Fedha na Mipango

Euro milioni 75 kusaidia utekelezaji wa mradi wa Usambazaji wa Majisafi Shinyanga

Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika lake la Maendeleo la Ufaransa (AFD) imesaini mkataba wa kuipatia Serikali ya Tanzania mkopo wa Euro milioni 75 sawa na takriban shilingi bilioni 195 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Usambazaji wa Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Mkoa wa Shinyanga.  Lengo kuu la mradi huo ni kutoa huduma za uhakika na endelevu za upatikanaji wa majisafi na usafi wa mazingira katika Manispaa ya Shinyanga.
 
Mradi huo utaboresha afya, ustawi wa jamii na hali za maisha ya wanufaika wa mradi huo kwa kuboresha na kuimarisha miundombinu iliyopo na kuongeza ufanisi wa uendeshaji na utoaji wa huduma bora kupitia Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA).  Hii ni ajenda kubwa  inayoendana na hatua za Serikali, kupitia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano unaotoa vipaumbele pamoja kuboresha upatikanaji na usambazaji wa Maji na huduma za usafi wa mazingira mijini na vijijini na utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira.


Mradi utaongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa asilimia 95 katika Manispaa ya Shinyanga na baadhi ya miji midogo katika Wilaya ya Shinyanga na itawanufaisha wananchi zaidi ya 306,566 ambao hivi sasa wanapata maji kwa wastani wa asilimia 60. .Aidha, moja ya vigezo vya Mpango huo ni kuongeza asilimia ya watu wa mijini wanaopata huduma ya maji safi 
 
Uzalishaji wa maji utaongezeka  kutoka mita za ujazo za sasa ambazo ni 25,877 kwa siku, hadi 33,944; na kuongeza nafasi za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja katika maeneo yanayozunguka mradi. 
 
Taasisi zitakazotekeleza mradi huo (Wizara ya Maji na SHUWASA) chini ya uongozi wa Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Sanga, wanatakiwa kutuma uzoefu uliopatikana katika utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa Sekta ya Maji Tanzania, Programu ya huduma endelevu za Maji na usafi wa Mazingira vijijini na  miradi mbalimbali ya maji na usafi wa mazingira iliyofadhiliwa na AFD ili kutoa huduma nzuri kwa ajili ya wananchi wa Shinyanga na nchini kwa ujumla.
 
Serikali itaendelea kuimarisha uhusiano wa kimaendeleo kwa faida ya wananchi wananchi na kuchukua hatua zote muhimu kuhakikisha kwamba mradi unatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati. 
 
Katika kipindi cha miezi mitano tu iliyopita kuanzia mwezi Februali, Ufaransa imeipatia Tanzania Euro milioni 330 kiasi ambacho ni kikubwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo hapa nchini.Nchi ya Tanzania na Ufaransa zina urafiki ambao umekuwa ukikuwa kama inavyojidhihirisha katika miradi ya kimaendeleo inayofadhili . Serikali ya Ufaransa itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta tatu ambazo ni Maji na Usafi wa Mazingira, Nishati na Usafirishaji na Uchukuzi.
 
Tangu mwaka 2014 Serikali ya Ufaransa imewekeza zaidi ya euro bilioni 1 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo duniani kote ikiwa ni jitihada ya nchi hiyo kuziwezesha nchi zinazoendelea kuondokana na uhaba wa maji na uharibu wa mazingira.
 
Kukamilika kwa mradi huu kutawezesha maji kufikia asilimia 95 au Zaidi ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambayo imeelekeza kufikia mwaka 2025 huduma ya maji mijini ifikie asilimia 95 na maji vijijini ifikie asilimia 85.
 

Dondoo za Bajeti 2022/2023

Serikali ya Tanzania imewasilisha bungeni bajeti yake kuu kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo jumla ya shilingi trilioni 41.48 zinatarajiwa kutumika. Bajeti ya mwaka 2022/23 inalenga kuongeza Kasi ya Kufufua Uchumi na Kuimarisha Sekta za Uzalishaji kwa ajili ya Kuboresha Maisha. Katika utekelezaji wa dhima hiyo kwa mwaka 2022/23 bajeti imeelekeza kipaumbele katika sekta za uzalishaji zikiwemo Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Nishati, Uwekezaji na Biashara. Lengo la Serikali ni kujenga uchumi, kukabiliana na umasikini pamoja na ukosefu wa ajira hasa kwa vijana. 

  • Katika mwaka wa Fedha 2021/2022 Serikali ilitarajia kukusanya jumla ya shilingi trilioni 37.99 kutoka katika vyanzo vyote vya ndani na nje ambapo hadi Aprili 2022, kiasi cha shilingi trilioni 29.84 kilikusanywa;

 

  •  Hadi April 2022 Deni la Serikali lilikuwa shilingi trilioni 69.44, sawa na ongezeko la asilimia 14.4 ikilinganishwa na shilingi trilioni 60.72 Aprili 2021. Kati ya kiasi hicho, deni la ndani ni shilingi trilioni 22.37, sawa na asilimia 32.2 na deni la nje ni shilingi trilioni 47.07, sawa na asilimia 67.8;

 

  • Misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo inatarajiwa kuwa shilingi trilioni 4.65, sawa na asilimia 11.2 ya bajeti yote;

 

  • Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 5.78 kutoka soko la ndani ambapo shilingi trilioni 3.30 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na Shilingi trilioni 2.48 ni kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo;

 

  • Kiasi kitakachokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania yanakadiriwa kuwa shilingi trilioni 23.65 na mapato yasiyo ya kodi kutoka wizara, Idara, Taasisi na Mamlaka za Serikali za Mitaa yanakadiriwa kuwa shilingi trilioni 4.37;

 

  • Bajeti ya Kilimo inatarajiwa kuongezeka kutoka shilingi billion 294 hadi shilingi bilioni 954. Ongezeko hilo la bajeti linalenga kuimarisha sekta ya mifugo ili ufugaji uwe wa
    kisasa zaidi na wenye tija (modernization).
Mpangilio