Katiba na Sheria

Muhtasari

Tembelea www.sheria.go.tz

Wizara ya Katiba na Sheria ndiyo mhimili mkuu wa masuala yote ya kisheria nchini. Bila shaka ni kutokana na umuhimu huu, ndiyo sababu Wizara hii ikawa na umri wa miaka 55 sawa na umri nchi yetu hii leo.

Historia ya Wizara ilianza mwaka 1961 wakati Waziri Mkuu wakati huo, Hayati Julius Nyerere alipomteua Chifu Abdallah Fundikira kuwa Waziri wa Sheria wa Kwanza Mzalendo kabla nafasi hiyo kuchukuliwa na Sheikh Amri Abeid Kaluta mwaka 1963 na baadaye Mhe. Hassan Nassor Moyo kuanzia mwaka 1964 aliyeshika nafasi hiyo hadi 1966. Baada ya hapo shughuli za Wizara zilihamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais chini Hayati Rashid Mfaume Kawawa.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1975, Wizara na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ziliunganishwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 10 la mwaka 1975 na Mhe. Jullie Manning aliteuliwa kuwa Waziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali hadi mwaka 1982 alipoteuliwa Mhe. Joseph Warioba kushika nafasi hizo. Utaratibu huu uliendelea hata baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1985 wakati Mhe. Damian Lubuva alipoteuliwa kushika nyadhifa hizo mbili hadi mwaka 1990.

Mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa mwaka 1990 yalipelekea Waziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutenganishwa tena na hivyo kofia ya Uwaziri na kofi ya Uanasheria Mkuu wa Serikali zikatofautishwa. Wakati huo, shughuli za Waziri zilihamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikabaki kuwa Idara inayojitegemea chini ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais. Mabadiliko haya yalifanywa kupitia Tangazo la Serikali Na. 140 la mwaka 1990.

Mwaka 1993, Rais Alli Hassan Mwinyi aliirudisha tena Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba na kumteua Mhe. Samuel Sitta kuwa Waziri na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikabaki kuwa Idara inayojitegemea chini ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, Rais Benjamin Mkapa aliendelea na Wizara hii kupitia Tangazo la Serikali Na. 720 la mwaka 1995 na kumteua Mhe. Harith Mwapachu kuwa Waziri. Katika muundo huu mpya, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilirudishwa chini ya Wizara hii kutoka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na Katibu Mkuu wa Wizara akawa pia ndiye Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mwaka 2005, baada ya Uchaguzi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete aliunda tena Wizara hii wakati huu ikiitwa Wizara ya Katiba na Sheria. Hata hivyo, ili kuongeza ufanisi, mwaka 2008 kufuatia mapendekezo ya Tume ya Jaji Mark Bomani, Wizara ilitenganishwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali hatua iliyopelekea pia kutenganishwa kwa nafasi ya Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali na ile ya Katibu Mkuu wa Wizara.

Mfumo Endelevu wa Kupambana na Rushwa - BSAAT

Wizara ya Katiba na Sheria ni moja ya Taasisi nufaika ya utekelezaji wa Programu ya BSAAT ambayo imejikita katika kutekeleza majukumu yanayohusiana na maboresho ya Mfumo wa Haki Jinai nchini hususan katika maboresho ya mifumo ya kisera na kisheria ambayo yana mchango mkubwa wa kuweka mazingira rafiki ya mapambano dhidi ya rushwa.

Mradi huu umeanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2019/2020 na unatarajia kukamilika ifikapo mwaka 2024/2025. Vilevile, maandalizi ya programu hii awamu ya pili unaendelea ambapo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano baada ya awamu ya kwanza kukamilika.

Malengo ya mradi huu ni pamoja kuzijengea Taasisi za Haki Jinai uwezo wa kupambana na rushwa nchini kwa maendeleo endelevu ya Taifa.

Matokeo tarajiwa ya programu hii ni pamoja na kuweka mifumo imara ya kisera na kisheria katika mapambano dhidi ya rushwa kubwa nchi ambazo ni kikwazo cha maendeleo na kupambana na umaskini nchini na kuongeza wigo wa kushughulikia mashauri makubwa ya rushwa kwa wakati.

Mradi huu unatekelezwa na Wizara ya katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mahakama ya Tanzania na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.

Taasisi zilizo chini ya Wizara

1. Mahakama Kuu ya Tanzania www.judiciary.go.tz

2. Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali www.agctz.go.tz

3. Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali www.osg.go.tz

4. Ofisi ya Taifa ya Mashtaka www.nps.go.tz

5. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora www.chragg.go.tz

6. Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini www.rita.go.tz

7. Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania www.lrct.go.tz

8. Tume ya Utumishi wa Mahakama www.jsc.go.tz

9. Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo www.lst.go.tz

10. Chuo cha Uongozi wa Mahakama www.ija.go.tz

Mradi wa Haki Mtandao (e-Justice)

Mradi huu unalenga kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika Sekta ya Sheria na kuunganisha mifumo ya taasisi ya utoaji huduma za kisheria kwa njia za kielektroni ili kuongeza ufanisi, kuharakisha upatikanaji wa haki na kupunguza gharama za utoaji wa huduma hizo. Matokeo ya awali ya mradi huu ni kuwa na mifumo iliyoainishwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa Taasisi za Haki Jinai nchini. Matokeo ya Kati ya Mradi huu ni kuona haki Jinai inapatikana kwa wakati nchini. Matokeo ya muda mrefu ni kuwa na Mfumo wa haki jinai unaochangia maendeleo endelevu ya nchi

Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia

Kampeni hii inafanyika kwa miaka mitatu kuanzia mwezi Machi, 2023 hadi mwezi Februari, 2026 katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar. 

Kampeni inajikita katika kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi hususan katika masuala ya ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi, mirathi, usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala, na masuala yahusuyo haki za binadamu kwa ujumla. Utekelezaji wa kampeni unafanyika kwa kushirikiana na Wizara na Taasisi za Serikali, Asasi za Kiraia, Wanazuoni na Wadau wa Maendeleo. 

Lengo kuu la Kampeni ni ni kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kwa wote kupitia huduma ya msaada wa kisheria nchini.

Katika kufikia lengo hilo, kampeni inaongeza uelewa wa kisheria na haki za binadamu kwa jamii hususan haki za wanawake na watoto; Inatoa  huduma ya  ushauri  wa kisheria na unasihi kwa waathirika na manusura wa ukatili wa kijinsia; kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu  elimu ya sheria,  masuala ya  haki na wajibu na misingi ya utawala bora.

Matokeo ya muda mrefu ya kampeni hii ni kuchangia katika kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wasiojiweza, hususan wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi. Vilevile, itachangia kuimarisha amani na utulivu, kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na  kuleta utengamano wa kisiasa hapa nchini.

Matokeo ya kati ni kuimarika kwa mfumo wa utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria katika ngazi za Serikali Kuu hadi Serikali za Mitaa.

Matokeo ya muda mfupi ni kuongezeka kwa idadi ya watu wanaotoa taarifa za matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto; kupungua kwa idadi ya migogoro na matukio yanayotokana na ukosefu wa uelewa wa sheria; Kuimarika kwa uwajibikaji na uwezo wa taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali zinazotoa huduma za msaada wa kisheria.

Kampeni imeanza kutekelezwa Jijini Dodoma tarehe 28 Mei, 2023 baada ya kuzinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) tarehe 27 Mei, 2023 Jijini Dodoma. Ratiba ya utekelezaji wa Kampeni hiyo kwa mwaka 2023 katika Mikoa imezingatia usawa wa Kikanda kama ifuatavyo:-

 

Kanda

Mkoa

Tarehe/Mwezi

Kati

Dodoma

Aprili, 2023

Kaskazini

Manyara

Mei, 2023

Ziwa

Shinyanga

Juni, 2023

Kusini

Ruvuma

Julai, 2023

Magharibi

Kigoma

Agosti, 2023

Mashariki

Morogoro

Septemba, 2023

Nyanda za Juu Kusini

Njombe

Oktoba, 2023

Nyanda za Juu Kusini 2

Rukwa

Novemba, 2023

Ziwa (Magharibi)

Kagera

Desemba, 2023

 

Maeneo yanayofikiwa

Kwa utaratibu wa sasa, ratiba inalenga kufikia Kata kumi (10) kwa kila Halmashauri na Mitaa/Vijiji vitatu (3) kwa kila Kata. Kuna maeneo ambapo idadi ya Vijiji/Mitaa inapungua kutokana na mazingira nje ya uwezo wa watoa huduma.

Vipaumbele vya Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2023/24

1. Kushughulikia Masaula ya Kikatiba.

Katika mwaka wa bajeti wa 2023/24 Wizara ya Katiba na Sheria imejipanga kutoa elimu ya Katiba na Sheria kwa umma kupitia Vyombo mbalimbali vya Habari vikiwemo redio, luninga, mitandao ya kijamii na tovuti za Wizara pamoja na kugawa Katiba kwa wananchi. Mkakati huu unalenga kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa Katiba na kuwajengea uwezo wa kufahamu   haki na wajibu wao kwa taifa na kuwawezesha kushiriki katika mijadala ya Katiba.

2. Kusimamia Mfumo wa Haki na Utoaji Haki.

Katika mwaka wa Bajeti 2023/24 Wizara ya Katiba na Sheria imejipanga kuendelea kusimamia mifumo ya haki na utoaji haki ili kuhakikisha inapunguza mlundikano wa mashauri mahakamani na kuhakikisha wananchi wote wanapata haki sawa na kwa wakati.

3. Kuratibu Masuala ya Haki za Binadamu na Utoaji wa Huduma ya Msaada wa Kisheria

Mwaka wa fedha 2023/24 Wizara ya Katiba na Sheria imejipanga kuendelea kuratibu masuala ya Haki za binadamu ikiwemo kushiriki vikao mbalimbali vinavyohusu masuala ya haki za binadamu. Pia Wizara imejipanga kuendelea kutoa msaada wa kisheria kupitia Kampeni ya Mama Samia Legal Aid Campaign ambayo imepangwa kufanyika mikoa yote nchini Tanzania Bara na Zanzibar.

4. Kutunga Sera zinazohusu Masuala ya Kisheria na Kusimamia Utekelezaji wake

Katika mwaka wa bajeti ya 2023/24 Wizara ya Katiba na Sheria imejipanga kutunga sera na sheria mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wa masauala ya sheria pamoja na Katiba ikiwa ni mkakati wa  kuimarisha  na  kuendeleza sekta ya sheria nchini.

5. Uandishi wa Sheria

Wizara ya Katiba na Sheria kupitia ofisi ya Mwanasheria Mkuu itaendelea  kuhakikisha kuwa sheria za nchi zinakwenda na wakati na zina akisi Sera na vipaumbele vya Serikali  katika Nyanja zote za kiuchumi, kisiasa, kijamii kiutamaduni, kimazingira pamoja na kiteknolojia.

6. Kuendesha Mashtaka ya Jinai. 

Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24 Wizara imejipanga kuendelea na kuendesha kesi mbalimbali za jinai kupitia ofisi ya  Taifa ya Mashtaka.

7. Kushughulikia Uendeshaji wa Mashauri ya Madai na Usuluhishi.

Katika Mwaka wa bajeti ya mwaka wa Fedha 2023/24 Wizara ya Katiba na Sheria kupitia Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imejipanga kuendesha mashauri mbalimbali ya kesi za madai pamoja na kesi zingine.

8. Usuluhishi wa Migoro ya Kibiashara, Sheria za Kimataifa na Mikataba.

Wizara ya Katiba na Sheria imejipanga kufanya mapitio ya Sheria mbalimbali za usuluhishi na kuandaa mapendekezo ya uboreshwaji wa Sheria hizo pamoja na kukusanya maoni ya kuhusu mapendekezo ya maboresho pamoja na kuandaa rasimu ya marekebisho ya sheria.

9. Kuratibu Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu, Usimamizi wa Ufilisi na Udhamini.

Wizara kupitia Wakala wa Usajili, Ufilishi na Udhamini - RITA itaendelea kuimarisha shughuli za usajili wa matukio muhimu ya binadamu, ufilisi na udhamini  kwa ajili ya mipango ya maendeleo ya Taifa.

Mpangilio