Hivi karibuni Serikali imezindua mwongozo wa utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo nchini, wenye lengo la kuhakikisha sekta binafsi na umma zinajua haki na wajibu katika zoezi zima la utoaji wa chanjo na kuhakikisha afya ya mnyama inabaki salama.
Ili kuhakikisha mwongozo wa utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo nchini, unakuwa na tija kwa taifa ni lazima kuwepo kwa haki na wajibu kwa wadau wote wa mifugo kuelewa vyema haki na wajibu huo katika katika kuboresha afya ya mifugo.
Mwongozo huo umeshirikisha wadau zaidi ya thelathini wakati wa kuundaa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ipo tayari kupokea maoni ya wadau sehemu ambazo mwongozo utaonekana kuwa na mapungufu ili kuurekebisha na kuufanya uwe bora zaidi. Lengo likiwa ni kuhakikisha afya ya mifugo nchini inalindwa na mfugaji kutopata hasara ya mifugo yake kufa au kupata madhara mengine yoyote baada ya kuchanjwa.
Serikali ilisimamisha kwa muda, utoaji wa chanjo unaofanywa na halmashauri nchini kupitia kampuni walizoingia nazo mikataba, baada ya kubaini chanjo kutolewa kiholela kwa mifugo bila kuwepo utaratibu sahihi na kusababisha madhara kwa mifugo na hasara kwa mfugaji.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi, mamlaka za serikali za mitaa, watoa huduma za afya ya mifugo na sekretarieti za mikoa wanatakiwa kuzingatia maelekezo yaliyopo kwenye mwongozo wa utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo nchini na kutoa maoni au kuuliza maswali sehemu ambazo zitakuwa na utata ili kuhakikisha mwongozo huo unatekelezwa kama ambavyo umezingatiwa kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya mifugo nchini.
Serikali bado inahakikisha inafanya jitihada mbalimbali za kupata masoko zaidi ya mazao ya mifugo yenye ubora ambayo yanachochewa na uwepo wa chanjo bora na mifugo kupatiwa chanjo hiyo kwa njia sahihi.
Ziwa Tanganyika huchangia takribani asilimia 19 ya samaki wote wanaozalishwa nchini ambapo kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2021 ziwa hilo lilizalisha tani 90,743 zenye thamani ya shilingi bilioni 592.5. Uvuaji wa samaki wachanga katika ziwa hilo kwa upande wa Tanzania unasababisha upotevu wa zaidi ya dola 690,000 za Marekani kila mwaka huku nchi ya Zambia ikipoteza zaidi ya dola 1,000,000 za Marekani kutokana na kitendo hicho.
Kwa kutambua hivyo, Serikali imezindua kampeni ya kitaifa ya Uelewa kuhusu Mkataba wa kikanda wa Usimamizi wa Uvuvi Endelevu wa ziwa Tanganyika iliyosheheni mikakati mbalimbali ya Ulinzi wa rasilimali za Uvuvi za ziwa Tanganyika. Kampeni hiyo ni miongoni mwa hatua za utekelezaji wa mkataba unaojumuisha nchi zote zinazonufaika na Uvuvi wa Ziwa Tanganyika ambazo ni Tanzania, Burundi, Zambia na Jamhuri ya demokrasia ya Kongo.
Miongoni mwa changamoto ambazo zilikuwa zikiikabili sekta ya Uvuvi kwenye mikoa inayopitiwa na ziwa Tanganyika ni utoroshwaji wa rasilimali za uvuvi kwenda nje ya nchi kupitia maeneo ya mipakani na baadhi ya wavuvi kuvamiwa na kuporwa mali zao hivyo mkataba huo utaondoa changamoto hizo.
Mkataba huu ni mwongozo wa pamoja baina ya nchi hizi zinazohusika na Ziwa Tanganyika na utasaidia kuweka uelewa wa pamoja kwenye utekelezaji wa kanuni na taratibu zinazopaswa kufuatwa kwa wavuvi waliopo kwenye nchi husika.
Wizara imeagiza watalaam wote wa Sekta ya Uvuvi waliopatiwa semina elekezi kuhusu mkataba huo kuhakikisha wanafikisha elimu kwa wavuvi ambao ndio walengwa wa mkataba huo ili wawe na uelewe kabla ya kuanza kuutekeleza.
Uzinduzi wa kampeni hiyo hapa nchini umefanyika mara baada ya nchi za Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Zambia na Burundi kufanya hivyo kwa lengo la kuunganisha nguvu ya pamoja katika ulinzi wa rasilimali za Uvuvi wa Ziwa Tanganyika na kuufanya uvuvi huo kuwa endelevu.
.
Sekta ya Mifugo
Sekta ya Uvuvi