Utumishi wa Umma na Utawala Bora

SIKU YA KIMATAIFA YA WAZEE

CHIMBUKO

Siku hii ilipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Kimataifa ya Mataifa kupitia Azimio na.45/106 la mwaka 1990. Azimio hili linzitaka nchi wanachama kuadhimisha Siku ya Wazee kila ifikapo tarehe 01, Oktoba ya kila mwaka.

Lengo la maadhimisho hayo ni kuongeza uelewa wa Jamii kuhusu masuala mbalimbali ya Wazee ikiwa ni pamoja na kutafakari fursa na changamoto zinzowakabili Wazee na namna ya kuzitatua. Kama Taifa siku hii imekuwa ikitumika kuwaenzi ipasavyo kwa kulinda, kuhifadhi, kukuza na kuimarisha upatikanaji wa haki zao katika Jamii

IDARA HUSIKA

 Idara ya Ustawi wa Jamii

Muhtasari

Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ina jukumu la kusimamia utekelezaji wa sera za Utawala wa Utumishi wa Umma, Serikali Mtandao, Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Mishahara, Usimamizi wa Mifumo ya Uendeshaji wa Serikali, Usimamizi wa Mifumo ya Utendaji Kazi Serikalini, Uendelezaji Rasilimaliwatu, Ukuzaji wa Maadili katika Utumishi wa Umma na Usimamizi wa Anuai za Jamii katika Utumishi wa Umma. Ofisi ya Rais pia ina dhamana ya kusimamia masuala ya Utawala Bora na Vilevile ina jukumu la kusimamia taasisi fungamanishi zinazoshiriki katika kuleta maendeleo na ustawi wa wananchi.
 

Lifahamu Gazeti la Serikali

1. Gazeti la Serikali ni kielelezo muhimu cha taarifa za Serikali, taasisi binafsi, wananchi na wadau mbalimbali zinazotumika katika utendaji wa kila siku. 


2.    Gazeti la Serikali lilianzishwa lini na kwa mujibu wa sheria ipi?
Gazeti la Serikali lilianzishwa kwa mujibu wa “General Orders” kifungu C.56- C.62 ya mwaka 1957 pamoja na marekebisho yake katika Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma Kifungu C.28-C.30 toleo la mwaka 1971, Kifungu C.28-C.31 toleo la mwaka 1994 na Kifungu C.27-C.30 toleo la mwaka 2009. Gazeti hili linategemewa katika kufanya maamuzi mbalimbali yakiwemo ya kisheria. 


3.    Nini lengo la kuanzishwa kwa Gazeti la Serikali?
Lengo la kuanzishwa kwa Gazeti la Serikali ni kuchapisha na kuhifadhi taarifa muhimu zitakazotumika kama marejeo katika kutatua migogoro au kufanya maamuzi muhimu kwani matangazo ya gazeti la Serikali yanapochapishwa huwa rasmi kwa utekelezaji hapa nchini. 


4.    Kuna umuhimu gani kwa Taasisi za Serikali kuwasilisha taarifa za kiutumishi ili zichapwe katika Gazeti la Serikali?

Kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma (Government Standing Orders) toleo la mwaka 2009 Kifungu C. 27 hadi C.30, ni muhimu kwa kila taasisi ya Serikali kuwasilisha taarifa mbalimbali za kiutumishi kwa ajili ya kutangazwa katika Gazeti la Serikali kwani hutumika kama marejeo katika kufanya maamuzi muhimu kwa mfano mtumishi akipoteza barua ya kuajiriwa (first appointment) huweza kutumia nakala ya Gazeti la Serikali lililochapisha taarifa zake kuthibitisha ajira yake.


5.    Ni taarifa zipi zinatakiwa kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali?
Taarifa za kiutumishi zinazopaswa kuchapishwa katika Gazeti la Serikali ni za;
•    Kuajiriwa na kukabidhiwa madaraka
•    Kuthibitishwa kazini
•    Kuacha kazi
•    Kufukuzwa kazi
•    Kustaafu na;
•    Tanzia


Ni taarifa zipi kutoka taasisi binafsi na wananchi zinazopaswa kuchapishwa katika Gazeti la Serikali? 
•    Kupotea kwa hati ya usimamizi wa ardhi 
•    Usimamizi wa Mirathi 
•    Mali iliyopotea (Loss report)
•    Kubadili jina (Deed poll)
•    Kufunga Kampuni 
Ni taarifa zipi kutoka katika taasisi za Serikali zinazotakiwa kuchapishwa katika Gazeti la Serikali?

•    Muundo wa Serikali na Majukumu ya Wizara
•    Sheria ndogondogo za halmashauri 
•    Uteuzi wa wajumbe wa baraza la ardhi 
•    Usajili wa vyama vya wafanyakazi 
•    Mali isiyo na mwenyewe na;
•    Kufutwa kwa kampuni

6.    Taarifa zinazotakiwa kuchapishwa katika Gazeti la Serikali zinawasilishwa wapi?

Matangazo yote ya Serikali pamoja na ya watu binafsi yanayotakiwa kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali huwasilishwa kwa Mhariri wa Gazeti la Serikali ambaye ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa ajili ya kuhaririwa. Mara baada ya matangazo hayo kuhaririwa huwasilishwa rasmi kwa Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali.

7.    Kuna gharama zozote zinatakiwa kulipwa pindi mdau anapotaka kuchapisha tangazo lake kwenye Gazeti la Serikali?
Hakuna gharama yoyote kwa matangazo yanayowasilishwa na Taasisi za Serikali kwa ajili ya kuchapishwa katika Gazeti la Serikali.
Kwa upande wa matangazo yanayowasilishwa na watu binafsi itawalazimu kulipa kiasi cha shilingi 20,000/= kwa Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kupitia namba ya malipo (Control Number) ili tangazo lake lipate uhalali wa kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali.


8.    Gazeti la Serikali huchapishwa siku gani?

Kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma toleo la mwaka 2009 Kifungu C. 27, Gazeti la Serikali linapaswa kuchapishwa kila Ijumaa ya wiki baada ya taarifa zinazowasilishwa na wadau kuhaririwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na kupelekwa kwa Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kila Jumanne ya wiki.


9.    Gazeti la Serikali linapatikana wapi pindi mdau anapolihitaji?

Gazeti la Serikali linapatikana kwenye Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali iliyopo eneo la Uhindini jijini Dodoma. Aidha, unaweza kulipata katika Maktaba ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa ajili ya rejea.


10.    Namna gani unapaswa kuwasilisha taarifa ili zichapishwe kwenye Gazeti la Serikali
Waajiri katika Taasisi za Umma wanatakiwa kuwasilisha taarifa za kiutumishi zinazopaswa kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali kwa njia ya nakala ngumu (hard copy) na nakala laini (soft copy). 
Aidha, taarifa zinazowasilishwa na watu binafsi kwa ajili ya kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali zinatakiwa kuwasilishwa kwa njia ya nakala ngumu (hard copy)
  
11.    Umuhimu wa Gazeti la Serikali
Gazeti la Serikali ni kielelezo muhimu kwa wadau mbalimbali hapa nchini katika utendaji kazi, hivyo ni vema waajiri na wananchi wakawasilisha taarifa zao muhimu ili ziweze kuchapishwa kwenye Gazeti ili zitumike kama marejeo katika utatuzi wa migogoro ikiwemo ya ardhi na kuwezesha kufanya maamuzi muhimu ya kiutendaji.

Mpangilio