Tawala za Mikoa

Kishindo cha OR- TAMISEMI

  • Hadi Februari, 2022 vyumba vya madarasa 11,988 kati ya vyumba 12,000 vya Shule za Sekondari vimejengwa na kukamilika sawa na asilimia 99.99. Vilevile, vyumba vya madarasa 2,978 kati ya 3,000 vimejengwa na kukamilika katika Vituo shikizi sawa na asilimia 99.26.

 

  • Ofisi za walimu 3,184, matundu ya vyoo 557 yamejengwa, ajira zilizozalishwa 21,872 wakiwemo wanaume 17,354 na wanawake, 4,518, madawati 47,149 na seti ya meza na viti 451,918 vimetengenezwa.

 

  • Ofisi ya Rais - TAMISEMI imeomba kibali cha kuajiri walimu 10,000 wa Shule za Msingi na Sekondari. Kati ya hao, walimu 5,000 ni kwa ajili ya shule za Awali na Msingi na 5,000 kwa ajili ya Shule za Sekondari. Hii itapunguza mahitaji ya walimu wa Shule za Sekondari kwa asilimia 6.56 na elimu ya Awali na Msingi kwa asilimia 10.65. 

 

  • Wanafunzi 907,803 waliofaulu mtihani wa darasa Saba mwaka 2021 kupata nafasi ya kuanza Kidato cha Kwanza Januari, 2022 bila kuwa na chaguo la pili.

 

  • Kupitia Programu ya Uboreshaji wa Elimu katika Shule za Sekondari (Secondary Education Quality Improvement Program-SEQUIP) jumla ya Shilingi bilioni 30 zimepokelewa ambapo kila Shule imepokea Shilingi bilioni 3.00 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Shule za Sekondari za masomo ya sayansi kwa Wasichana

Mwongozo wa Utoaji wa Vibali vya Ujenzi na Usimamizi wa Ukaguzi wa Ujenzi wa Majengo

Ongezeko la kasi ya ujenzi ni moja ya sababu za Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwa na uwezo mdogo wa kupanga, kusimamia na kudhibiti uendelezaji na hivyo kufanya usimamizi wa ukaguzi wa ujenzi wa majengo uwe dhaifu na majengo kuwa na viwango hafifu na kukosa usalama. Ukaguzi wa ujenzi wa majengo haufanyiki inavyotakiwa hivyo, kuathiri ubora wa majengo.

Waendelezaji wengi hawatumii ipasavyo ushauri wa kitaalamu na baadhi ya Makampuni yasiyozingatia maadili ya kitaaluma huonyesha majina na ushiriki wao kwenye mabango yenye taarifa za Ujenzi. Wapo pia, wataalam wanao saini kwenye vitabu vya ukaguzi (Inspection books) bila ya kukagua jengo husika kama inavyotakiwa.

Mwendelezaji anao mchango mkubwa katika kufikia ubora wa jengo uliokusudiwa. Vile vile, ni wajibu wake kuzingatia maelekezo yote yaliyomo kwenye Kibali cha Ujenzi kilichotolewa. Iwapo atamwaajiri mtaalamu mshauri na mkandarasi mahiri na mwaminifu,itarahisisha kazi ya ukaguzi. Kumekuwepo na udhaifu kwenye usimamizi unaosababishwa na waendelezaji kuajiri wataalamu washauri wasio na sifa na baadhi yao kutotembelea maeneo ya Ujenzi kufanya ukaguzi.

Hivyo, Ofisi ya Rais –TAMISEMI iliandaa Mwongozo utakaotumika wakati wa kutoa Vibali vya Ujenzi na Usimamizi wa Ukaguzi wa Ujenzi wa Majengo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa. Mwongozo huu umeandaliwa ili kuondoa changamoto zilizopo kwenye utaratibu wa utoaji wa Vibali vya Ujenzi na usimamizi wa Ujenzi wa majengo.

Kwa mujibu wa Vifungu 124 na 125 vya Kanuni za Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) (Udhibiti Uendelezaji), Sura 288 (GN 242 ya mwaka 2008), Ujenzi wowote ndani ya Mamlaka za Upangaji ambazo ni Mamlaka za Miji Midogo, Halmashauri za Miji, Manispaa na Ma-jiji ni lazima upate kibali cha Ujenzi kutoka kwenye Mamlaka husika.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 35 (i) cha Sheria ya Mipangomiji Na. 8 ya mwaka 2007, Mamlaka ya Upangaji inatakiwa kutoa kibali cha Ujenzi katika kipindi kisichozidi siku 60 kuanzia tarehe mwombaji alipowasilisha maombi yake. Aidha, ndani ya muda huo mamlaka inatakiwa kumjulisha mwombaji kuwa amekubaliwa au amekataliwa ombi lake na kutaja sababu zilizopelekea ombi lake kukataliwa.

Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Kifungu 122(4) imezipa majukumu Mamlaka za Wilaya ya kutoa au kubadilisha majina, namba za barabara, mitaa na nyumba kama ilivyobainishwa kwenye Mwongozo wa Anwani za Makazi na Postikodi wa Agosti 2016. Kufanya hivyo, kutadhibiti uendelezaji holela wa Vijiji na Miji Midogo inayochipukia.

Mwongozo huu ukifuatwa kikamilifu, kwa kigezo cha kiashiria cha utoaji wa Vibali vya Ujenzi, utaboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa. Mamlaka hizo zinatakiwa kutoa Vibali vya Ujenzi ndani ya kipindi cha kati ya siku saba na mwezi mmoja. Pia, mwongozo utaboresha usimamizi wa ukaguzi wa Ujenzi wa majengo.Mwongozo wa Utoaji Vibali vya Ujenzi

Kwanini Anwani za Makazi?

Majukumu ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ni pamoja na kupanga, kupima, kugawa, kumilikisha na kusimamia uendelezaji wa makazi katika maeneo ya utawala. Utaratibu huu unahitaji ufanisi katika usimamizi na udhibiti wa uendelezaji wa makazi na matumizi mengine. Utaratibu uliopo ni wa kutoa vibali vya kuendeleza maeneo yote yaliyopimwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa baada ya kuzingatia masuala muhimu ya uendelezaji kama vile umiliki, matumizi ya Ardhi, upimaji na masharti mengine ya uendelezaji.

Hata hivyo, kutokana na kasi kubwa ya ongezeko la watu na mahitaji makubwa ya makazi, Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeshindwa kukidhi matakwa ya kupima maeneo ya kutosha ambayo wananchi wanaweza kuendeleza makazi yao kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo. Hali hii imefanya majengo mengi kujengwa bila vibali vya ujenzi na mengine kuendelezwa kwenye maeneo yasiyopimwa hivyo kuleta changamoto ya uundaji wa anwani za makazi. Itazingatiwa kuwa utaratibu wa anwani za makazi ulikuwepo siku za nyuma hususani miongo miwili baada ya uhuru na kufifia baadae kutokana na mabadiliko mbalimbali ya kiutawala na kisiasa.

Kutokuwepo kwa majina ya barabara, njia na nambari za nyumba ikichangiwa na ukuaji wa maeneo ya mijini, inaleta tatizo kwa sababu huduma nyingi za miji zinaathiriwa zikiwa ni pamoja na huduma za kijamii, kiuchumi na miundombinu. Ili kuondokana na matatizo yaliyoelezwa hapo juu, Wizara zenye dhamana na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa pande zote za Muungano, zilipewa jukumu la kutoa Mwongozo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini ili ziweze kutoa anwani za makazi kwa wananchi wote.Mwongozo wa Anwani za Makazi 

Mpangilio
Marekebisho ya Lugha
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi