MAJIBU NA MAELEZO KUHUSU “GAME CARNAGE IN TANZANIA ALARMS KENYA”

 

1.0     UTANGULIZI:

 

          Kwenye gazeti la East African la tarehe 4 – 10 Februari, 2002, iliandikwa makala yenye kichwa cha habari “Game Carnage in Tanzania Alarms Kenya” iliyoandikwa na John Mbaria na taarifa za nyongeza kutoka kwa Mwandishi Apolinari Tairo wa Dar es Salaam.  Makala hayo yanahusu Kampuni ya Uwindaji ya Ortello Business Corporation iliyoanza kuwinda katika Pori la “Loliondo Game Controlled Area” toka mwaka 1992.

 

          Hoja zilizotolewa katika makala hayo ni zifuatazo:

 

(a)              Kutokana na uwindaji unaofanywa Loliondo G.C.A., Kenya inapoteza asilimia 80 ya wanyamapori wake wote walio karibu na mpaka wa Tanzania na Kenya.

(b)             Wanyamapori hao  wanawindwa kwenye njia ya mapito (migratory routes) ya wanyama yaliyo kati ya kusini mwa Kenya na Serengeti National Park.  Wanyama hao wanawindwa wakiwa njiani wakati wanapohamia Kenya na wakati wanaporudi Tanzania mwezi Julai hadi Desemba.

(c)              Kwamba uwindaji wa kitalii unatishia kuharibu biashara ya utalii Kenya ambao umekadiriwa kuwa na thamani ya US$ 256 millioni kwa mwaka.

(d)             Imedaiwa kwamba uwindaji huo unaua wanyama kiholela na kwamba hakuna utaratibu wala mpangilio wa ufuatiliaji ili kuelewa idadi halisi ya wanyama wanaouawa au kusafirishwa nje.

(e)              Kwamba ndege za Kampuni ya OBC wakati zinaporuka toka Loliondo kwenda UAE zinasafirisha nje wanyama na ndege hai wa kila aina, na kwamba zinaruka moja kwa moja kuingia na kutoka Loliondo bila kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (KIA).

 

 

 

 

 

 

 

 

Yafuatayo ni maelezo na majibu ya hoja zilizotolewa na gazeti la East African:-

 

2.0.    Uhifadhi wa Wanyamapori Tanzania

 

Tanzania ni moja ya nchi nne duniani zinazoongoza kwa kuwa na bioanuwai nyingi na za aina mbalimbali. Tanzania pia inaongoza katika shughuli ya uhifadhi wanyamapori katika Afrika.  Tanzania ina Hifadhi za Taifa kumi na mbili (12) ikijumuisha Hifadhi ya Serengeti ambayo ni maarufu sana duniani;  Mapori ya Akiba (Game Reserves) 34 na Mapori Tengefu (Game Controlled Areas) 38.  Maeneo ya hifadhi ya wanyamapori yamechukua kiasi cha asilimia 28 ya eneo kavu la Tanzania.  Kutokana na kazi nzuri ya uhifadhi na matumizi endelevu, Tanzania ilitunukiwa zawadi ya kimataifa ya kuhifadhi wanyamapori na Shirika la Kimataifa la Uwindaji (Safari Club International) mwaka 1995. Makao Makuu ya Shirika hilo yako Marekani.

 

Tanzania bado ina umaarufu mkubwa duniani kwa kuwa na aina  nyingi za wanyamapori ambao wako katika hatari ya kutoweka duniani katika mazingira yao ya asili.  Wanyama hao ni kama vile faru, sokwe mtu, tembo na mamba (slender snouted crocodile).

 

Mwaka 1998, Serikali ya Tanzania iliunda Sera ya Wanyamapori ambayo ilitoa mwongozo na  kusisitiza uhifadhi wa wanyamapori na matumizi endelevu ya rasilimali ya wanyamapori kwa ajili ya faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

 

3.0                Uwindaji wa Kitalii

 

Uwindaji wa Kitalii au wa aina yeyote ile ambao unafanyika kulingana na taratibu na sheria za uhifadhi na kwa mpangilio hauathiri idadi ya wanyamapori popote pale duniani.  Hii ni kwa sababu desturi ya uwindaji ni kuchagua wakati wa kuua na siyo kupiga kiholela.  Katika miaka ya 1973 – 1978, Tanzania ilifunga uwindaji.  Matokeo yake ujangili uliongezeka.  Kitendo cha kutokuwepo kwa uwindaji wa kitalii ilisababisha kushuka kwa mapato ya serikali.  Upungufu huu wa mapato ulisababisha serikali kuwa na bajeti finyu kwa shughuli za uhifadhi na hivyo kutopatikana kwa vitendea kazi inavyostahili.  Watumishi, hususan askari wanyamapori, walikosa huduma muhimu.  Hali hii ilipelekea majangili kuvamia mapori na kuua wanyama hovyo kwa manufaa yao. 

 

Tanzania inayo mipango mizuri inayopelekea ongezeko la wanyama na mapato mwaka hadi mwaka.  Mfano Tanzania ilikuwa moja ya nchi zilizopendekeza kufungwa kwa biashara ya meno ya tembo  duniani mwaka 1989 chini ya mkataba wa CITES.  Pia Tanzania iliendesha zoezi kubwa la kuzia ujangili duniani kote, “Operation Uhai” kwa kipindi cha meizi 18 kuanzia mwaka 1989.  Katika kipindi cha 1989 – 1994 tembo waliongezeka kutoka 55,000 (1989) hadi zaidi ya 80,000 (2001). Tembo ni “keystone species” na kwa sababu ya umaarufu wa “products” zake katika biashara pia ni “indicator” nzuri ya hali na idadi ya aina nyingine za wanyama katika mazingira yao.

Aidha kutokana na uwindaji wa kitalii mapato ya Serikali kati ya mwaka 1989-1993 yaliongezeka toka USD 2,422,500.00 hadi USD7,377,430.00  Mwaka 2000 mapato ya Serikali kutokana na Uwindaji huo yalifikia zaidi ya USD milioni 9.3.  Hivyo ongezeko la mapato ya Serikali na idadi ya wanyama walio hatarini kutoweka duniani kama vile tembo ni matokeo ya utekelezaji wa mipango mizuri na sera sahihi za uhifadhi na matumizi endelevu.

 

4.0     Majibu ya hoja zilizotolewa:

 

4.1 . Kampuni ya Ortello Business Corporation kuwinda bila kufuata kanuni.

Kampuni hii ni mojawapo ya Kampuni za Uwindaji wa Kitalii 40 zinazowinda nchini.  Kampuni hiyo inamilikiwa na Serikali ya “United Arab Emirates (UAE)”.  Tofauti na Kampuni nyingine za Uwindaji, kampuni hiyo haifanyi biashara ya uwindaji wa kitalii.  Kampuni hiyo inawindisha wafalme na familia za falme za nchi za “United Arab Emirates” katika Pori Tengefu la Loliondo (Loliondo Game Controlled Area) kuanzia mwaka 1992.

 

          Katika kufanya uwindaji wa kitalii, kampuni hiyo hufuata sheria na kanuni zote za uwindaji wa kitalii ambazo   ni:-

 

4.1.1.   Kulipia “concession fee” ya USD 7,500.00 kwa kila kitalu

4.1.2.   Kuomba mgao (quota) wa wanyama wa kuwinda kabla ya kupewa kibali cha kuwinda.

4.1.3.   Kulipa ada ya kuwinda mnyama kulingana na kima kilichowekwa na Serikali.

4.1.4.   Kuwinda wanyama wale tu walioonyeshwa katika kibali cha kuwinda (Hunting permit). 

4.1.5.   Kutoa michango kwa ajili ya, kuendeleza eneo la kuwindia (Hunting block development), miradi ya maendeleo ya wananchi na uzuiaji ujangili.  Katika haya Kampuni ya OBC imefanya yafuatayo:

·        Imetoa fedha kiasi cha USD 46,000.00 kwa ajili ya maendeleo ya Wilaya ya Ngorongoro.

·        Kujenga Shule ya Sekondari ya Waso, Shule ya Msingi ya Waso, visima 6 vya maji, majosho ya ng’ombe na imenunua mabasi 2 ya kusafirisha wananchi.  Vilevile imetoa Tsh. 30 milioni kwa ajili ya vijiji 6 vilivyomo kwenye eneo la uwindaji, kwa ajili ya kusomesha elimu ya sekondari watoto 21.

·        Vilevile imenunua “generator” na pampu ya kusukuma maji ya thamani ya Sh. Milioni 11.0. na imejenga kiwanja cha ndege na barabara za kudumu.

 

4.1.6.   Tofauti na Kampuni nyingine, Kampuni ya OBC huwinda kwa miezi 4 kwa mwaka.  Kwa kawaida uwindaji unafanyika kwa kipindi cha miezi 6 kwa mwaka..  Aidha, Kampuni hii huwinda wanyama wachache tu kati ya wale walioidhinishwa katika kibali chake cha kuwinda.  

 

4.2.          Wanyama wanawindwa kwenye “Migratory Routes”:

Tanzania inaruhusu uwindaji katika Pori Tengefu la Loliondo (Loliondo Game Controlled Area) na siyo “migratory route” ya Masai Mara - Serengeti National Park.  Pori hilo ni mbuga ya wazi inayopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.  Upande wa mashariki.  “Migratory Route” ni eneo lililo kati ya Serengeti N.P. na Masai Mara.

Aidha, Pori Tengefu la Loliondo siyo mapito ya wanyama waendao Amboseli kama inavyodaiwa.

 

4.3.          Haki ya Tanzania ya kutumia wanyama wake katika               Pori la Loliondo G.C.A:

 

Wanyama walioko Tanzania ni mali ya Tanzania.  Hoja ya kwamba wanyama hao ni wa Kenya siyo sahihi.  Wanyamapori wa Loliondo G.C.A. hawana uraia wa nchi mbili.  Kwa vile baadhi ya wanyama hao wanahamahama toka Tanzania hadi Kenya na kurudi, basi ni vema tu kutambua kuwa wanyama ni wa Kenya au wa Tanzania katika kipindi wanapokuwa katika nchi husika. Wanyama wa Masai-Mara, Serengeti, Loliondo na Ngorongoro wapo katika “Ecosystem” moja.  Lakini Tanzania kama nchi huru inayojitegemea na yenye sera yake ina haki ya kisheria kutekeleza sera zake.  Hivyo hivyo Kenya inajitegemea na ina haki ya kutekeleza maamuzi yake ya kutowinda kulingana na utawala wake wa kisheria. Hivyo Tanzania haijakosa kuendesha uwindaji katika ardhi yake.

 

4.4     Uwindaji kutishia utalii wa Kenya:

Wanyama wengi wanahama toka Tanzania kwenda Kenya wakati mvua inanyesha upande wa Kenya. Na hivyo hivyo mvua zinapoacha kunyesha Kenya wanyama hao huhamia Tanzania. Wanyama wanaowindwa katika Pori Tengefu la Loliondo katika kipindi hicho ni wachache sana;  mwaka 2000 waliwindwa wanyama 150 tu na mwaka 2001 waliwindwa wanyama 139 tu.  Hivyo siyo kweli kwamba asilimia 80 ya wanyama wanaopatikana mpakani wanauawa.  Kwa misingi hiyo siyo kweli kwamba uwindaji unaofanywa na Kampuni ya OBC unatishia utalii wa Kenya. Tanzania (Katika mkutano wake na CITES Serecretariat uliofanyika Geneva (1993) haitoi idhini ya kuwinda tembo kiasi cha kilometa 10 kutoka mpaka wa Kenya.  Huu ni mfano wa hatua zinazochukuliwa kuzuia kinachoitwa na gazeti la East African  “haphazard hunting  of animals   of  Kenya”.

 

Aidha, siyo madai sahihi kuwa Idara ya Wanyamapori haielewi wanyama wanaouawa.  Udhibiti unafanywa na maofisa wa wanyamapori, Halmashauri za wilaya na vyombo vingine vya dola wakati uwindaji unapofanyika.  Vile vile Kampuni ya OBC haikamati wanyama na kuwasafirisha nje kwa vile haina leseni ya kufanya shughuli hiyo.

 

4.5     Kwamba ndege za kampuni ya OBC wakati zinaporuka toka Loliondo kwenda UAE zinasafirisha nje wanyama na ndege hai wa kila aina.

 

Biashara ya ukamataji na usafirishaji nje ndege, wanyama na viumbe hai inafanyika kulingana na sheria ya wanyamapori Na. 12 ya mwaka 1974, masharti ya "Convention on International Trade of Endangered Species of Wild Fauna and Flora (CITES). Aidha, biashara hii inafuata kanuni za “International Air Transport Association” - IATA juu ya vipimo vya masanduku ya kubebea ndege, wanyama na viumbe hai ili viumbe vinavyosafirishwa visife.  Aidha, msingi wa biashara ya wanyama hai ni kwamba biashara iwe endelevu (sustainable).  Vineingevyo CITES itakataza kusafirisha wanyama nje ya nchi ambayo matumizi ya wanyama wake siyo “sustainable”. Kwa maana hiyo CITES na hivyo nchi 156 duniani ambazo ni wanachama  wa CITES kwa pamoja zinatambua wazi kuwa biashara ya wanyama hai nchini Tanzania ni endelevu.

 

Wafanya biashara wa kusafirisha nje ya nchi wanyama, ndege na viumbe hai ni lazima wafuate utaratibu ufuatao:-

 

(i)                Kupata leseni ya biashara ya wanyama hai na nyara.

(ii)              Kupata kibali cha kukamata wanyama hai na hati miliki kwa ajili ya kumiliki wanyama waliokamatwa.  Idadi ya viumbe hai waliobainishwa kwenye hati miliki lazima walingane na wale walikamatwa na kuandikwa kwenye kibali cha kukamata.

(iii)            Kupata kibali cha kusafirisha nje (export permit /certificate)  wanyama hai walioandikwa kwenye hati miliki.

(iv)            Afisa wanyamapori aliye kwenye kituo cha kusafirisha nje "exit port" kama vile kiwanja cha ndege au mpakani kuthibitisha kuwa viumbe wanaosafirishwa ni wa aina ya wanyama walioandikwa katika hati ya kusafirisha nje.  Idadi ya wanyama hai lazima iwiane na idadi iliyobainishwa kwenye hati ya kuwasafirisha nje. 

 

Kazi ya kuthibitisha wanyama hai wanaosafirishwa nje  inafanywa kwa ushirikiano na watumishi wa Idara ya Forodha na Polisi.

 

(v)              Ndege inayosafirisha viumbe hai inakaguliwa na hati husika zinasainiwa na maofisa wa kampuni inayohudumia wasafiri na mizigo kwenye kiwanja cha ndege cha Dar es Salaam na Kilimanjaro (DAHACO).

(vi)            Kwa wanyama hai ambao wako chini ya kanuni za CITES, "Export" na "Import  certificate/permits" hutumika wakati wanyama hao wanaposafirishwa nje.  Kama kuna makosa yoyote ya kusafirisha wanyama hai wasioruhusiwa kulingana na kanuni za CITES, Mamlaka ya CITES iliyo katika nchi inayopokea wanyama (Importing Country) hutoa taarifa Makao Makuu ya CITES na nchi iliyosafirisha nje (Exporting Country) inafahamishwa kuhusu makosa yaliyofanyika na  wanyama husika wanarudishwa mara moja katika nchi walikotoka “exporting country”.

 

Kulingana na maelezo haya na misingi ya jinsi biashara ya wanyama hai inavyoendeshwa, madai ya kwamba ndege za OBC zinasafirisha nje wanyama hai kinyume na sheria na kanuni za CITES si za kweli; kwani vyombo vya serikali vinavyohusika katika kusimamia biashara hii vingetoa taarifa au kukamata wanyama hai waliokusudiwa kusafirishwa nje.  Aidha, serikali ingepata taarifa ya kukamatwa wanyama hai waliosafirishwa kinyume cha sheria na kanuni kutoka CITES Management  Authority ya UAE na “CITES Secretariat” yenyewe.     Serikali ya Tanzania haina kumbukumbu zozote za kuonyesha usafirishaji nje wa wanyama hai kwenda UAE kinyume na sheria.

 

 

 

 

 

4.6     Hoja nyingine (specific)

 

4.6.1  Wawindaji wa kitalii – kupewa vibali vya kuwinda vilivyo wazi (Blank permits)

 

Kabla Kampuni haijaanza kuwinda katika kitalu ilichopewa, hupewa kwanza mgao wa idadi ya wanyama anaoruhusiwa kuwindwa  (animal quota).  Kila  mwindaji hupewa kibali cha kufanya hivyo ambacho huonyesha aina na idadi ya wanyama anaoruhusiwa kuwinda kulingana na mgao wa idadi ya wanyama aliokuwa amepewe na aina ya safari.  Zipo aina nne za safari kama ifuatavyo: - safari ya siku 7, 14, 16 na 21.  Kila aina ya safari inabainisha aina ya wanyama wa kuwindwa na idadi yao.  Wakati mnyama yeyote akiuawa au kujeruhiwa, Askari Wanyamapori anayesimamia uwindaji anasaini kuthibitisha kuwa mnyama husika ameuawa. Kama mnyama  amejeruhiwa ni lazima atafutwe na kuhakikisha kwamba ameuwawa na hivyo kuzipa uwezekano wa kuwaua mnyama mwingine kama mbadala wa yule aliyejeruhiwa na kutoweka.  Utaratibu huo ni njia thabiti ya ufuatiliaji wa wanyama wanaowindwa na wawindaji wa kitalii.

 

4.6.2  Mikutano ya ujirani mwema kati ya Kenya na Tanzania

 

          Nchi za Kenya na Tanzania zinazo maeneo matatu ya kukutana kujadili masuala ya uhifadhi wanyamapori kama ifuatavyo:-

 

(a)              Jumuia ya Afrika Mashariki kwenye kamati maalum inayohusika na masuala ya uhifadhi wa mazingira na uendelezaji wa utalii. 

(b)             Mikutano ya Mkataba wa “Lusaka Agreement”.  Mikutano yote ya Mkataba huu, ambao Makao yake Makuu yako Nairobi,  hujadili uhifadhi na uzuiaji ujangili wa wanyamapori katika nchi zote wanachama.

(c)              Mikutano ya ujirani mwema, ambapo watendaji katika maeneo ya mpakani hukutana kuzungumzia maeneo ya ushirikiano kiutendaji, k.m. katika kuendesha operesheni za pamoja za kuzuia ujangili.  Kulingana na kanuni za kuendesha uwindaji wa kitalii, wanyama hawawezi kutishiwa kumalizika kwa sababu wanyama wanaowindwa ni madume na wenye umri mkubwa (wazee) ili kupata nyara (trophy) nzuri.  Nyara ndiyo kivutio kikubwa kwenye uwindaji huu.  Kutokana ukweli huu na kwa sababu uwindaji huu unafuata sheria, ndiyo maana suala la uwindaji wa kitalii hauongelewi katika vikao vilivyotajwa, kwa vile hoja hiyo siyo tatizo kwenye uhifadhi kwa pande zote mbili.

 

4.6.3  Ndege za UAE kuruka moja kwa moja hadi kiwanja cha ndege kilichopo Loliondo G.C.A na kurudi UAE bila kupitia Kilimanjaro International Airport.

         

Sheria ya Air Traffic ya Tanzania inataka ndege zote za nje zitue kwanza kwenye Uwanja wa Ndege wa KIA kabla hazijakwenda kwenye mbuga za wanyama.  Zikiwa KIA au DIA, Idara za Forodha na Uhamiaji zinatekeleza majukumu yake ipasavyo.  Hivyo hivyo wakati ndege hizo zinaporudi UAE hazina budi kutua kwanza KIA kwa madhumuni ya kufanyiwa uthibiti na Idara ya Forodha na Uhamiaji.  Hivyo madai kwamba ndege za UAE hazipitii KIA siyo sahihi.  Aidha, Mamlaka ya Usafiri wa Anga inadhibiti ndege zote ziingiazo nchini ikiwa ni pamoja na za UAE.

 

4.6.4. OBC inasambaza chumvi katika baadhi ya maeneo ya Loliondo G.C.A. kwa nia ya kuvutia wanyama toka Hifadhi ya Serengeti.

 

          Madai hayo hayana ukweli wowote.  Kanuni (Regulations) za uwindaji wa kitalii – 2000 – haziruhusu usambazaji wa maji na chumvi katika eneo la uwindaji kwa nia ya kuvutia wanyama wa kuwinda.  Aidha, Askari Wanyamapori wanaosimamia uwindaji wa kitalii katika eneo hili hawajatoa taarifa ya aina hiyo.   Kadhalika hakuna taarifa zozote kwamba Kampuni ya OBC inahusika na mioto inayochomwa kusini mwa Hifadhi ya Serengeti.

 

4.6.5. Serikali kufuta milki ya OBC ya kitalu cha Loliondo G.C.A. mwaka 1999 kwa vile OBC ilikuwa inasafirisha nje wanyama.

 

          Madai haya siyo sahihi.  Ukweli ni kuwa vitalu vinagawanywa kwa kampuni za uwindaji kila baada ya miaka mitano.  Mgao wa Vitalu uliofanyika mwaka 1995 kwa kampuni zote za uwindaji uliisha mwaka 1999.  Hivyo mgao uliofuata ulifanyika mwaka 2000 na   kampuni zilizopewa kutumia vitalu hivyo hadi 2004.

 

4.6.6. Familia ya Kifalme ya UAE kutoa misaada mbalimbali kwa Idara ya Wanyamapori.

 

          Hoja hii ni sahihi.  Idara ya Wanyamapori, ilipewa misaada mbalimbali na UAE ikiwemo magari, radio za upepo (Radio calls) na vifaa vya kufanyia kazi porini (field gears) mwaka 1996.  Hii ni sehemu ya kutekeleza matakwa ya kampuni zote zinazowindisha watalii,  kwamba ni lazima  wachangie katika uhifadhi na uzuiaji ujangili.

 

HITIMISHO

 

          Kumbukumbu za wizara zinaonyesha hakuna Wilaya yoyote, mbali na ya Ngorongoro, ambayo ina eneo la kuwindisha watalii ambalo linapata fedha nyingi kiasi cha ile inavyoelekezwa kwa wananchi wa Loliondo kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maendeleo ya wananchi kutokana na fedha za uwindaji wa kitalii.  (Kwa mwaka OBC anatoa wastani wa shs. 354,967,000 kuwaendeleza watu wa Loliondo).

         

          Aidha,  Serikali haioni sababu yoyote ya kuizuia kampuni ya OBC kuendelea na shughuli za uwindaji katika Pori Tengefu la Loliondo.  Serikali inaona wanavijiji na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro wanafaidika kimaendeleo kutokana na  uwindaji unaofanywa.