Vijana na Ajira

Muhtasari

Serikali ya Tanzania imetengeneza mfumo unaowezesha kurahisisha michakato ya ajira ambayo ilikuwa ikishughulikiwa kwa mikono iliyokua inaweze kupelekea kutokea kwa makosa mbalimbali. Mfumo huu ni dirisha moja la kutafuta kazi na maombi ya nafasi za kazi mbalimbali Serikalini

Kikototoo kipya kuweka Uwiano na Usawa wa Mafao

Kikokotoo kipya kinachotarajiwa kuanza tarehe 1 Julai mwaka 2022, faida yake kubwa ni kuweka Uwiano na Usawa wa Mafao baina ya Wastaafu, ambapo watumishi wote wa sekta Binafsi na Umma watalipwa mafao ya mkupuo wa asilimia 33.

Athari zilizokuwa zinajitokeza kwa kikokototoo cha zamani cha mkupuo wa asilimia 50, ni kukosekana kwa uwiano na usawa wa mafao kwa maana kwamba mchangiaji katika mfuko ambaye amechangia kwa miezi 467 na michango yake kwa muda wa utumishi wake wote ni shilingi mil. 36, kanuni ya zamani alikuwa analipwa sh. milioni 129, yaani kachangia shilingi milioni 36 lakini anapata mafao ya mkupuo shilingi milioni 129 na kwa Wafanyakazi wengine ambao wamechangia shilingi milioni 86 na kufanya kazi kwa miezi 350 kwa kutumia mkupuo wa asilimia 25, anapata mafao ya mkupuo ya shilingi milioni 54. Huyu amechangia milioni 36 analipwa milioni 129, huyu amechangia milioni 86 analipwa milioni 54

Kikokotoo kipya kinaweka wafanyakazi wote wa Tanzania wa sekta ya binafsi na Umma, ambao wanasimamiwa na sheria za kazi na ajira zinazofanana kutumia viwango sawa vya ukokotozi wa mafao. Kikokotoo kipya kitaondoa utofauti kwa wastaafu ambapo baadhi walikuwa wanalipwa mkupuo wa asilimia 25 wakati wengine walikuwa wanalipwa mkupuo wa asilimia 50. Kikokotoo hiki kinasaidia kwa sasa mifuko ya pensheni inazungumza lugha moja.

Kutokana na malalamiko ya watumishi na wadau kuhusu Kanuni za mwaka 2018 ambapo watumishi wote walikuwa wanalipwa mafao ya mkupuo kwa asilimia 25. Serikali ili sitisha kanuni hizo na kuagiza kamati maalum iliyowahusisha wadau wote ambao ni serikali, Waajiri na Waajiriwa. Lengo ilikuwa kuchambua hali ya uhimilivu na uendelevu wa mifuko. Aidha, makubaliano yaliyofikiwa ndiyo yaliyofikiwa katika kamati maalumu ndiyo yatakayotekelezwa katika mwaka mpya wa fedha 2022/2023.

Kikokotoo kipya kitawasaidia watumishi kwa kuwa aliyechangia milioni 86 na mafao yake ya mkupuo yatapanda kuwa shilingi milioni 71 na ataendelea kulipwa pensheni ya kila mwezi shilingi mil. 1,840,000 mpaka Mwenyezi Mungu atakapomwita.

Mchango wa Sekta Binafsi katika Ukuaji wa Ajira na Uchumi wa Nchi.

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan inathamini na kutambua mchango mkubwa unaotolewa na Sekta Binafsi katika ukuaji wa ajira na uchumi nchini.

Sekta Binafsi ni msingi wa ukuaji wa ajira, na ni injini ya uchumi wa nchi. Sekta binafsi inatoa mchango mkubwa katika uzalishaji wa bidhaa na uwekezaji katika sekta za kimkamakati. Wizara itaendelea kushirikiana na Wadau wa Utatu (Serikali, Wafanyakazi na Waajiri) hususani katika kuboresha mahusiano mahali pa kazi na kulinda Sekta Binafsi kama mdau muhimu wa uchumi nchini.

Serikali itaendelea kushirikiana na Waajiri wote hususani wa Sekta Binafsi katika kuibua fursa za maendeleo, kujadili changamoto zao na kuzipatia ufumbuzi kwa haraka. Serikali ina imani kubwa na ATE na Waajiri wote katika kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini.

Masuala mbayo serikali inaendelea kushirikiana na wadau wa utatu ni pamoja na mapitio ya Kanuni za Mafao kwa Wastaafu kwa watumishi wote wa Sekta ya Umma na Binafsi. Pia, inaendelea kupanga kima cha chini cha mshahara katika sekta binafsi kwa kushirikiana na wadau.

Katika Mwaka wa Fedha 2021/2022 Serikali ilipunguza mchango wa Waajiri katika Sekta Binafsi kwenye Mfuko wa Fidia ya Wafanyakazi kutoka asilimia 1% Hadi asilimia 0.6%. Kuanzia Septemba 2021 Serikali ilipunguza adhabu ya kuchelewesha michango kwa mfuko wa fidia kwa Wafanyakazi kutoka 10% iliyokuwa ikitozwa kwa kila mwezi na kuwa 2.0% kwa mwezi. Waajiri wote waliokuwa wamechelewa kulipa michango yao kwa kipindi cha kuanzia tarehe 01 Oktoba, 2017 hadi tarehe 31 Agosti 2021 walisamehewa riba baada ya kulipa michango yao.

 

Tupinge Utumikishwaji wa Kazi kwa Watoto.

Serikali imetaka ushirikiano na wadau wa kupinga utumikishwaji wa kazi kwa watoto ili kufanikiwa kukomesha utumikishwaji huo hapa nchini.

Wadau ambao hawanabudi kutoa ushirikiano madhubuti kwa Serikali ni pamoja na Mashirika ya Kimataifa, Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Vyama vya Wafanyakazi, Vyama vya Waajri, Asasi za Kidini na za Kiraia pamoja na wananchi. Kila mdau anaowajibu wakuhakikisha haki za msingi za watoto zinalindwa kwa kutimiza wajibu wake.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Mtoto ametafsiriwa kuwa ni mtu yeyote mwenye Umri wa chini ya miaka 18.Katika kutokomeza Utumikishwaji wa Watoto katika kazi hatarishi lazima kuzingatia matakwa ya Mikataba ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) na mapendekezo yake kupitia Sheria za Kazi za nchini. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Serikali (Integrated Labour Force Survey) wa mwaka 2014, umeonesha, 29% ya watoto wenye umri kati ya miaka 5- 17 sawa na watoto millioni 4.2, wavulana wakiwa ni 29.3% na wasichana 28.4% wako katika utumikishwaji .

Utafiti huo umebainisha kuwa, watoto wengi wapo katika sekta za kiuchumi ikiwa ni pamoja na mashambani, majumbani, migodini, na biashara ndogondogo. Kwa mujibu wa utafiti huo, sababu kuu zinazo chochea matukio ya utumikishwaji ni Umasikini, Vifo vya Wazazi na Walezi, Mifarakano katika Familia, Mila na Desturi zisizofaa pamoja na Nguvu Kazi Rahisi (Cheap Labour).

Pia, unabainisha madhara ya moja kwa moja yanayosababishwa na utumikishaji wa watoto ni Kuwa na Taifa la Watu Wasiojua Kusoma na Kuandika pamoja na Kuenea kwa Magonjwa kama vile UKIMWI.

 

Mpango Maalum wa Kutathmini Mazingira ya Kazi katika Ofisi za Serikali

Mpango maalumu wa kutathmini Mazingira ya Kazi katika Ofisi za Serikali ni mwendelezo wa mkakati wa Taasisi yake wa kufanya tathmini ya mazingira ya kazi nchini kisekta. Mpango huu utakaofanyika sambamba na upimaji wa afya za wafanyakazi wote pamoja na kuwapa mafunzo stahiki ya usalama na afya mahali pa kazi utahusisha mambo mbali mbali ikiwemo; Ukaguzi wa Mifumo ya Usalama katika Ofisi za Wizara mbali mbali ikiwemo miradi ya ujenzi katika Mji wa Serikali-Mtumba, Uchunguzi wa afya za wafanyakazi, Mafunzo ya Huduma ya Kwanza mahali pa kazi pamoja na mafunzo kwa Wawakilishi wa Kamati za Usalama na Afya mahali pa kazi yatakayoambatana na uundaji wa Kamati husika.

Kimsingi OSHA ina wajibu wa kulinda nguvukazi kupitia kusimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake. Kwa mujibu wa Sheria tajwa, OSHA inapaswa kuhakikisha kwamba inayatambua maeneo yote ya kazi nchini kwa kuyapatia usajili na kisha kuyafikia kwa ajili ya kufanya tathmini ya hali ya mazingira ya kazi, kutoa mafunzo stahiki kwa wafanyakazi pamoja na kuchunguza afya za wafanyakazi kutegemeana na shughuli wanazozifanya.

Mpango huo utasaidia katika kuboresha mazingira ya kazi na kuwasaidia watumishi kufanya kazi kwa kuzingatia tahadhari muhimu dhidi ya vihatarishi mbali mbali. Aidha, kupitia mpango huu ambao utahusisha tathmini ya kina ya mazingira ya kazi, itakuwa ni fursa muhimu kwa mwajiri kuboresha mazingira ya kazi kutokana na mapendekezo yatakayotolewa na wataalam wa OSHA.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri Prof. Ndalichako katika uzinduzi, mpango huo utatekelezwa kwa mwezi mmoja ambapo mazingira ya kazi katika Wizara zote yatafanyiwa ukaguzi na wataalam wa OSHA. Aidha, baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, yatatolewa mapendekezo ya kitaalam ambayo yatatumika na serikali katika kuboresha mazingira ya kazi.

OSHA ni Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu yenye jukumu ya kulinda nguvukazi ya nchi kupitia kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 ambapo hufanya utambuzi wa maeneo ya kazi na kuyafikia kwa ajili ya ukaguzi, mafunzo ya usalama na afya pamoja na uchunguzi wa afya za wafanyakazi.

Mpangilio