TAMKO LA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA BENJAMIN WILLIAM MKAPA AKIZINDUA ‘‘WEBSITE’’ YA TAIFA, UWANJA WA TAIFA, DAR ES SALAAM, 09 DESEMBA 2001

Ndugu Wananchi,

Kwa kutumia wataalam wazalendo, Serikali imeanzisha “Website” ya Taifa yenye lengo la kudumisha na kuielezea taswira sahihi ya Tanzania kwa wananchi wake na ulimwengu mzima. Itatoa pia taarifa sahihi kuhusu nchi yetu, kwa manufaa ya wanaotaka kujua ukweli wa mambo. “Website” hii itatuwezesha na sisi kushiriki kikamilifu katika utandawazi na hivyo kutangaza na kukuza utalii pamoja na kuvutia wawekezaji.  Aidha, kupitia “Website” hiyo Serikali itaongeza uwazi katika shughuli zake na kurahisisha upatikanaji wa habari za Tanzania katika mtandao wa kompyuta unaotumika ulimwenguni, yaani “Internet”. Haya yote ni katika kudumisha malengo ya uwazi na ukweli kama ambavyo nimekuwa nikizungumza katika hotuba zangu nyingi.

“Website” hii ya Taifa ina taarifa mbali mbali za Wizara za Serikali ya Jamhuri ya Muungano, taarifa za kisekta, taarifa za kipekee kuhusu Zanzibar, na taarifa nyinginezo nyingi kuhusu Tanzania.  Hotuba zangu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na hii ya kuadhimisha miaka arobaini ya uhuru ambayo inasikika sasa hivi inaweza kupatikana katika “Internet” kupitia Website ya Taifa.  Aidha, maadhimisho haya yanashuhudiwa moja kwa moja na watu mbalimbali ndani na nje ya Tanzania kupitia “Internet”.

Ndugu Wananchi,

“Website” hii ya Taifa, ambayo anuani yake ni: www.tanzania.go.tz, imekuwepo hewani kwa karibu mwaka mmoja hivi sasa kwa majaribio. Majaribio hayo yamekuwa na mafanikio, na leo hii tunapoadhimisha miaka 40 ya Uhuru wetu, ninaona fahari, na ninayo furaha kubwa, kutangaza kuwa ninaizindua rasmi ‘‘Website’’ ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na ninatumia fursa hii kuwataka viongozi wote na wananchi wanaoweza waende na wakati na kutumia teknolojia za mawasiliano kama hizi za kisasa kwa ajili ya elimu, burudani na biashara, lakini kwa mujibu wa sheria.  

AHSANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA