Utamaduni, Sanaa na Michezo

Tuenzi Utamaduni Wetu

Safari Kubwa ya Mageuzi ya Kuimarisha Utamaduni Yapamba Moto hii ikiwa ni baada ya kuanzisha Tamasha kubwa la Kitaifa la Utamaduni. Tamasha hili linaleta mwamko mpya wa kiutamaduni ambao unajenga umoja kwa kuwaleta Watanzania pamoja kwa wakati mmoja.

Safari kubwa ya mageuzi ya kuimarisha utamaduni imepamba moto nchini na kuwa darasa kwa vijana wanaokua. Tamasha hili limewezesha wananchi wote kukutana nchi nzima na kuwa wa moja. Wasiojua utamaduni wao watanapata fursa ya kujifunza, ikiwa ni ukurasa mpya kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo. Serikali itaendelea kuthamini, kulinda na kuendeleza utamaduni wa mtanzania wakati wote. Huu ni mwanzo mzuri wa safari kubwa ya kuimarisha utamaduni kwa kuwa matamasha yatainua na kuibua hazina kubwa ya kiutamaduni miongoni mwa jamii nchi nzima na yana tija kwa kuleta taifa.

Tamasha la Kitaifa la Utamaduni ni Tamasha lililozinduliwa kwa mara ya kwanza na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa na kukutanisha mikoa yote nchini. Katika Tamasha hili shughuli mbalimbali za utamaduni hufanyika ikiwemo ngoma na maonesho ya vyakula na historia mbalimbali za makabila ya Tanzania.

Tamasha hilo ni maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa mkoani Mwanza mwaka 2021 wakati wa kuvikwa uchifu Hangaya.Kimsingi tamasha hili limejumuisha vitu vikubwa vitatu, shughuli za utamaduni ambazo ni maonesho ya ngoma na vyakula vya asili, matembezi ya kiutamaduni, usiku wa taarabu na maadhimisho ya siku ya Kiswahili.

Vitu hivyo vyote vitatu vikubwa kwa pamoja ni ubunifu ambao umefanya wananchi kufurahia kuona tamaduni zao kwa wakati mmoja katika matukio ya kijamii. Matukio haya yamefungua historia mpya ya nchi yetu ya kuyatumia ili kutangaza nchi yetu. Hakika huu ni mwanzo mzuri wa kutumia utamaduni katika kuitangaza nchi yetu.

Utamaduni ni Hazina ya Nchi

Serikali inaendelea kushirikiana na kufanya kazi na makabila yote nchini ili kuendeleza mila njema kwa vizazi vijavyo.  Utamaduni ni hazina ambayo kila kabila na taifa wanapaswa kuulinda na kuendeleza kwa kizazi hadi vizazi vijavyo. Utamaduni  ni tunu kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo hivyo machifu hawana budi kusimamia mila na desturi njema kwa watoto.

Serikali inathamini Utamaduni wa taifa letu kwa kuzingatia kauli ya Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema “Utamaduni ni kiini ama roho ya taifa lolote, taifa lisilo na utamaduni ni sawa na mkusanyiko wa watu usio na roho".Kila mmoja wetu anawajibu wa kulinda Utamaduni, kuendeleza na kuuhifadhi ndiyo maana tunasema “Utamaduni wetu; Fahari yetu;"

Aidha, Kila mtu kwenye eneo lake atumie mazingira yake vizuri kwa kupanda miti ya asili ikiwemo ya matunda ili kuimarisha afya  kwa kula vyakula vya asili. Ipo miti pesa ambayo inamanufaa kiuchumi ikiwemo mikarafuu ambayo inakua na kuanza kuvunwa baada ya mika mitano na kudumu hadi miaka 100 pamoja na amdalasini ambayo hupandwa na kuanza kuvuna baada ya miaka mitatu hatua ambayo itapata pesa zaidi ya kiasi anachopata sasa ili kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Kiswahili, Lugha yangu

Kiswahili ni miongoni mwa lugha za kiafrika zenye wazungumzaji wengi barani hapo ambapo takribani watu milioni mia moja wanakitumia Kiswahili pamoja na wazungumzaji kutoka nje ya Bara la Afrika.

Muasisi wa taifa la Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipigania kuingiza lugha ya Kiswahili kutumika kama lugha ya taifa kupitia Chama cha Siasa cha TANU mwaka 1954 na Rais wa awamu ya Tano hayati John Pombe Magufuli alipigania Kiswahili iwe lugha ya kimataifa na sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa msitari wa mbele kukibidhaisha Kiswahili duniani.

Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) linahitaji kuboresha miundombinu ya mitandao kwa ajili ya kazi mbalimbali za kukuza, kueneza na kuhifadhi Kiswahili ikiwemo kubidhaisha kiswahili, pia kuandaa kanzidata inayoainisha wataalam waliopo, kiwango chao cha elimu ili kuona wakihitajika wanapatikana wapi.

Kiswahili kilichaguliwa kuwa lugha ya kazi katika Umoja wa Mataifa mara baada ya Serikali kuwasilisha ombi hilo la lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha za kazi katika mikutano ya Umoja wa Afrika. Kutokana na umuhimu wa lugha ya Kiswahili  tayari inatumika katika jumuiya mbalimbali ikiwemo jumuiya ya Afrika Mashariki,Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na kufundishwa kwa lugha hiyo katika nchi nyingi za Afrika shuleni. Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni limetangaza tarehe saba Julai ya kila mwaka kuwa siku ya maadhimisho ya lugha Kiswahili Duniani.

Michezo ni Soko la Ajira

Tanzania ina wachezaji 54 wa kulipwa nje ya nchi wengi wao wamepitia michezo  ya UMISSETA na UMITASHUMTA, na sasa wamepata ajira, na kuliletea heshima kubwa taifa. Mashindano haya yameleta mafanikio makubwa kiuchumi na kijamii kwa wanachi.

Mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi na Sekondari  (UMITASHUMTA) na Sekondari (UMISSETA) ni mashindano ya michezo yanajumuisha mikoa yote kutoka Tanzania Bara na Visiwani ambapo michezo mbalimbali hushindanishwa ili kuleta uhai katika timu za Taifa ambao unatokana na kuwepo kwa vipaji vinavyozalishwa kuanzia shule za msingi na sekondari.

Katika UMITASHUMTA michezo inayoshindaniwa ni pamoja na mpira wa miguu kwa wasichana na wavulana, mpira wa miguu maalum kwa wavulana (wenye ulemavu wa kusikia) mpira wa pete, mpira wa goli kwa wasichana na wavulana wasioona na wenye uoni hafifu, mpira wa wavu kwa wasichana na wavulana, mpira wa mikono kwa wasichana na wavulana, mpira wa meza kwa wasichana na wavulana, riadha jumuishi, kwaya na ngoma.

Kwa upande wa UMISSETA michezo inayochezwa ni yote ya UMITASHUMTA pamoja na mchezo wa mpira wa kikapu kwa wasichana na wavulana isipokuwa mchezo wa mpira wa goli, pamoja na  mashindano ya usafi katika mazingira.Mashindano haya hupambwa na wasanii ili kutoa hamasa na burudani. Pia vyama vya michezo, mashirikisho na vilabu vya michezo mbalimbali hushiriki kuangalia vipaji mbalimbali.

Serikali inaangalia uwezekano wa kuwa na kanda za UMISSETA na UMISHUMTA kwa maana ya kuwa na kanda au mikoa itakayochaguliwa maalum na shule maalum zenye miundombinu ya michezo ili miundombinu ya kisasa iongezewe kwenye shule hizo.Hii itawafanya vijana waweze kucheza katika mazingira ya kiwango cha kimataifa ili wakienda kwenye mashindano ya kimataifa waone mazingira yanafanana na nyumbani hatimaye waendelee kufanya vizuri zaidi.

Mashindano haya huandaliwa na Wizara tatu zinazohusika na Elimu, Habari na TAMISEMI chini ya Kamati ya Uratibu ya Kitaifa ya Makatibu Wakuu wa Wizara hizo. Kupitia mashindano haya, wanafunzi wanapata fursa adhimu ya kujifunza uzalendo kupitia vilevile, vijana wanapata nafasi ya kuonesha na kujifunza tamaduni za Makabila ya Mikoa mbalimbali kupitia Ngoma ya Ndani ya Mkoa na Ngoma ya Nje ya Mkoa na vipaji binafsi huibuliwa Wizara inajukumu kubwa kama wasimamizi wa Sekta wa kuweka mfumo mzuri wa kuvuna vipaji na kuviingiza katika Soko la ajira katika Sekta ya Sanaa.

Mpangilio