Afya

Vipaumbele vya Wizara ya Afya 2025/2026

i.  Kuimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza yakiwemo magonjwa ya milipuko, magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, magonjwa yasiyoambukiza na huduma za Lishe kwa kutekeleza afua mbalimbali ikiwemo: -  

a. Kuendelea kuimarisha usimamizi katika Mikoa 20 na kuanzisha vituo vya Operesheni ya Matukio ya Dharura za Afya (PHEOCs) katika mikoa sita (6) ya Simiyu, Geita, Pwani, Njombe, Singida na Shinyanga kwa ajili ya kuratibu, kujiandaa, kukabiliana na dharura za afya ikiwemo milipuko ya magonjwa;

b. Kukamilisha uanzishwaji wa Programu ya Taifa yaLishe nchini;

c. Kuendelea kuimarisha huduma za afya mipakani kwa kujenga Miundombinu ya kuwatenga wahisiwa wa magonjwa ya kuambukiza katika mipaka 16 na ununuzi wa magari matano (5), boat ambulance tatu (3) na vipima joto tembezi 28;

d. Kuendelea kutekeleza Programu ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kwa kuwajengea uwezo Wahudumu 28,000 kutoka Mikoa yote; na

e. Kuendelea kuimarisha huduma za chanjo kwa kuwafikia Watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wasichana na mama wajawazito. 

  ii.  Kuimarisha upatikanaji na ubora wa huduma za afya zinazotolewa katika ngazi zote kuanzia zahanati hadi taifa kwa kutekeleza afua mbalimbali ikiwa ni pamoja na: - 

a. Kuimarisha matumizi ya TEHAMA ikiwemo matumizi ya akili mnemba (Artificial Intelligence) ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kuunganisha mifumo iweze kusomana, kubadilishana taarifa na kupunguza gharama za huduma za afya nchini; 

b. Kuhuisha na kuzindua Sera ya Afya pamoja na Mkataba wa Huduma kwa Mteja (Client Service Charter);

c.  Kuanzisha Taasisi ya Taifa ya Afya ya Jamii (National Public Health Institute); 

d. Kuimarisha Hospitali ya Benjamin Mkapa ili kuwa na hadhi ya Hospitali ya Taifa; 

e. Kuanzisha kituo cha umahiri cha Afrika Mashariki cha matibabu ya magonjwa ya damu na uloto katika hospitali ya Benjamin Mkapa;

f. Kuanzisha kituo cha kimataifa cha upandikizaji figo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa. Kituo hicho kitakuwa ni kituo kikubwa na kitaongoza katika ukanda wa kusini mwa jangwa la sahara; 

g. Kuzitangaza na kuzipa hadhi ya kuwa taasisi Hospitali za Afya ya Akili Mirembe na Hospitali ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya; 

h. Kuimarisha ufuatiliaji, uratibu na udhibiti wa usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa (Antimicrobial Resistance) na kusimamia uingizaji na matumizi sahihi ya Antibiotics nchini;

i.  Kuongeza kasi ya matumizi ya Tiba Mtandao (Telemedicine) ili kusaidia utoaji wa huduma za ushauri, ubingwa na ubingwa bobezi kwa maeneo yasiyo na wataalam hao;

j.  Kuweka mazingira wezeshi ya viwanda vya ndani vya kuzalisha bidhaa za afya ili kuwezesha upatikanaji wa bidhaa hizo kwa urahisi na unafuu wakati wote; 

k.  Kuendelea kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya (dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi) kwa kuboresha mifumo ya maoteo, ununuzi, utunzaji na usambazaji wa dawa na bidhaa nyingine katika ngazi zote za utoaji wa huduma za afya;

l.  Kuwezesha Hospitali ya Taifa, Hospitali Maalum, Hospitali za Rufaa za Kanda na Hospitali za Rufaa za Mikoa kujiunga katika mchakato wa kupata ithibati ya kimataifa hivyo kuongeza viwango vya ubora wa huduma na kukuza utalii wa tiba nchini; na

m. Kuwezesha upatikanaji wa huduma za mama mwambata na matumizi ya chati ya uchungu iliyoboreshwa katika ngazi zote za kutolea huduma za kujifungua kwa akina mama wajawazito.

   iii.  Kuimarisha mifumo ya ugharamiaji wa huduma za afya nchini ikiwa ni pamoja na kuendelea na utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote kwa kutekeleza afua mbalimbali pamoja na: -

a. Kutenga fedha kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya Sera za Kimataifa katika ufadhili wa Sekta ya Afya; na

b. Kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote nchini kwa kuanza uandikishaji wa makundi mbalimbali. 

 iv.  Kuendelea kufanya tafiti na kuhimiza matumizi ya matokeo ya tafiti hizo kwa maeneo ya kimkakati kwa kutekeleza afua mbalimbali ikiwemo: -

a. Magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo Saratani na afya ya akili; 

 b. Magonjwa ya kuambukiza ikiwa ni pamoja na magonjwa ya milipuko;

c. Usugu wa vimelea dhidi ya dawa; na 

d. Dawa za tiba asili na tiba mbadala.

 v.  Kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga kwa kutekeleza afua mbalimbali ikijumuisha: - 

a. Kuendelea na ununuzi na usambazaji wa dawa muhimu za uzazi salama pamoja na dawa za uzazi wa mpango, dawa kinga za minyoo, dawa za kuongeza damu, dawa za Malaria, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi;

b. Kuimarisha upatikanaji wa dawa ya vidonge myeyuko vya amoxycillin, ORS/Zinc kwa ajili ya kutibu nimonia na kuhara kwa Watoto, dawa za Surfactant na vifaa vya kusaidia upumuaji (CPAP) ili kusaidia changamoto za upumuaji kwa watoto waliozaliwa kabla ya wakati na waliozaliwa na uzito pungufu; na  

c. Kuendelea na ununuzi wa vifaa tiba vya wodi 100 maalum za watoto wachanga wagonjwa na waliozaliwa na uzito pungufu.

 vi.  Kuimarisha upatikanaji na uendelezaji wa wataalam katika Sekta ya Afya kwa fani za kati, ubingwa na ubingwa bobezi kwa kutekeleza afua mbalimbali ikiwemo:-

a.   Kuendelea kutoa ufadhili wa mafunzo ndani na nje ya nchi kwa utaratibu wa Seti kwa wataalam wa ngazi ya ubingwa na ubingwa bobezi na kufadhili mafunzo ya kada za kati za kimkakati; 

b.   Kuendelea kutoa mafunzo ya afya ya kada za kati katika vyuo vya afya vya umma; na 

c.    Kusimamia ubora wa mafunzo katika vyuo vya umma na binafsi.

 

vii.  Kuimarisha huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi pamoja na kuimarisha tiba utalii nchini kwa kutekeleza afua mbalimbali ikiwa ni pamoja na :- 

a.   Kuendelea kutoa huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi katika Hospitali ya Taifa, Hospitali maalum, Hospitali za Rufaa za Kanda na Hospitali za Rufaa za Mikoa pamoja na kuanzisha na kuimarisha huduma mpya kulingana na mahitaji;

 b.   Kuanzisha kiwanda cha kuzalisha viungo tiba na viungo saidizi (Prostheses Manufacturing Plant) katika Hospitali ya Kanda KCMC; na

c.    Kuendeleza na kuimarisha huduma za mkoba za kimkakati za ubingwa na ubingwa bobezi ndani na nje ya nchi (International Medical Camps)

 viii.  Kuendeleza na kusimamia afua za Tiba Asili na Tiba Mbadala kwa kutekeleza afuazinazojuisha :-

a.  Kuongeza Hospitali zinazotoa huduma jumuishi za Tiba Asili kutoka Hospitali za Rufaa za Mikoa 14 hadi 21; 

b.  Kuendeleza huduma za Tiba Asili kwa kufanya tafiti, kuongeza na kuendeleza mashamba ya miti dawa kwa kila kanda ili kuhamasisha uzalishaji endelevu wa dawa za tiba asili; na

c.    Kuhamasisha usajili wa dawa asili na tafiti za majaribio ya dawa. 

 ix.  Kuimarisha upatikanaji wa huduma za tiba dhidi ya magonjwa ya kuambukiza, magonjwa yasiyoambukiza na magonjwa ya mlipuko kwa kutekeleza afua mbalimbali pamoja na :-

a. Kuimarisha uzalishaji wa viuadudu katika viwanda vya ndani, kununua na kusambaza vyandarua, vitendanishi na dawa za Malaria;

b. Kuimarisha udhibiti na kutokomeza Kifua Kikuu na Ukoma, UKIMWI, Homa ya Ini na magonjwa ya ngono; 

c. Kufufua kiwanda cha Tanzania Pharmacetical Industry (TPI) kilichopo Arusha cha kuzalisha dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI;

d. Kuanza hatua za awali za uanzishwaji wa viwanda vya bidhaa za tiba zitokanazo na pamba; na

e. Kuhamasisha wawekezaji kuanzisha viwanda vya kuzalisha chanjo na dawa za kupunguza makali ya UKIMWI.

 x.  Kuimarisha huduma za afya ya akili, huduma za utengamao hususan kwa watoto, wazee na watu wenye ulemavu kwa kutekeleza afua mbalimbali ikiwemo:-

a. Kuimarisha utambuzi wa mapema wa watoto wenye ulemavu kwa kununua vifaa vya uchunguzi wa usikivu na macho kwa Hospitali za Rufaa za Mikoa 14 na Hospitali za Kanda 5 na kuimarisha huduma za utengamao katika Hospitali za Halmashauri 50;

b. Kuongeza idadi ya Hospitali za Rufaa za Mikoa zinazotoa huduma tatu za utengamao za Viungo tiba na viungo Saidizi (Prosthetics and Orthotics), Fiziotherapia (Physiotherapy), Tiba kwa Vitendo (Occupational Therapy), kutoka nane (8) hadi 18; 

c. Kuendelea kuhamasisha uanzishwaji wa Klabu za Afya za Wazee (Healthy Ageing Clubs) katika ngazi ya Halmashauri ili kuongeza idadi kutoka 14 hadi 30; na

d. Kuhuisha Mkakati wa Afya ya Akili ili kuboresha huduma hizo nchini.

 

 

Mama Kinara

Kitendea kazi cha “Mama Kinara” kimetengenezwa na jumla ya Mama Kinara 818 na Wakufunzi 40 walipata mafunzo yaliyofanyika katika mikoa ya Morogoro, Pwani, Tanga, Dodoma, Manyara, Arusha, Mwanza, Shinyanga, Geita na Tabora. Hadi sasa jumla ya akinamama 68,028 wanaonyonyesha walio na VVU wamefikiwa kati ya akinamama 73,935. Lengo la hatua hii ni kuhakikisha wanawake wenye maambukizi ya VVU/UKIMWI wananyonyesha Watoto wao ili kuweza kuwafanya wawe na afya bora.

Wizara imeanzisha afua mpya ya Mama Kinara katika ngazi ya Jamii kwa ajili ya kuwezesha ufuatiliaji wa wajawazito na akina mama wanaonyonyesha ambao wamekwisha thibitika kuwa na maambukizi ya VVU.

Wizara inaboresha afua mbalimbali ambazo zinahamasisha wananchi kwenda kupima na kutambua hali zao za maambukizi ya VVU/UKIMWI, ili waweze kupatiwa huduma za ushauri, upimaji, matunzo na huduma za dawa kwa haraka pale inapoonekana kuwa wameambukizwa. Jumla ya wateja 1,519,013 sawa na asilimia 84.6 ya watu 1,795,905 wanaokadiriwa kuishi na virusi vya UKIMWI nchini walikuwa wanatambua hali zao za maambukizi.

Kati yao, wateja 1,507,686 sawa na asilimia 99.3 walikuwa wameanza kutumia dawa za kufubaza Virusi vya UKIMWI (95 ya pili). Aidha, asilimia 95.8 ya wateja waliokuwa wanatumia dawa za ARV nchini walikuwa wamefubaza wingi wa virusi vya UKIMWI ambayo ni sawa na chini ya nakala 1,000 (95 ya tatu). Idadi ya vituo vinavyotoa huduma ya Tiba ya UKIMWI (CTC) vimefikia 6,759 na kati ya hivyo CTC kamili ni 3,075 na vituo vya huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto (RCHS) vinavyotoa huduma ya kutoa dawa ya kufubaza Virusi vya UKIMWI vipo 3,684. 

Aidha, Wizara ilisaini mwongozo wa utekelezaji wa utoaji dawa kinga na kuanza kwa huduma hiyo, jumla ya walengwa 13,285 walianza huduma hiyo katika Mikoa yote nchini. Huduma ya Kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) zinatolewa katika vituo 6,996 sawa na asilimia 98 kati ya vituo 7,138 vinavyotoa huduma za afya ya uzazi na Mtoto. 

Pia, Wizara imepanua huduma ya upimaji wa pamoja wa VVU na kaswende kwa wajawazito ambapo jumla ya vituo 3,497 kati ya 7,138 sawa na asilimia 49 vinavyotoa huduma za afya ya uzazi na mtoto vimeanza kupima VVU na kaswende kwa kutumia kitepe kimoja, lengo ni vituo vyote viweze kutoa huduma ya upimaji huo.

Wizara imeendelea kupanua huduma za upimaji wa Watoto wachanga waliozaliwa na akina mama wenye VVU kutoka Idadi ya vituo vinavyotoa huduma hizi kutoka vituo 50 mwaka 2020 hadi vituo 141 mwaka 2021. Upimaji huo hufanyika kwa kutumia vinasaba vya VVU mahali zitolewapo huduma (EID Point of Care). Jumla ya watoto 54,134 waliozaliwa na akina mama wanaoishi na VVU walipimwa vinasaba vya VVU na kati yao watoto 1,299 sawa na asilimia 2 walikutwa na maambukizi ya VVU na wote waliunganishwa na huduma ya matibabu lengo ni kuzuia kabisa maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto.

 

 

Usichukulie Poa Nyumba ni Choo

Wizara inaratibu na kusimamia utekelezaji wa awamu ya pili ya Kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira yenye kaulimbiu isemayo “USICHUKULIE POA NYUMBA NI CHOO” yenye lengo la kuhimiza ujenzi na matumizi ya vyoo bora na vifaa vya kunawia mikono vyenye maji tiririka na sabuni katika ngazi ya kaya na Taasisi.


Kupitia kampeni hii, idadi ya kaya zenye vyoo bora imeongezeka kutoka asilimia 64 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 72 mwezi Machi, 2022. Vilevile, kaya zenye vifaa vya kunawia mikono vyenye maji tiririka na sabuni zimeongezeka kutoka asilimia 40 Mwaka 2020 kufikia asilimia 41 mwezi Machi, 2022. Watanzania wanaendelea kuhimizwa kuzingatia kanuni za usafi binafsi na usafi wa mazingira ili kujikinga na magonjwa mbalimbali kwani Kinga ni Bora kuliko Tiba.

Mafanikio katika Sekta ya Afya kwa mwaka 2020-2025

 

Kujenga vituo vya kutolea huduma za upasuaji kutoka vituo 388 hadi kufikia vituo 577; Imeongeza vyumba maalum (NCU) kwa ajili ya huduma za watoto wachanga wenye changamoto mbalimbali ikiwemo uzito pungufu kutoka 80 hadi kufikia 362;

Kuimarika kwa huduma za Mkoba za Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia, kumewezesha kuwafikia watanzania zaidi ya 154,015 ikiwemo wanawake katika Halmashauri zote nchini pamoja na kujengea uwezo watumishi 9,434;

​​​​​​​Akinamama 135,526 wameokolewa maisha yao wakati wa uzazi kupitia Mfumo wa rufaa za dharura wa M-Mama ulio asisiwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na unaotekelezwa nchi nzima. 

Maono ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu uzazi salama, mifumo bora ya rufaa, uwajibikaji katika utendaji, miundombinu, vifaa na vifaa tiba na ushirikishwaji wa vyama vya kitaaluma vimewezesha kupunguza vifo vya akinamama vitokanavyo na uzazi kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000.

 

Mafanikio hayo yamesababisha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutunukiwa tuzo ya kimataifa ijulikanayo kwa jina la Goalkeeper Award, iliyotolewa na Taasisi ya Gates ya Marekani, tarehe 4 Februari, 2025. Tuzo hii hutolewa kwa Viongozi waliofanikiwa kutekeleza kwa mafanikio Malengo ya Maendeleo Endelevu:

 

Mheshimiwa Rais amekuwa Rais wa kwanza Barani Afrika kutunukiwa tuzo hii;

Amekuwa Rais wa kwanza mwanamke kutunukiwa tuzo hii;

Amekuwa ni Rais wa kwanza kutunukiwa tuzo hii nchini kwake;

Amekuwa ni Rais wa kwanza Duniani kutunukiwa tuzo ya kuokoa vifo vya wanawake wakati wa uzazi; na

Amekuwa ni Rais wa kwanza kupokea tuzo hiyo na kuikabidhi kwa watumishi wa Sekta ya Afya waliochangia kuokoa vifo vya akinamama na watoto.

 

Mheshimiwa Rais na Serikali yake ameanzisha Mpango Jumuishi na Shirikishi wa Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii kwa lengo la kuwafikia wananchi katika ngazi ya kaya. Wahudumu hao ni macho yetu, masikio yetu na mikono yetu katika kaya, vijiji na mitaa wenye jukumu la kuelimisha, kutambua mazingira hatarishi ya kiafya mapema na kuwezesha jamii na Serikali kuchukua hatua za udhibiti mapema. Wahudumu hao si tu watoa huduma, bali ni viongozi wa mabadiliko ya afya katika jamii zao. Hivyo natoa wito kwa wananchi kuwapokea na kuwapa ushirikiano wanapokuwa kwenye majukumu yao maana ni kiungo muhimu katika kufikia afya bora kwa wote. Mpaka sasa jumla ya wahudumu 12,832 wamechaguliwa na kati yao 3,706 wamehitimu mafunzo na 4,309 wanaendelea na mafunzo katika vyuo 45 nchini. Lengo ni kufikia wahudumu ngazi ya jamii 137,294 ifikapo 2029.

Kuongezeka kwa miundombinu yenye ubora ya kutolea huduma za afya katika ngazi zote ikiwemo ukamilishaji wa miradi ifuatayo:-

Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Geita, Njombe, Songwe, Simiyu, Katavi na Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kwangwa;

Jengo la huduma za tiba mionzi kwa matibabu ya magonjwa ya Saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) na Huduma hizo zitaanza kutolewa rasmi tarehe 25 Juni 2025;

Jengo la Damu Salama katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma-Maweni; ​​​​​Maabara yenye uwezo wa Usalama wa Kibailojia Daraja la 3 katika hospitali ya Kibong’oto. Maabara hii ni mojawapo ya maabara tano (5) Afrika zenye hadhi ya kuwa maabara za rufaa za kimataifa;

Vichomea taka 44 katika mikoa yote kikiwemo kichomea taka maalum chenye uwezo wa kuteketeza taka tani moja kwa saa mbili;

Vituo vya kutolea huduma za afya kutoka 10,153 mpaka kufikia vituo 12,846;

Vitanda vya wagonjwa mahututi (ICU) kutoka vitanda 258 hadi kufikia vitanda 1,362; na  

Vitanda vya kulaza wagonjwa wa kawaida kutoka vitanda 86,131 hadi vitanda 153,683.

 

“Ongezeko la miundombinu ya kutolea huduma za afya nchini limeiwezesha Serikali kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi kama inavyoelekezwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 - 2025. Hadi sasa wastani wa asilimia 80 ya wananchi wanapata huduma za afya ndani ya kilometa 5 za maeneo wanayoishi, lengo ni kufikia asilimia 95 ifikapo mwaka 2030”.

 

Mafanikio makubwa yamepatikana katika huduma za uchunguzi na Vifaa tiba:-

MRI zimeongezeka kutoka saba (7) hadi kufikia 13 na zinapatikana katika Hospitali zote za Kanda, Hospitali Maalum na Hospitali ya Taifa nchini;

CT Scan zimeongezeka kutoka 12 hadi 45 na zinapatikana katika Hospitali zote za Rufaa za serikali na binafsi;

​​​​​​​Ultrasound kutoka 476 hadi 970 zimesambazwa hadi katika ngazi ya Vituo vya Afya nchini;

Angio Suite kutoka 4 hadi 5;

​​​​​​​Fluoroscopy kutoka 9 hadi 13;

​​​​​​​Digital X-ray 147 hadi 491;

Cathlab moja (1) hadi nne (4); na

PET CT - Scan haikuwepo sasa ipo moja (1) yenye thamani ya Shilingi Bilioni 18.5 na yenye kazi ya uchunguzi na ufuatiliaji wa matibabu ya wagonjwa wa saratani.

Kuongezeka kwa vifaa na vifaa tiba vya uchunguzi kumepunguza rufaa za ndani na nje ya nchi, kumewezesha kusogeza huduma kwa wananchi kwa gharama nafuu na kusaidia kutoa matibabu yenye ubora zaidi na kwa wakati.

‘Mheshimiwa Spika, Tanzania ni miongoni mwa nchi Mbili (2) kati ya nane (8) zilizopo kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki na ni miongoni mwa nchi Tatu (3) katika Jumuiya ya SADC na kwa Bara la Afrika ni moja kati ya nchi tisa (9) zenye mashine ya PET CT - Scan’.

Serikali imefanikiwa kuimarisha huduma za uokoaji wakati wa dharura kwa kupunguza vifo vya wananchi kwa asilimia 40 hadi 50 kutokana na kuongezeka kwa idadi ya majengo ya kutolea huduma za dharura kutoka 7 hadi 125 katika hospitali ngazi ya Kanda hadi Taifa. Vilevile Serikali imeongeza magari ya kubebea wagonjwa kutoka 540 hadi 1,267 ili kuimarisha huduma za uokoaji wakati wa dharura.

​​​​​​​Ubora wa huduma umeimarika kwa kuongeza rasilimali watu kutoka 48,633 hadi kufikia watumishi 177,711 wenye ajira za kudumu.

Kupitishwa kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote na Kanuni zake  zitakazowezesha wananchi kupata huduma za afya bila kikwazo cha fedha na kuelekea kufikia lengo la kidunia la huduma za afya kwa wote (Universal Health Coverage).

​​​​​​​Kuimarika kwa makusanyo ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kutoka Shilingi Bilioni 560.8 hadi 619.8. Ongezeko hilo limeimarisha Uhai na uhimilivu wa Mfuko.

​​​​​​​Idadi ya wataalam bingwa na ubingwa bobezi imeongezeka kutokana na Samia Health Super Specialization Scholarship Program kutoka 2,188 hadi 4,967. Lengo la Serikali katika kuanzisha program hii ni pamoja na;

Kupata wataalam wa afya wenye ubingwa na ubobezi ndani ya nchi watakaokuza uwezo na ujuzi kwa wataalam wa ndani

Kupunguza rufaa za nje na ndani

Kupunguza gharama za matibabu na

Kupunguza utegemezi wa wataalam wa nje

Kuimarisha upatikanaji wa huduma za ubingwa bobezi kwa wananchi wasio na uwezo wa kugharamia matibabu ambapo jumla ya Shilingi Bilioni 11 zimetolewa. Wananchi 1,022 wamenufaika na mpango huo na kupatiwa huduma bobezi katika Hospitali ya Taifa, Hospitali Maalum na Hospitali za Kanda. Aidha baadhi ya huduma zilizotolewa ni Upandikizaji wa figo, vifaa vya usikivu, uloto, upasuaji wa moyo, upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo.

“Huu ni ubunifu alioutoa mama Samia katika kuwawezesha wananchi wasio na uwezo kuweza kupata huduma za ubingwa bobezi. Upatikanaji wa fedha hizo pamoja na kuwawezesha wananchi kupata huduma, umewezesha ukuaji na ubora wa huduma zinazotolewa na taasisi zetu za afya hapa nchini”.

Kuimarika na kuongezeka kwa hali ya upatikanaji wa bidhaa za afya muhimu za kipaumbele 382 kutoka asilimia 58 mpaka asilimia 87 pamoja na kuongezeka kwa viwanda vya dawa, vifaa na vifaa tiba kutoka 23 hadi 92. Ongezeko hilo la viwanda limepunguza uagizaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba kutoka nje ya nchi kwa asilimia 20“Nitumie fursa hii, kumshukuru tena Mheshimiwa Rais kwa kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya nchini ambapo jumla ya Shilingi Bilioni 183.2 sawa na asilimia 91.6 zimekuwa zikitolewa kila mwaka. Aidha, Serikali imeendelea kukiimarisha MSD kwa kuipatia mtaji wa jumla ya shilingi bilioni 150 ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa MSD”.

Kuongezeka kwa uzalishaji wa dawa za kuua viluwiluwi wa mbu katika kiwanda cha Kibaha ambapo Serikali imetoa jumla ya Shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya ununuzi wa dawa ambazo zimewezesha ununuzi wa lita 833,333.3 na zinaendelea kusambazwa katika Halmashauri zote nchini.

​​​​​​​Kuendelea kuimarika kwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba nchini (TMDA) kwa kuendelea kuwa kinara katika ngazi ya tatu (Maturity Level 3) kwa viwango vya Shirika la Afya Duniani.

​​​​​​​Kuimarika kwa tiba utalii nchini ambapo wagonjwa kutoka nje ya nchi wameongezeka kutoka 5,705 hadi 12,180.

​​​​​​​Kuongezeka kwa vituo vya menejimenti ya dharura za afya kutoka mikoa sita (6) hadi 20 vilivyoimarisha ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu za kukabiliana na magonjwa ya milipuko.

Kuimarika kwa uwezo wa nchi katika uchunguzi wa kimaabara wa magonjwa mbalimbali ikiwemo ununuzi wa Maabara jongezi mbili (2).

​​​​​​​Kuimarika kwa usalama wa afya mipakani kwa kusimika mashine 16 za kisasa za uchunguzi wa jotomwili kwa ajili ya kuchunguza wasafiri wote wanaoingia na kutoka nchini.

​​​​​​​Kukamilika kwa ujenzi wa maghala tisa (9) ya kuhifadhia chanjo pamoja na ununuzi wa magari 96 na pikipiki 300 kwa ajili ya kusambaza chanjo ambako kumepelekea kuongezeka kwa kiwango cha utoaji wa huduma za chanjo kutoka asilimia 81 hadi kufikia asilimia 97 ambacho ni zaidi ya kiwango kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani cha asilimia 90.

Maisha ya wananchi yameokolewa dhidi ya magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kwa kufanya upasuaji wa mabusha kwa watu 11,228 na kufanya upasuaji mdogo wa usawazishaji wa vikope kwa watu 13,779. 

​​​​​​​Kuboresha hali ya lishe nchini kwa kuongeza mashine 230 za kunyunyizia virutubishi (dosifiers) kwenye vyakula na kufikia 1,402 zilizofungwa katika mikoa yote nchini.

 

Lishe bora ni muhimu kwa uhai

Lishe bora ni muhimu kwa uhai, ukuaji na maendeleo ya binadamu kiakili na kimwili na hivyo kuchangia katika kuongeza tija katika uzalishaji mali kwa kaya na kuimarisha uchumi wa jamii na Taifa kwa ujumla.

Wizara imefanya utafiti wa hali ya lishe kwa wanafunzi wa shule za msingi za Serikali nchi nzima, ambapo jumla ya wanafunzi 63,000  kutoka shule 650 wamefanyiwa tathmini ya hali ya lishe na kudodoswa masuala ya ulaji na wanafunzi 21,000 wamepimwa kiasi cha damu. Utafiti huu umefanyika mwezi Agosti na Oktoba, 2021,uchakataji wa takwimu unaendelea. Matokeo ya utafiti huu yatachangia katika kuboresha hali ya lishe kwa vijana hususani walioko mashuleni. 

Aidha, Serikali imeendelea kuimarisha lishe na afya ya watoto wachanga na wadogo kwa kuendelea kutekeleza Kampeni ya Kitaifa ya utoaji wa matone ya Vitamini A kwa watoto walio chini ya miaka mitano.  Malengo ya kampeni ya mwaka 2021/22 yalikuwa ni kutoa matone ya Vitamin A kwa watoto 8,248,450, kati ya umri wa miezi (6 – 59). 


Zoezi hili lilikamilika kwa kuweza kuwafikia walengwa 8,015,463 sawa na asilimia 97.2 ikilinganishwa na asilimia 95 ya mwaka 2020. Vilevile, Wizara imeendelea kuimarisha huduma za matibabu ya utapiamlo mkali kwa watoto kwa kuimarisha upatikanaji wa chakula dawa, upatikanaji wa vifaa vya kufanyia tathmini ya hali ya lishe pamoja na kuboresha miundombinu ya kufanyia matibabu ya utapiamlo mkali kwa watoto.

Pia vituo vinavyotoa matibabu ya utapiamlo mkali kwa kulaza vimeongezeka kutoka vituo 365 mwaka 2020 kufikia vituo 385 vya kutolea huduma za afya hadi kufikia Machi, 2022. 

Wizara kwa kushirikiana na wadau wa lishe nchini imefanya maadhimisho ya Siku ya Lishe Kitaifa tarehe 18 – 23 Oktoba, 2021.Uzinduzi na Kilele cha Maadhimisho hayo umefanyika Mkoani Tabora. Aidha, Wizara ilifanya uraghibishi na mafunzo kwa timu za uendeshaji wa huduma za afya za Mikoa na Halmashauri (RHMT na CHMT) pamoja na watoa huduma za Afya kuhusu uanzishwaji wa vitengo vya kuratibu huduma za Lishe kwenye Vituo vya kutolea huduma za Afya katika Mikoa ya Tabora,Manyara na Dodoma, ambapo jumla ya watoa huduma 150 wamejengewa uwezo.

Mpangilio