Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa tarehe 26 Aprili, 1964. Baada ya Muungano, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheikh Abeid Aman Karume akawa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Rashidi Mfaume Kawawa alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Tanzania na Kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni.
Mwaka 1992, Tanzania ilipitisha Mfumo wa Demokrasia ya Vyama Vingi ambao ulihitaji marekebisho makubwa ya Katiba. Marekebisho haya yalihusu suala la Makamu wa Rais na kuanzishwa mfumo wa mgombea mwenza uliowashirikisha mgombea Urais na Makamu wa Rais. Hii ilimaanisha kwamba, Rais wa Zanzibar aliacha kuwa Makamu wa Rais wa Muungano moja kwa moja lakini akawa Mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Muungano.
Bonyeza chini kusoma Kitabu cha Historia ya Muungano
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umekuwepo kutokana na sababu mbalimbali kama vile kuwepo kwa mahusiano ya karibu na ya kihistoria baina ya Tanganyika na Zanzibar katika nyanja mbalimbali kama vile udugu wa damu, biashara, utamaduni, lugha na mahusiano ya karibu kisiasa hususan baina ya vyama vya TANU na ASP.
Pia, adhma ya kuwa na Muungano wa Afrika hususan kwa kuanzia na Shirikisho la Afrika Mashariki. Hata kabla ya uhuru wa Tanganyika, Mwalimu Nyerere pamoja na viongozi wengine waliokuwa wakipigania uhuru katika ukanda wa Afrika walikuwa na matarajio ya kuwa na Muungano wa Afrika. Mwalimu Nyerere binafsi alipendelea uwepo Muungano wa Afrika kwa kuanzia na Mashirikisho ya kikanda.
Kimsingi zipo sababu mbalimbali zilizosababisha Muungano huu kama vile historia za nchi hizi mbili, ukaribu wa nchi hizi mbili, muingiliano wa kijamii, ushirikiano wa kibiashara, ushirikiano madhubuti na wa muda mrefu wa kisiasa baina ya TANU na ASP, ushirikiano na urafiki wa muda mrefu kati ya watu, viongozi, na wakati wa harakati za utaifa uliopelekea uhuru wa nchi hizo mbili.
Msingi wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ni Hati za Muungano za mwaka 1964. Hati za Muungano zilitiwa saini na waasisi wa Muungano tarehe 22 Aprili, 1964, na kupelekea Tanganyika na Zanzibar kuwa dola moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Baada ya Muungano, Mwalimu J. K. Nyerere alikuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya ya Muungano wa Tanzania na Sheikh Abeid Amani Karume, alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aprili 26, 1964 Bunge la Tanganyika lilipitisha Sheria za Muungano.Halikadhalika, Sheria hizi zilithibitishwa na Baraza la Mapinduzi Zanzibar. Sheria hizi za Muungano zilithibitisha Hati za Muungano, zilitaja Rais na Makamu wa Rais, zilitaja Muundo wa Muungano na Katiba ya Muungano.
Aidha, Aprili 27, 1964, waasisi wa Muungano walibadilishana Hati za Muungano na wajumbe saba wa Baraza la Mapinduzi waliapishwa kuwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ni Sheikh Abeid Amani Karume, Kassim Abdala Hanga, Abdulrahaman Mohamed Babu, Hassan Nassor Moyo, Sheikh Aboud Jumbe, Hasnu Makame na Sheikh Idris Abdul Wakil. Baada ya kuapishwa kuwa Wabunge wakateuliwa kuwa Mawaziri wa Serikali ya Muungano.
Hoja zilizopatiwa ufumbuzi katika kikao hicho ni kama ifuatavyo;
Hoja nne za Muungano zinazoendelea kutafutiwa ufumbuzi