Nishati

Dondoo za Bajeti 2022/2023

  • Shilingi Trilioni 1.44 fedha za ndani zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza kazi mbalimbali kwenye mradi wa umeme waJulius Nyerere (JNHPP);

 

  • Shilingi Milioni 500 zimetengwa ili kufanya kampeni kubwa ya kuhamasisha matumizi ya nishati bora ya kupikia pamoja na tafiti za kubaini nishati, mfumo sahihi na vivutio vya kusambaza nishati hiyo kwa maeneo ya vijijini;

 

  • Usambazaji Umeme vijijini kuongezwa kilomita mbili kwa kila kijiji tofauti na wigo wa sasa wa kilomita moja, ili kuwezesha wengi kupata umeme;

 

  • Shillingi Bilioni 10.00 mradi wa kupeleka na kusambaza gesi asilia katika makazi ya wananchi walio katika mkuza wa bomba kuu la gesi mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani. Mradi huu ambao ni wa kwanza nchini utakuwa wa majaribio;

 

  • Kuanza ujenzi wa mradi wa Kuzalisha Umeme Jua wa Shinyanga – MW 150 unaogharimu jumla ya Shilingi Bilioni 9.55;

 

  • Umeme kupelekwa kwenye vijiji 35 vilivyopo katika visiwa na maeneo yaliyombali na Gridi ya Taifa. Gharama ya mradi ni Tsh Bilioni 54.48;

 

  • Mradi wa kuwezesha ujenzi wa vituo vidogo vya kusambaza Bidhaa za petroli vijijini kwa njia ya mkopo nafuu. Mradi huu ni wa majaribio katika kutafuta mbinu bora zaidi za kusambaza nishati ya mafuta salama na kwa bei nafuu vijijini.

Uzalishaji Umeme Jotoardhi

Tanzania inategemewa kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 200 zinazotokana na Jotoardhi kabla ya mwaka 2025.Tanzania ina jumla ya maeneo 52 yanayoweza kutoa nishati ya Jotoardhi ambayo tayari yameshatambuliwa. Aidha, Serikali ina mpango wa kuongeza megawati 1100 zinazotokana na Nishati Jadidifu kabla ya mwaka 2025 na hizo megawati zitatokana na vyanzo mbalimbali kama vile Jotoardhi, Jua na Upepo.

Wizara ya Nishati inaweka nguvu kubwa katika kuendeleza vyanzo vya nishati ya Jotoardhi kwa sababu vyanzo hivyo haviishi. Kipindi cha ukame maji yanaweza kupungua, lakini Jotoardhi katika kipindi cha ukame au mvua, mvuke unaotoka chini ya ardhi uko palepale. Baadhi ya nchi kama Kenya ina zaidi ya megawati 1100 zinazotokana na Jotoardhi na Tanzania kutokana na eneo lake kubwa kupitiwa na Bonde la Ufa kuna uwezekano wa kupata umeme mwingi zaidi unaotokana na nishati hiyo.

Mkoa wa Mbeya katika eneo la Rungwe ni moja ya sehemu zilizoonekana kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kutoa nishati ya Jotoardhi kwa sababu tawi moja la Bonde la Ufa kuiingia katika eneo hilo na Tawi jingine kuelekea upande wa Malawi, eneo jingine ni la Kiejo-Mbaka ambalo linaweza kuzalisha megawati 60 zinazotokana na Jotoardhi na eneo la Ngozi, ambalo linategemewa kuwa litazalisha megawati 70 zinazotokana na Jotoardhi

Serikali imetoa takribani shilingi Bilioni 20 kwa ajili ya uendelezaji wa eneo hilo na wizara imenunua mtambo wa kuchoronga eneo hilo. Wataalam kutoka TGDC na Wahisani wameshirikiana katika kufanya tafiti zote zinazotakiwa katika kuhakikisha kuwa Tanzania inapata umeme kutoka kwenye nishati hiyo Jadidifu.

Nishati Jadidifu Kupunguza Uharibifu wa Mazingira

 

Nishati Jadidifu ni muhimu kwasababu inatoa mchango mkubwa katika kupunguza matumizi ya mkaa hasa katika maeneo ya mjini na vijijini lakini pia inasaidia kuimarisha afya za watu kwakuwa hewa itokanayo na moshi wa matumizi ya mkaa na kuni unamadhara kwa afya ya mtumiaji.

Wizara imejipanga kuhakikisha kuwa mwaka huu inazalisha megawati 150 kutoka kwenye vyanzo vya nishati jadidifu kwa maana ya jua na upepo na tayari Serikali imeanza kusaini mikataba na wawekezaji mbalimbali ili kuanza kutekeleza miradi hiyo.

Hivi karibuni Serikali ilizindua miradi miwili, mradi wa kwanza ukiwa ni ule unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya lakini unapewa fedha na UN unalenga kuhakikisha kunakuwa na matumizi machache ya kuni na mkaa katika maeneo ya majumbani, na mradi wa pili uliozinduliwa ni mradi unaolenga zaidi kwenye kilimo lakini kwa kutumia umeme jua. Miradi yote hii imelenga katika matumizi sahihi ya nishati jadidifu.

Mradi wa nishati mbadala uliojikita kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia,utaanza kutekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani,Morogoro, Dodoma na Mwanza ambapo imeelezwa kuwa katika majiji hayo mkaa unatumika kwa kiwango cha juu kulinganisha na mikoa mengine, ambapo mkoa wa Dar es salaam unaongoza kwa matumizi ya mkaa kwa asilimia 50 ya mkaa wote unaotumika nchini.

 

Mpangilio