Afya

Usichukulie Poa Nyumba ni Choo

Wizara inaratibu na kusimamia utekelezaji wa awamu ya pili ya Kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira yenye kaulimbiu isemayo “USICHUKULIE POA NYUMBA NI CHOO” yenye lengo la kuhimiza ujenzi na matumizi ya vyoo bora na vifaa vya kunawia mikono vyenye maji tiririka na sabuni katika ngazi ya kaya na Taasisi.


Kupitia kampeni hii, idadi ya kaya zenye vyoo bora imeongezeka kutoka asilimia 64 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 72 mwezi Machi, 2022. Vilevile, kaya zenye vifaa vya kunawia mikono vyenye maji tiririka na sabuni zimeongezeka kutoka asilimia 40 Mwaka 2020 kufikia asilimia 41 mwezi Machi, 2022. Watanzania wanaendelea kuhimizwa kuzingatia kanuni za usafi binafsi na usafi wa mazingira ili kujikinga na magonjwa mbalimbali kwani Kinga ni Bora kuliko Tiba.

Mama Kinara

Kitendea kazi cha “Mama Kinara” kimetengenezwa na jumla ya Mama Kinara 818 na Wakufunzi 40 walipata mafunzo yaliyofanyika katika mikoa ya Morogoro, Pwani, Tanga, Dodoma, Manyara, Arusha, Mwanza, Shinyanga, Geita na Tabora. Hadi sasa jumla ya akinamama 68,028 wanaonyonyesha walio na VVU wamefikiwa kati ya akinamama 73,935. Lengo la hatua hii ni kuhakikisha wanawake wenye maambukizi ya VVU/UKIMWI wananyonyesha Watoto wao ili kuweza kuwafanya wawe na afya bora.

Wizara imeanzisha afua mpya ya Mama Kinara katika ngazi ya Jamii kwa ajili ya kuwezesha ufuatiliaji wa wajawazito na akina mama wanaonyonyesha ambao wamekwisha thibitika kuwa na maambukizi ya VVU.

Wizara inaboresha afua mbalimbali ambazo zinahamasisha wananchi kwenda kupima na kutambua hali zao za maambukizi ya VVU/UKIMWI, ili waweze kupatiwa huduma za ushauri, upimaji, matunzo na huduma za dawa kwa haraka pale inapoonekana kuwa wameambukizwa. Jumla ya wateja 1,519,013 sawa na asilimia 84.6 ya watu 1,795,905 wanaokadiriwa kuishi na virusi vya UKIMWI nchini walikuwa wanatambua hali zao za maambukizi.

Kati yao, wateja 1,507,686 sawa na asilimia 99.3 walikuwa wameanza kutumia dawa za kufubaza Virusi vya UKIMWI (95 ya pili). Aidha, asilimia 95.8 ya wateja waliokuwa wanatumia dawa za ARV nchini walikuwa wamefubaza wingi wa virusi vya UKIMWI ambayo ni sawa na chini ya nakala 1,000 (95 ya tatu). Idadi ya vituo vinavyotoa huduma ya Tiba ya UKIMWI (CTC) vimefikia 6,759 na kati ya hivyo CTC kamili ni 3,075 na vituo vya huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto (RCHS) vinavyotoa huduma ya kutoa dawa ya kufubaza Virusi vya UKIMWI vipo 3,684. 

Aidha, Wizara ilisaini mwongozo wa utekelezaji wa utoaji dawa kinga na kuanza kwa huduma hiyo, jumla ya walengwa 13,285 walianza huduma hiyo katika Mikoa yote nchini. Huduma ya Kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) zinatolewa katika vituo 6,996 sawa na asilimia 98 kati ya vituo 7,138 vinavyotoa huduma za afya ya uzazi na Mtoto. 

Pia, Wizara imepanua huduma ya upimaji wa pamoja wa VVU na kaswende kwa wajawazito ambapo jumla ya vituo 3,497 kati ya 7,138 sawa na asilimia 49 vinavyotoa huduma za afya ya uzazi na mtoto vimeanza kupima VVU na kaswende kwa kutumia kitepe kimoja, lengo ni vituo vyote viweze kutoa huduma ya upimaji huo.

Wizara imeendelea kupanua huduma za upimaji wa Watoto wachanga waliozaliwa na akina mama wenye VVU kutoka Idadi ya vituo vinavyotoa huduma hizi kutoka vituo 50 mwaka 2020 hadi vituo 141 mwaka 2021. Upimaji huo hufanyika kwa kutumia vinasaba vya VVU mahali zitolewapo huduma (EID Point of Care). Jumla ya watoto 54,134 waliozaliwa na akina mama wanaoishi na VVU walipimwa vinasaba vya VVU na kati yao watoto 1,299 sawa na asilimia 2 walikutwa na maambukizi ya VVU na wote waliunganishwa na huduma ya matibabu lengo ni kuzuia kabisa maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto.

 

 

Lishe bora ni muhimu kwa uhai

Lishe bora ni muhimu kwa uhai, ukuaji na maendeleo ya binadamu kiakili na kimwili na hivyo kuchangia katika kuongeza tija katika uzalishaji mali kwa kaya na kuimarisha uchumi wa jamii na Taifa kwa ujumla.

Wizara imefanya utafiti wa hali ya lishe kwa wanafunzi wa shule za msingi za Serikali nchi nzima, ambapo jumla ya wanafunzi 63,000  kutoka shule 650 wamefanyiwa tathmini ya hali ya lishe na kudodoswa masuala ya ulaji na wanafunzi 21,000 wamepimwa kiasi cha damu. Utafiti huu umefanyika mwezi Agosti na Oktoba, 2021,uchakataji wa takwimu unaendelea. Matokeo ya utafiti huu yatachangia katika kuboresha hali ya lishe kwa vijana hususani walioko mashuleni. 

Aidha, Serikali imeendelea kuimarisha lishe na afya ya watoto wachanga na wadogo kwa kuendelea kutekeleza Kampeni ya Kitaifa ya utoaji wa matone ya Vitamini A kwa watoto walio chini ya miaka mitano.  Malengo ya kampeni ya mwaka 2021/22 yalikuwa ni kutoa matone ya Vitamin A kwa watoto 8,248,450, kati ya umri wa miezi (6 – 59). 


Zoezi hili lilikamilika kwa kuweza kuwafikia walengwa 8,015,463 sawa na asilimia 97.2 ikilinganishwa na asilimia 95 ya mwaka 2020. Vilevile, Wizara imeendelea kuimarisha huduma za matibabu ya utapiamlo mkali kwa watoto kwa kuimarisha upatikanaji wa chakula dawa, upatikanaji wa vifaa vya kufanyia tathmini ya hali ya lishe pamoja na kuboresha miundombinu ya kufanyia matibabu ya utapiamlo mkali kwa watoto.

Pia vituo vinavyotoa matibabu ya utapiamlo mkali kwa kulaza vimeongezeka kutoka vituo 365 mwaka 2020 kufikia vituo 385 vya kutolea huduma za afya hadi kufikia Machi, 2022. 

Wizara kwa kushirikiana na wadau wa lishe nchini imefanya maadhimisho ya Siku ya Lishe Kitaifa tarehe 18 – 23 Oktoba, 2021.Uzinduzi na Kilele cha Maadhimisho hayo umefanyika Mkoani Tabora. Aidha, Wizara ilifanya uraghibishi na mafunzo kwa timu za uendeshaji wa huduma za afya za Mikoa na Halmashauri (RHMT na CHMT) pamoja na watoa huduma za Afya kuhusu uanzishwaji wa vitengo vya kuratibu huduma za Lishe kwenye Vituo vya kutolea huduma za Afya katika Mikoa ya Tabora,Manyara na Dodoma, ambapo jumla ya watoa huduma 150 wamejengewa uwezo.

Mpangilio
Marekebisho ya Lugha
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi