ngazi zote; na kuendelea kuendesha mafunzo ya muda mfupi kulingana na mahitaji ya wateja.
Uendelezaji wa Sera ya Tija, Mapato na Bei
36. Mheshimiwa Spika, pamoja na ufinyu wa bajeti Baraza la Taifa la Tija limejitahidi kutekeleza yale machache yaliyopo ndani ya uwezo wake ikiwa ni pamoja na kuelimisha na kuhamasisha umma kuhusu tija kwa njia ya kipindi cha Redio cha ‘Tija na Maendeleo’ Katika mwaka wa fedha wa 2001/02 kazi kubwa ya Baraza itakuwa ni kuhuisha na kurekebisha Sera ya Taifa ya Tija, Mapato na Bei ya mwaka 1980 ili iweze kuendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025. Pamoja na kurekebisha Sera, uhuishaji huo pia utarekebisha muundo wa Baraza.
Uendelezaji Taaluma ya Mipango ya Maendeleo Vijijini
37. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2000/01, Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kimeendelea kuendesha taaluma ya Mipango ya maendeleo vijijini, katika viwango vya kozi za cheti katika Mipango na Maendeleo Vijijini, Stashahada ya Juu na Stashahada ya Uzamili katika fani za Mipango ya Mikoa na Mipango ya Mazingira. Aidha, mafunzo ya muda mfupi katika ngazi mbali mbali yaliendeshwa, kwa watendaji na viongozi wa vijiji, vitongoji na mitaa nchini. Chuo kilitoa ushauri katika maeneo mbali mbali nchini kuhusu upangaji na utekelezaji wa programu za mipango ya maendeleo vijijini.
38. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2001/02, Chuo kitaendelea kujiwekea miundo mbinu ya ujenzi wa jengo la bweni, kitaweka mtandao wa mawasiliano ya kisasa ikiwa ni pamoja na ununuzi wa kompyuta; kitaimarisha kitengo chake cha takwimu na habari ili kiweze kukusanya, kuchambua, kuweka na kusambaza takwimu na taarifa muhimu zinazotumika katika upangaji mipango ya maendeleo vijijini kwa watumiaji mbali mbali, na kitaanzisha mitaala ya kozi mpya za upangaji mipango kwa kutumia kompyuta, idadi ya watu, jinsia na maendeleo.
MWISHO
39. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa napenda kuainisha masuala ambayo Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji na Taasisi zilizo chini yake itayapa kipaumbele katika mwaka wa Fedha wa 2001/02 kama ifuatavyo:
Makadirio Kwa Mwaka wa 2001/02
40. Mheshimiwa Spika, sasa naomba Bunge lako liidhinishe jumla ya Sh. 14, 441,222, 500 zinazoombwa kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na ya Maendeleo ya Ofisi ya Rais, Mipango na Ubinafsishaji na Taasisi mbali mbali zilizo chini yake. Kati ya fedha hizo Sh. 13,958,122,500 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Sh. 483,100,000 ni kwa ajili ya matumizi ya miradi ya maendeleo.
41. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja